1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo ya Beijing kufunguliwa kesho.

7 Agosti 2008

Michezo ya 29 ya olimpik itafunguliwa rasmi kesho na halafu itakua zamu ya wanariadha.

https://p.dw.com/p/EsNN
Mjumbe wa Ujerumani katika IOC Bach na timu ya judo.Picha: picture-alliance/dpa

Baada ya maandamano na malalamiko yaliouandama mwenge wa michezo ya olimpik ya Beijing, mwenge huo utawasili kesho katika Uwanja mkuu wa jiji la Beijing kwa ufunguzi rasmi wa michezo hiyo ya 29 ya olimpik.

Rais wa Halmashauri Kuu ya olimpik Ulimwenguni (IOC) Jacques Rogge huenda ikambidi kuitangaza michezo ya Beijing ndio bora kabisa kimaandalio tangu ile ya kwanza mjini Athens, Ugiriki, 1896.

►◄

Tarehe 8, mwezi 8 mwaka 2008 itawasili kesho-tarehe iliochaguliwa na waandazi wa michezo ya 29 ya olimpik ya Beijing kuifungua rasmi michezo hiyo katika dola la wakaazi bilioni 1.3.

-

Waandazi pamoja na rais wa IOC-Halmashauri Kuu ya olimpik Ulimwenguni, mbelgiji Jacques Rogge, wanatumai viwanja na zana za kisasa walivyojenga na kutayarisha vitawatia moyo na shime mastadi wakubwa katika hodhi la kuogolea kama bingwa wa mabingwa Michael Phelps wa Marekani,Mswisi bingwa mara 5 wa Wimbledon, Roger Federer,stadi wa dimba wa Brazil ilioilaza Ubelgiji leo bao 1:0 Ronaldinho, mastadi wa riadha wa Ethiopia Gebrselassie na Kenenisa Bekele, kutamba na kunyakua medali za dhahabu,fedha na shaba.

Tayari bendera za mataifa yote yanayoshiriki zinapepea katika kijiji cha Olimpik ambacho wengi wanadai ndicho bora kuliko vyote vilivyojengwa hadi sasa.

China yenye wakaazi wengi kabisa duniani, ilikua na wafanyikazi wa kutosha -jeshi la watumishi 70,000 wa kujitokea kuiandaa michezo hii inayoanza rasmi kesho na kumalizika August 24.

Sherehe za ufunguzi za hapo kesho zitafungua pazia kwa changamoto za siku 16 na mwishoe, China inatumai itaudhihirishia ulimwengu maendeleo makubwa iliopiga mnamo miaka iliopita.

Ufunguzi wa kesho utaangaliwa kwa makini tangu na wenyeji wachina hata wageni.Muamerika ,mzaliwa wa Sudan,Lopez Lomong amechaguliwa kubeba bendera ya Marekani na anapanga kumkumbusha rais Hu jintao atakaekuwa ubavuni mwa rais George Bush wa Marekani,Lula wa Brazil,Sarkozy wa Ufaransa ambao ni kati ya viongozi 80 walioitikia mualiko, baadhi ya mambo kiongozi wa china hangependa kukumbushwa.

Waandazi wa michezo hii wa china wamekariri tena na tena kwamba hawataki spoti kuchanganywa na siasa .

Halmashauri kuu ya olimpik Ulimwenguni ikiongozwa na Mbeklegiji Jacques Rogge imesisitiza kuwa michezo ya Beijing itaingia katika historia.Kinyume na mtangulizi wake ,mspain, Juan Antonio Samaranch ambae ndie aliemkabidhi michezo hii ya beijing,miaka 7 iliopita ,hatumii sifa "michezo bora kabisa iliowahi kufanyika."

Akitumia asitumie, fashfash zikianza hapo kesho katika uwanja mkuu wa jumba la ndege,China yatumai, ulimwengu mzima utatoa sifa hiyo.

Kuanzia kesho,olimpik ni mali ya wanariadha,wanasiasa washacheza olimpik yao-alao hayo ndio matarajio ya wakaazi wa Beijing-wale wa Tibet, watakua na maoni mengine.