1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michuano ya Champions League yaendelea

3 Oktoba 2012

Baada ya Bayern Munich kuondoka patupu katika michuano ya kombe la vilabu bingwa barani Ulaya, Champions League, timu nyengine za Ujerumani, ikiwa ni pamoja na Borussia Dortmund, zinateremka viwanjani leo hii

https://p.dw.com/p/16JOh
Pambano kati ya BATE Borisov na Bayern MünchenPicha: Getty Images

Leo ni zamu ya Schalke 04 na Borussia Dortmund kuteremka kwa mara ya pili viwanjani kuania kombe la vilabu bingwa barani Ulaya-Champions League. Mabingwa watetezi, baada ya ushindi wake nyumbani dhidi ya Ajax Amsterdam, leo itapimana nguvu na mabingwa wa Uingereza, Manchester City, na wachezaji wake nyota, akina Edin Dzeko, Mario Balotelli, Sergio Aguero na carlos Tevez. Hilo linatajikana kuwa pambano kali kabisa katika kundi "D". Hata hivyo, Manchester City inaonyesha imedhoofika baada ya kushindwa na Real Madrid katika pambano lililopita, huku Borussia Dortmund ikifunga safari kwenda ugenini kifua mbele baada ya ushindi wa matano kwa bila dhidi ya Borussia M'Gladbach katika michusano ya ligi kuu ya Ujerumani.

Kocha wa Manchester City, Roberto Mancini, anaungama, akisema Borussia Dortmund ni miongoni mwa timu bora wakati huu barani Ulaya.

Jürgen Klopp Borussia Dortmund v VfL Borussia Moenchengladbach
Jürgen Klopp -kocha wa timu ya Borussia DortmundPicha: Reuters

Schalke ndio timu pekee ya ligi kuu ya Ujerumani iliyobahatika kuranda nyumbani leo katika pambano la Champions League.Tikiti zote zimeshanunuliwa, kwa hivyo uwanja wa Schalke Arena utasheheni pomoni, wakati timu hiyo ya eneo la mto Ruhr itakaporanda uwanjani dhidi ya mabingwa wa ligi kuu ya Ufaransa, Montpelier HSC. Itafaa tuseme hapa kwamba katika duru ya mwanzo, Schalke 04 iliondoka na ushindi wa mawili kwa moja ugenini dhidi ya timu ya Ugiriki ya Olympiakos Piräus katika wakati ambapo Montpelier iliondolewa patupu 1-2 na Arsenal katika kundi B. Arsenal wanacheza leo hii dhidi ya Olympiakos ya Ugiriki. Pindi mabingwa wa ligi kuu ya Ufaransa wakiondolewa patupu, matumaini yao ya kusonga mbele katika mashindano ya Champions League yatakuwa finyu, ikizingatiwa kwamba hadi sasa kundi B linaongozwa na Arsenal inayofuatiwa na Schalke. Montpelier inakamata nafasi ya tatu mbele ya Olympiakos inayoburura mkia.

Katika kundi A, timu ya Ufaransa, Paris Saint Germain, inateremka leo usiku mjini Porto kupimana nguvu na mabingwa wa ligi kuu ya Ureno. Watu sita wamejeruhiwa leo asubuhi huko Porto kufuatia ugomvi kati ya mashabiki.

)
Benedikt Howedes wa Schalke 04Picha: REUTERS

Katika Kundi C, AC Milan ya Italy haina njia nyengine isipokuwa kuondoka na ushindi itakapoteremka uwanjani ugenini dhidi ya St.Petersburg ya Urusi.

Na katika pambano la kundi D kati ya Real Madrid na Ajax Amsterdam, timu hiyo, inayoongozwa na Jose Morinho, inapewa nafasdi nzuri ya kuondoka na ushindi. Nyota yake-Ronaldo- imeanza upya kung'ara.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/SID/AFP/Reuters

Mhariri: Miraji Othman