1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka mitano tangu kuundwa Umoja wa Afrika, AU.

9 Julai 2007

Mkutano wa kilele wa wa Umoja wa Afrika, AU, uliofanyika katika mji mkuu wa Ghana, Accra, wiki iliopita ulikuwa mchangamfu sana kushinda mikusanyiko yeyote ya aina hiyo ya wakuu wa nchi na serekali za Kiafrika.

https://p.dw.com/p/CHBI
Mwenyekiti wa Komisheni ya Umoja wa Afrika, AU, Alpha Oumar Konare.
Mwenyekiti wa Komisheni ya Umoja wa Afrika, AU, Alpha Oumar Konare.Picha: AP

Hadi usiku wa manani wakuu hao walijadiliana juu ya namna siku za mbele wawe na jumuiya za kiuchumi za kimkoa zilizo na nguvu au kuwa na Umoja wa dola za Afrika, kwa kimombo USA, kama vile ilivyo Marekani hivi sasa.

Jumuiya ya AU ilianzishwa katika mkutano uliofanyika July 8 hadi 10 mjini Durban, Afrika Kusini, ikichukuwa nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU. Jumuiya ya sasa ndani yake mna nchi zote za Afrika isipokuwa Moroko. Uwanachama wa Madagascar ulisimamishwa July 2003, na Mauritania, kutokana na mapinduzi ya kijeshi yaliotokea nchini humo hapo Agosti 5, 2005, ilitolewa kwenye jumuiya hiyo kwa muda.

Mwanzoni, hisia za kutaka kuwa na umoja wa Afrika wenye sura kama ile ya Umoja wa Ulaya wa hivi sasa zilizuka katika mkutano maalum wa kilele wa OAU ulioitishwa na na Rais Muammar Ghaddafi wa Libya.

Aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya kigeni wa Kenya, Kalonzi Musyoke, anasema hivi kuhusu kile kilichopelekea kuundwa AU:

Licha ya haja iliotambuliwa kuwa na mfumo wa kidemokrasia, kulindwe haki za binadamu, kuletwe umoja wa Afrika, itanzuliwe kwa pamoja mizozo na kubeba dhamana ya kupinga vita, hati ya umoja huo ilipewa kibali cha mwisho na nchi za OAU hapo Mei 2001, baada ya zaidi ya nchi 36 kuidhinisha. Hapo tena OAU ikabadilika kuwa AU na kikafuata kipindi cha mpito cha miaka miwili ambapo jumuiya zote mbili ziliishi ubavu kwa ubavu ili kuiwezesha OAU ijibadili kuwa AU. Makao makuu ya Umoja huo yako Addisababa, japokuwa Libya ilijitahidi kutaka yahamishiwe Sirte, mahala alipozaliwa kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Ghaddafi.

Jee AU ilianzishwa kwa vile malengo ya OAU yalishindwa kufikiwa, kama vile waasisi wake katika miaka ya sitini walivowaza? Waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Kenya, Kalonzi Musyoke, anajibu hivi:

Taasisi muhimu ya AU ni mkusanyiko wa wakuu wa nchi na serekali na maamuzi hupitishwa kwa wingi wa thuluthi mbili za kura; ni chombo hicho kinachoshughulikia kutekelezwa maazimio yaliofikiwa, na kila mwaka humchagua mmoja wao kuwa kiongozi wa AU. Mara mbili kwa mwaka hukutana baraza tendaji la umoja huo; wanachama wake ni mawaziri wa mambo ya kigeni.

Bunge la Afrika, likiwa na makao yake mjini Addis ababa, lilianzishwa Machi 2004, likiwa na kazi ya ushauri tu, kila bunge la nchi mwanachama linapeleka watu watano. Hatua ya mwanzo ya kuelekea njia ya kuwa na Umoja wa dola za Afrika, USA, lazima iwe kulipa bunge hilo uwezo wa kutunga sheria.

Tangu mwaka 2003, kiongozi wa komisheni ya AU ni aliyekuwa rais wa Mali, Alpha Oumar Konare. Ndani ya komisheni hiyo kuna baraza la Usalama la AU lenye watu 15, na ambalo linafanya kazi na lina haki ya kujiingiza ili kuzuwia mizozo na mafarakano, uhalifu dhidi ya binadamu, uhalifu wa kivita na mauaji ya kiholela.

Ujiingizaji wa mwanzo katika nchi mwanachama ulikuwa mwezi Mei, mwaka 2003 pale wanajeshi wa Afrika Kusini, Ethiopia na Msumbiji walipelekwa Burundi. Na katika kutekeleza mapatano ya kusitisha mapigano katika mkoa wa Darfur wa Sudan ulio na mzozo, AU ilituma wanajeshi 7000 waliopewa jukumu la kuhakikisha kuna amani na wakimbizi wanalindwa. Lakini majeshi hayo yamekubaliwa na matataizo ya kutimiza majukumu yao kwa vile hayana vifaa vya kutosha, kama vile mafuta na ndege za uchunguzi. Mwezi Juni, serekali ya Sudan ilikubali rasmi kuweko jeshi la AU na la Umoja wa Mataifa katika eneo hilo la Darfur.

Huko Somalia, AU hivi sasa ina wanajeshi 1500 katika nchi hiyo, lakini lile lengo la kuweko huko wanajeshi 8000 halijafikiwa. Hiyo inaonesha kwamba ile fikra ya kuyatanzua matatizo ya Kiafrika kupitia suluhisho la Kiafrika inabaki kuwa ni ndoto tu.

Tangu kuanzishwa, AU imefanya maendeleo kuelekea mafungamano ya kiuchumi, kama vile kuweko jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, na ile ya Afrika Magharibi, ECOWAS. Ule mpango wa maendeleo wa Afrika, NEPAD, au kwa jina lengine ushirikiano kwa maendeleo ya Afrika, hadi sasa haujaleta yale matarajio yaliowekewa.

Pindi juhudi za Muammar Ghaddafi na viongozi wengine wa nchi za Afrika Magharibi kutaka kuwa na serekali moja kwa Afrika nzima yatafanikiwa, basi jambo hilo huenda likajengeka juu ya msingi wa sasa wa AU. Lakini waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Kenya, Kalonzi Musyoke, anahoji juu ya kujenga tufali moja juu ya jengine, hatua kwa hatua:

Hapo tena kutakuja taasisi nyingine kama vile benki moja kuu na mahakama kuu kwa Afrika nzima. Tatizo liko katika kuziweka nchi hizo mbali mbali chini kivuli kimoja, ukiangalia matatizo ya lugha mbali zinazotumika katika Afrika. Kwa miaka kumezungumziwa kwamba lugha ya Kiswahili inayozungumzwa sana katika Afrika Mashariki na ya Kati iwe lugha ya kazi ya AU; hivyo kuachana mwishoni na mabaki ya kikoloni. Lakini hadi sasa ni maendeleo madogo mno yaliopatikana katika suala hilo. Katika vikao vya jumuiya hiyo bado lugha za madola ya zamani ya kiloni ndizo zinazozungumzwa.

Bila ya kujali jina gani Waafrika wanaupa Umoja wa nchi zao, njia ya kuufikia umoja kama ule wa Ulaya au wa Shirikisho la Marekani, USA, ni ndefu mno, na jambo hilo limedhihirika katika mkutano wa kielele wa wiki iliopita mjini Accra, Ghana, kama anavosema Hamida Maalim, mhadhiri wa Chuo Kikuu katika nchi hiyo aliyeyafuatiliza majadiliano katika mkutano huo: