1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michuano ya kuania Nusu Fainali za Champions League

9 Aprili 2014

Mabingwa watetezi Bayern Münich wanapimana nguvu na ManUnited huku mafahali wawili wa Hispania Atletico Madrid na FC Barcelona wakitifua vumbi nyumbani katika michuano ya kuingia nusu fainali za Champions League

https://p.dw.com/p/1BeT8
Msimamizi Felix BrychPicha: picture alliance/Claus Bergmann

Watoto wa Pep Guardiola-Bayern Munich wana nafasi nzuri ya kuondoka na ushindi nyumbani baada ya kutoka sare wiki iliyopita katika uwanja wa Old Trafford moja kwa moja dhidi ya Manchester United.Hata hivyo ujia unaozitenganisha timu hizi mbili ni mwembamba mno na hofu ni kubwa tukizingatia ule ukweli kwamba tangu watawazwe mabingwa wa ligi kuu ya Ujerumani kabla ya wakati,mabingwa hao watetezi wa kombe la vilabu bingwa barani Ulaya -Champions League, hawajashinda tena katika medani ya ligi kuu-Bundesliga.

Hata hivyo kocha wa Bayern Munich Pepe Guardiola anajiamini anasema:"Nna hakika mie tutaingia nusu fainali.Tunabidi turande ipasavyo,tutashinda.Nna hakika mie,ili kuingia nusu fainali tunahitaji kushinda."

Hata kocha wa Manchester United Moyes anategemea kuondoka na ushindi mjini Munich anasema:"Nnataraji tutafanya vyema zaidi kuliko duru ya kwanza na nnamini tunaweza na ndivyo tutakavyofanya hasa .

Nani wataondoka na ushindi

Katika wakati ambapo Bayern Munich itateremka bila ya Javi Martinez ,Bastian Schweinsteiger na Thiago,Manchester United inategemea kumteremsha uwanjani Patrice Evra na Wayne Rooney.Wakishindwa, itakuwa mara ya kwanza kwa timu hiyo bingwa ya Uingereza kutowakilishwa katika kundi la nne bora katika kipindi cha miaka 23 iliyopita.

Champions League Manchester United - Bayern München
Duru ya kwanza ya pambano kati ya Bayern Munich na Manchester UnitedPicha: Reuters/Stefan Wermuth

Pambano la pili leo usiku linawateremsha uwanjani mafahali wawili wa jadi wa Hispania Atletico Madrid na Barcelona."Litakuwa pambano kali na la kusisimua" ameungama kocha wa Atletico Madrid Diego Simeone.Nani atanyakua tiketi ya kuingia nusu fainali ya kombe la Champions League baada ya kutoka sare moja kwa moja katika raundi ya kwanza,nasema tusiandikie mate na wino upo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu