1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo wiki hii

17 Oktoba 2008

Nusu-finali ya Klabu bingwa barani Afrika:Al Ahly na Enyimba uwanjani.

https://p.dw.com/p/FcAK
Hamburg SV (Jazi buluu)Picha: picture-alliance /dpa

Jumamosi hii ni nusu-finali ya kombe la klabu bingwa barani Afrika mjini Cairo ,Misri na Garoua,Kamerun baina ya Al Ahly na Enyimba na Dyanamo ya Zimbabwe na Contonsport ya Kamerun.

Rais wa UEFA-shirikisho la dimba la Ulaya na nahodha wa zamani wa Ufaransa Michel Platini, asema uamuzi wa rais wa Ufaransa wakuvunja mechi yoyote ya mpira endapo wimbo wa Taifa ukizomewa ni "upumbavu".

Maandalio ya Kombe la dunia 2010 nchini Afrika Kusini yamefikia wapi baada ya timu kadhaa za Afrika kuania tiketi zao mwishoni mwa wiki iliopita ?

Baada ya Al Ahly na Enyimba kuondoka suluhu 0:0 katika duru ya kwanza ya nusu-finali hii huko Aba,Nigeria, Enyimba inaahidi mara hii kuipokonya Al Ahly tiketi yake ya ubingwa wake wa 6 wa kombe la klabu bingwa barani Afrika.kufanya hivyo si rahisi, kwani Al Ahly ,wanacheza nyumbani na ni vigumu ikawaachia wanigeria tiketi ya finali ya kutwaa taji lao la 6 la kombe hili la Afrika.

Enyimba itatosheka tu kutoka sare na kutegemea bao la ugenini kuwachukua katika finali ya kombe hili.

Kuzuwia sare nyengine, Al Ahly watabidi kuhujumu lango la wanigeria na wakati huo huo kutia nta ngome yao isivuje.Mashabiki wa Al Ahly, waamini kwamba kombe la 6 la klabu bingwa liko njiani kurudi Cairo na wamepania leo kuishangiria timu yao hadi firimbi ya mwisho kulia.Hatahivyo, ngome ya Enyimba ina ufa na Al Ahly haitaachia kila nafasi kuutumia ufa huo.Mastadi wake akina Mohamed Aboutraika na Ahmed Hassan na mzaliwa wa Angola Flavio Amado hawatachoka kupiga hodi katika lango la Enyimba leo hadi kuitikiwa .

Enyimba inatapia ushindi wake wa kwanza dhidi ya Al Ahly tangu kuzabwa bao 1:0 nyumbani na 2-1 ugenini na Al Ahly katika kinyanganyiro cha kombe hili 2005.

Sitapenda kuagua nani mwishoe atatoroka na tiketi ya finali kutoka Cairo jioni hii.

Katika changamoto ya pili, nathubutu kusema Contonsport Garoua,hawatawaachia wazimbabwe Dynamo kurudi Harare na tiketi ya finali.kama wenzao Canon Yaounde waliotwaa ubingwa 1980,Contonsport wameahidi kunguruma kama simba porini Garoua.Dynamo kwahivyo, haina kibarua rahisi jioni hii. Lakini, Contonsport wasishangirie na mapema, kwani timu nyingi maarufu za Afrika ziligundua ni vigumu kufua dafu mbele ya Dynamo .Waulize watunisia Etoile du Sahel mjini Sousse huko kwao walikiona nini ? Waulize ASEC Abidjan Waivory Coast kilichowafika ?

KOMBE LA DUNIA 2010 AFRIKA KUSINI:

Maandalio ya Kombe la dunia la kwanza barani Afrika nchini Afrika Kusini yamefikia hatua gani ? Je, shaka shaka zilizotolewa kuwa pengine mashindano hayo yatabidi kuandaliwa nchi nyengine zimetoweka kabisa ?

Wiki iliopita, serikali ya rais mpya wa Afrika kusini iliwatimua nje ya Kamati ya Maandalio ya Kombe la dunia wajumbe wote 3 waliowakilisha serikali ndani ya Kamati hiyo na ambao walikuwa watiifu kwa rais Thabo Mbeki aliejiuzulu karibuni.

