1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 60 ya kuasisiwa UNHCR

Saumu Ramadhani Yusuf14 Desemba 2010

Shirika hilo linaiomba Jamii ya Kimataifa isichoke kuwasaidia wakimbizi na kuwapa hifadhi

https://p.dw.com/p/QXjG
Antonio Guterres,Kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCRPicha: picture-alliance/ dpa

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi linaadhimisha miaka 60 tangu kuzinduliwa rasmi.Maadhimisho hayo yanafanyika wakati ambapo bado suala  la wakimbizi linautatiza ulimwengu mzima pamoja na kuwa na watu wasiokuwa na uraia.Moja ya mataifa yanayokabiliwa na vita na ghasia ni Somalia iliyo jirani ya Kenya na wakimbizi wanaotokea huko huikimbilia.

Siku hii inaadhimishwa kote ulimwenguni kukiwa na changamoto nyingi zinazowakabili wakimbizi na wahudumu.Akizungumza katika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi,UNHCR,Mkurugenzi mkuu Antonio Guterres aliitolea wito jamii ya kimataifa kuziimarisha juhudi zake na mchango ili kupambana na tatizo la wakimbizi.Bwana Guterres alitahadharisha kuwa kuna vyanzo vipya vinavyosababisha watu kuyakimbia mataifa yao.Kiongozi huyo alilielezea pia tatizo la Somalia ambako bado vita vinaendelea na kuwafanya wengi kutorokea nchi jirani ya Kenya.'Shirika la UNHCR lina kitengo maalum nchini Kenya kinachowahudumia wakimbizi wa Somalia.Wengi wao wanaishi katika kambi zilizoko kaskazini mwa Kenya na hali kwa kweli ni mbaya.Kuna uhaba wa maji safi ya matumizi na kambi hizo zina uwezo wa kuwahudumia kiasi ya thuluthi moja tu ya wakimbizi wote wanaohifadhiwa hapo.   

Straßenkämpfe in Mogadischu
Vita vinavyoendelea nchini Somalia vinasababisha watu chungunzima kuitoroka nchi hiyoPicha: AP

Kiasi ya wakimbizi milioni 1.5 wameachwa bila makazi Somalia kwenyewe na laki tatu wengine wamekimbilia nchi jirani ya Kenya na wanahifadhiwa katika kambi za Dadaab na Kakuma. Hivi karibuni taarifa zilieleza kuwa baadhi ya wakimbizi wa Somalia walioko Kenya wanalazimishwa kurejea walikotokea.Roberta Russo wa kitengo cha Somalia katika shirika la UNHCR ameiomba Kenya kujaribu kuwaruhusu wakimbizi wa Somalia kuingia nchini humo pamoja na kwamba kuna kitisho cha magaidi wanaosadikiwa mara nyingi wanatokea Somalia na kuingia Kenya kwa jina la Ukimbizi. Aidha UHCR imeitolea mwito  jamii ya kimataifa kuwapa hifadhi wakimbizi wa Somalia wanaovikimbia vita. Inaeleweka kuwa serikali ya Kenya inajitahidi kuwa chonjo zaidi kwasababu za kiusalama ukizingatia kitisho cha ugaidi.

Flüchtlinge in Somalia
Wakimbizi wa Somalia nchini Kenya eneo la ManderaPicha: AP

Ili kujaribu kupambana na hali hiyo,Umoja wa Mataifa umetolea wito jamii ya kimataifa kuchangia kiasi ya dola milioni 530 zitakazotumika kuifadhili misaada ya wakimbizi wa Somalia.

Zaidi ya wakimbizi laki nne wa Somalia wamelikimbilia eneo la Afgooye lililoko karibu na mji mkuu wa Somalia wa Mogadishu. Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa idadi hiyo ni kubwa zaidi ulimwenguni ya watu walioachwa bila makazi nchini mwao. 

Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-UNHCR website/DPAE

Mhariri:Yusuf Saumu Ramadhan