1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo: Ligi kuu ya vilabu bingwa vya Ulaya Jumatano.

Mohammed AbdulRahman23 Oktoba 2007

Michuano inaendelea leo Jumatano katika viwanja mbali mbali

https://p.dw.com/p/C7nD
Nembo ya mashindano ya ligi ya vilabu bingwa vya Ulaya.
Nembo ya mashindano ya ligi ya vilabu bingwa vya Ulaya.Picha: AP GraphicsBank

Miongoni mwa michuano hiyo ni Real Madrid ya Uhisapania inayomenyana na Olimpiakos ya Ugiriki imo katika shinikizo la kusaka ushindi jioni ya leo kwa udi na ambari: Kibarua Kigumu kinamuandama kocha Bernd Schuster mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani aliyewahi kulisakata gozi katika kilabu hiyo akiimudu vilivyo enzi hizo nafasi ya kiungo. Schuster amechukua mamlaka tangu alipoachishwa kazi Mtaliani Fabio Capello na ameahidi kurudisha heshima kwa kuleta ushindi na soka la kuwavutia mashabiki.Schuster anakabiliwa na majeruhi wakiwemo Gabriel Heinze anayecheza nafasi ya ulinzi, mchezaji wa pembeni Arjen Robben na mchezaji wa kiungo Mahmadou Diarra anayesumbuliwa na goti.

AC Milan ya Itali nayo itakua bila ya mlinda mlango wake Mbrazil Dida wakati itakapochuana na Shakhtar Donetsk ya Ukraine, lakini nahodha Paolo maldini anatarajiwa kurudi uwanja hii leo. Maldini alishiriki katika fainali yake ya nane ya kombe la ulaya mwezi Mei, alicheza mechi ya kwanza msimu huu pale Milan ilipojikuta ikilala uwanja wa nyumbani mbele ya Empoli bao 1-0 . AC Milan inatajwa na wachambuzi wa kandanda kuwa haitokua na kazi rahisi mbele ya Waukrain ambao walishailaza Celtic ya Scotland nyumbani na kushinda pia mchezo wa kwanza dhidi ya Benfica ya Ureno nyumbani kwao Lisbon.Shakhtar inafundishwa na Mrumania Mircea Lucescu aliyewahi kuwa kocha wa mahasimu wa AC Milan Inter Milan katika msimu wa 1998/99.

Liverpool ya England inarudi Istanbul mji walikonyakua ushindi wa tano wa kombe la ulaya miaka miwili iliopita pale ilipokua nyuma mabao 3-0 mbele ya AC Milan kabla ya kuzusha maajabu na hatimae kuitoa Milan katika mikwaju ya Penalty. Leo wataumana na Besiktas ya Uturuki. Liverpool hadi sasa ina pointi moja kutokana na michezo miwili.Kikosi cha Liverpool The Reds kama wanavyoitwa na mashabiki wao, kinatarajiwa kuwa na nahodha Steven Gerrard baada ya kukosana na kocha wake Benitez kutoka Uhispia na kumuondoa katika mchezo wa ligi wiki iliopita dhidi ya Everton. Benitez aliuambia mtandao wa kilabu hiyo kuwa sasa hakuna tatizo lolite kati yake na Gerrad.

Kwa upande mwengine Chelsea iliokua na mgogoro baada ya kuondoka kocha wake maarufu Jose Morinho na sasa ikiwa na mwalimu mpya Muisraili Avram Grant inaikaribisha Schalke O4 ya Ujerumani .

Celtic Glasgow ya Scotland inakibarua kigumu pia leo wakati itakapotoana jasho na Benefica ya mjini Lisbon . Celtic bado haikushinda mchezo wowote ugenini katika mashindano hayo na kwa jumla imetoka sare moja na kufungwa mara 13 ikiwa ni pamoja na kipigo cha mabao 3-0 mbele ya Wareno hao Novemba mwaka jana. Kwa Benefica ushindi ni muhimu kuweka matumaini ya kusonga mbele baada ya kufungwa na AC Milan na Shaktar Donetsk ya Ukraine katika mechi zilizotangulia. Benfica ina kocha mpya Jose Antonio Camacho wa Uhispania aliyechukua nafasi ya Fernando Santos baada ya mechi moja tu ligi ya msimu mpya.

Kwa jumla mashabiki wa soka barani ulaya na kwengineko, wanatega masikio na kukodolea macho televisheni zao, kwa michuano hiyo ya champions league-ligi ya vilabu bingwa vya ulaya leo jioni.