1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo-mwishoni mwa wiki

Ramadhan Ali5 Oktoba 2007

Tukifungua pazia,nusu-finali ya kombe la klabu bingwa barani Afrika uwanjani.Bundesliga na premier League zinatamba na ni robo-finali ya kombe la dunia la rugby.

https://p.dw.com/p/C7nb

Mwishoni mwa wiki hii,duru ya pili ya nusu-finali ya kombe la klabu bingwa barani Afrika-champions League, yarudi uwanjani leo Etoile Sahel ya Tunisia ikiwa nyumbani Souse kucheza na mahasimu wao Al Hilal ya Sudan.Mabingwa al Ahly ya Misri, watateremka kesho uwanjani kupambana na Al-Ittihad ya Libya na kukata tiketi yao nyengine ya finali.

Bundesliga na Premier League pia ziko uwanjani lakini pia kombe la dunia la rugby linaingia nalo hatua ya robo-finali kwa Spring Boks -Afrika kusini wakiwa na miadi na Fiji.

Mabingwa wa Afrika Al Ahly na Etoile du sahel ya Tunisia, yaonesha wanajiwinda kukutana tena kwa mara ya pili mnamo miaka 3 kwa finali ya kombe hili la klabu bingwa.Al Ahly yatumai kuwa timu ya kwanza ya Afrika kulinyanyua Kombe kwa mara ya 6 na kulitetea taji mara mbili.Ni wao wanaopigiwa upatu na kuhanikiza kubakia na kombe mradi tu kesho watamba mbele ya jirani zao walibya-Al Ittihad.jumapili iliopita,Al Ahly ilimudu sare ya 0:0 mjini Tripoli na kesho wanacheza nyumbani.

Etoile pia wako nyumbani huko seousse na wameshinda kila kombe la Afrika isipokua champions League-kombe hili.Etoile ina nafasi nzuri leo ya kukata tiketi ya finali kwavile iliondoka na bao 1 kikapuni ilipolazwa 2:1 na Al Hilal,huko Sudan.

Mwishoni mwa wiki hii pia kuna changamoto ya kombe la shirikisho la dimba la Afrika:CS Sfaxien ya Tunisia na Al-Merreikh ya Sudan zinaania pia kucheza finali ya kombe hilo.

Sfaxien inabidi kuizima mamelodi Sundowns ya Afrika kusini mjini Pretoria kuhakikisha inacheza kwa mara ya pili finali ya kombe hili la Afrika mnamo muda wa mwaka baada ya kulazwa na Al Ahly katika finali ya klabu bingwa mwaka jana.Ikiwa si hivyo, TP Mazembe inavizia ,mradi ilete ushindi Lumbubashi kwa kuilaza Astres Douala ya Kamerun.

Huku Ulaya,Bundesliga-ligi ya Ujerumani na Premier League –Ligi ya uingereza zitatupa msisimko mwengine mwishoni mwa wiki hii:

Karlsruhe iliopanda daraja ya kwanza msimu huu wana nafasi nzuri ya kutobanduka kileleni mwa ligi ikiwa watatamba mbele ya Schalke inashika nafasi ya pili.Karslruhe imeanza uzuri ikiwa na jumla ya pointi 15.

Viongozi wa ligi Bayern munich wana nafasi ya kubakia juu kileleni wqanapocheza kesho na mahasimu wao wa kusini Nüremberg.Munich lakini, haichezi na kipa wake Oliver Kahn alieumia wala mshambulizi wake Miroslav Klose.

Mabingwa Stuttgart wanakutana na hannover na watahitaji pointi 3 na hasa kwavile wako nyumbani.Hertha Berlin baada ya kujiweka nafasi 3 za kwanza kileleni,sasa imeregeza kamba na kuangukia safu ya 9.Mahasimu wao ni Energie Cottbus.Werder Bremen inacheza na Duisburg wakati hamburg inaumana na Bielefeld.Bayer Leverkusen itakamilisha duru ya mwishoni mwa wiki hii ikicheza na Frankfurt.

Katika Premier League-Ligi ya Uingereza,kuumia kwa wachezaji kadhaa katika ngome ya mabingwa Manchester United, kunaipa wasi wasi timu hii katika kampeni ya kutetea taji lao.Si chini ya wachezaji 6 si fit kucheza.Manchester inaikaribisha Wigan Athletic jioni ya leo.

Kombe la dunia la rugby likendelea nchini Ufaransa,Springboks-Afrika kusini, wana miadi na Fiji mwishoni mwa wiki hii katika hatua ya robo-finali.Uingereza ndio mabingwa wanaotetea taji lao.