1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo wiki hii

11 Julai 2008

Kinyan'ganyiro cha kombe la Afrika mashariki na kati kinaanza jumamosi hii Dar-es-salaam.

https://p.dw.com/p/Eae5

Jumamosi hii firimbi italia mjini Dar-es-salaam ,kuanzisha kinyan'ganyiro cha kombe la klabu bingwa -kanda ya Afrika mashariki na kati.Tanzania, wenyeji ,

wanaingia na timu 3-moja ikitoka visiwani Zanzibar-Miembeni.Nyengine mbili Simba na Young Africans.Simba inafungua dimba na tusker ya Kenya.

Uwanja wa Durban, utakaochezewa kombe la dunia 2010 huko Afrika kusini, utamaliza ujenzi wake mapema kuliko ilivyopangwa.

Kocha mpya wa Mexico -zamani England -Sven Goran-Eriksson, adai Mexico ni wajibu kukata tiketi kwa kombe hilo lijalo la dunia.

Na Mahkama ya spoti mjini Lausanne,Uswisi, itasikiliza keshokutwa jumatatu-rufaa iliokatwa na klabu 2 za Ureno: Benefica Lisbon na Vitoria Guimaraes.

►◄

Firimbi italia leo mjini Dar-es-salaam na Morogoro kuanzisha changamoto ya kombe hilo .Kwa mara nyengine tena kombe hili linafanyika Tanzania na inatia timu 3 : Simba na Young Africans na Miembeni kutoka Zanzibar.

Lakini wingi wa timu si dhamana kuwa kombe litabakia Tanzania,kwani wartwanda -mabingwa wapanga kuridi nalo.

Mbali na Dar-es-salaam, mechi nyengine zinachezwa Morogoro,kuanzia jumatatu.

Uwanja wa Mandela Bay huko Port Elizabeth,Afrika Kusini ulitolewa wiki hii katika orodha ya viwanja vitakavyoandaa kombe la mashirikisho-Confederations Cup-kombe linalofungua pazia mwaka mmoja kabla kuanza kombe la dunia.

Kuepuka hatima kama hiyo, uwanja wa mji wa Durban:King Senzangakhona Stadium,utakaochezewa nusu-finali za kombe la dunia 2010,umetangaza utamaliza ujenzi hata mapema zaidi ya wakati uliowekwa. Kwani, unadai uko wiki 8 mbele ya maandalio.

Taarifa hii pia inakaribishwa mikono 2 na kamati ya maandalio ya kombe la dunia ya Afrika Kusini kutokana na mkasa wa uwanja wa Mandela Bay huko Port Elizabeth.

Pia Rais wa shirikisho la dimba ulimwenguni-FIFA-Sepp Blatter alitangaza wiki hii kwamba, amezungumza na nchi nyengine 3 juu ya kuwa tayari kuandaa kombe hilo la dunia-la kwanza barani Afrika endapo Afrika Kusini itashindwa.

Afrika kusini itadai maelezo kwanini rais wa FIFA ametoa matamshi hayo.

Msemaji wa FIFa mjini Johannesberg,Bibi Delia Fischer, hakuyatia mno maanani matamshi ya Blatter,akidai kuwa Afrika kusini itapokonywa tu jukumu la kuandaa pindi pakizuka msiba wa kimaumbile.

Jarome Valcke,katibu mkuu wa FIFA alizuru Afrika kusini wiki hii.

Tukisalia na mada hii ya kombe lijalo la dunia, Mexico chini ya kocha wake mpya Goran-Eriksson, zamani kocha wa Uingereza, inahisi kushiriki katika kombe lijalo la dunia 2010 ni wajibu wake.Mechi ya kwanza ya mexico chini ya Eriksson itakua na hondurus mwezi ujao.

Mexico mbali na Hondurus, inacheza pia Kanada na jamaica katika duru ya kwanza ya kuania tiketi za kombe hilo la dunia-mapambano ambayo yatachezwa kati ya August na Novemba. Timu 2 za usoni zinaingia duru ya mwisho ya kanda ya CONCACAF itakayojumuisha timu 6 hapo mwakani.

Kuteuliwa kwa mswede huyo-kocha wa zamani wa Uingereza,kulizusha balaa nchini Mexico.Wakosoaji walidai Eriksson,hana wakati kuwajua wachezaji bora wa Mexico na hatafahamu masharti ya m chezo wa timu hiyo.

CHAMPIONS LEAGUE:

Mahkama ya Upatanishi ya michezo huko Lausanne,Uswisi,keshokutwa jumatatu itasikiliza rufaa iliokatwa na klabu 2 za ureno-Benefica Lisbon na vitoria Guimaraes .Klabu hizo 2 zimepeleka malalamiko zikitaka mabingwa wa ureno FC Porto wamepigwe kumbo nje ya kombe la klabu bingwa barani Ulaya msimu ujao-champions League-mashindano manono kwa fedha.

Mawakili 3 watasikiliza kesi hiyo na watazamiwa siku moja baadae hapo jumaane kutoa hukumu yao.

Benefica na Guimaraes wanabisha uamuzi wa UEFA-shirikisho la dimba la ulaya linaloandaa kombe la champions league- kubadilisha marufuku yake kwa Porto kutokana na kashfa ya kulishia mrungura.Kikao cha jumatatu cha mahkama kitajishughulisha kuamua iwapo UEFA ina mamlaka ya kujishughulisha na kesi ya Porto wakati uchunguzi na rufaa juu ya mkasa huu ukiendelea nchini Ureno.

Kaka, stadi wa Brazil aliechaguliwa mwanasoka bora wa mwaka wa dunia mwakajana na anaeichezea AC Milan amesema yungali anahisi maumivu kufuatia opresheni ya goti lake.Hatahivyo, Kaka yuko njiani kupata nafuu kujiunga na klabu yake ya AC Milan kabla kuanza msimu mpya.

Kaka asema atakuwa fit hadi julai 16 pale Milan itakapoanza mazowezi kwa kujiandaa kwa msimu mpya.

Chipukizi wa kiungo wa Ufaransa, Samir Nasri amekubali kujiunga na Arsenal london kutoka klabu yake ya Olympique Marseille.

Arsenal haikutoa taarifa za kutosha za mkataba wake, mbali na kusema chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 21 atafunga mkataba wa muda mrefu kwa kitita kisichofichuliwa.

Nasri atakaejiunga na kikosi cha Arsenal kwa mazowezi hapo Julai 21,aliichezea timu ya Taifa ya Ufaransa mara 2 katika kombe la ulaya la mwezi uliopita lililomalizikia ushindi wa Spain.