Wajumbe hao watatu wakionekana wenye maarifa na uzoefu na kuwabadili kiasi cha miaka 2 kabla firimbi kulia Juni 11, 2010 kuanzisha kombe la dunia kungeongeza matatizo zaidi mbali ya yale ya uhalifu na miundo mbinu.

Kuondosha shaka shaka hizo, ujumbe wa Kamati hiyo ya maandalio na wajumbe wa FIFA -shirikisho la dimba ulimwenguni ulikuwa na kikao maalumu katika Ubalozi wa Afrika Kusini mjini Berlin,Ujerumani hivi majuzi.Ulionesha picha na video jinsi maandalio yalipofikia na kuondosha wasi wasi wowote kuwa Kombe la dunia halitaanza kwa wakati.

Tumalizie sasa Ligi mashuhuri barani Ulaya:

Viongozi wa Bundesliga-ligi ya Ujerumani Hamburg wakiwa wamefungua mwanya wa pointi 3 kileleni, wana miadi kesho na Schalke 04 mjini Hamburg.huu ni mpambano pekee hapo kesho baada ya mabingwa hii leo kucheza na Karlrsruhe na Hoffenheim, klabu iliopanda daraja ya kwanza msimu huu tu na ikisimama nafasi ya pili nyuma ya Hamburg kileleni imecheza hivi punde na Hannover.

Hamburg kesho ili kubakia kileleni inalazimika kutamba mbele ya Schalke.Schalke inacheza na Kevin Kuranyi,yule mchezaji wa timu ya Taifa ,alieiacha mkono jumamosi iliopita pale Ujerumani ilipocheza na Urusi katika kanda ya Ulaya ya kuania ,kufuzu kwa Kombe lijalo la dunia.Wakuu wa Schalke wako nyuma ya hatu ya Kuranyi ingawa aliomba radhi kwa hatua aliochukua .

ni kwa jicho hili mpambano huu wa Bundesliga utaangaliwa hapo kesho.

Ama katika Premier League-Ligi ya Uingereza ,kesho itakua zamu ya West Ham united kuonana na Hull City wakati Stoke City ina miadi na Tottenham Hotspur.Duru ya mwishoni mwa wiki hii itakamilishwa jumatatu pale New Castle United itakapoikaribisha n yumbani Manchester City.

Tayari leo uwanjani timu 2 za usoni Chelsea na Liverpool zimeteremka uwanjani. Chelsea na Middelsbrough wakati Liverpool iko nyumbani kwa miadi na Wigan .

Chelsea na Liverpool zikitumai kabla kuingia uwanjani kuseleleza rekodi yao ya kutoshindwa hadi sasa msimu huu.Chelsea imekuwa ikiongoza premier League hadi leo kwa tofauti ya magoli.

Katika La Liga, ligi ya Spian Malaga ina miadi kesho na Getafe wakati Racing Santander ina kibarua kigumu mbele ya Deportivo La Coruna.Real Betis inachuana na Real Mallorca huku Athletico Bilbao wanawakirimu nyumbani wageni wao FC Barcelona. Real Madrid inashuka uwanjani jioni hii ya leo kucheza na Atletico Madrid.Espanyol mahasimu wao leo ni Villareal.

Pale kati ya wiki hii, Ufaransa na Tunesia zilipokumbana kwa dimba la kirafiki katika Stade de France, mjini Paris, mashabiki was Tunisia walizomea wimbo wa Taifa wa Ufaransa ulipopigwa uwanjani kabla dimba kuanza.

Hii ilimkasirisha mno rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na akaamua kuanzia sasa mkasa kama huo ukitokea tena basi mechi ivun jwe na mashabiki kuondoka uwanjani.

Rais wa UEFA-shirikisho la dimbala Ulaya na aliekua nahodha wa timu ya Ufaransa Michel Platini anasema mpango huo wa serikali ya Ufaransa kuvunja mechi iwapo wimbo wa taifa umezomewa ni upubavu.

Platini anadai kwa mara nyengine huu ni mfano mwengine wa "mchezo wa dimba kutekwanyara na wanasiasa" .