1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Migogoro ziada kuibuka barani Afrika nmwaka 2018

Oumilkheir Hamidou
12 Januari 2018

Kitisho cha kuripuka mizozo zaidi barani Afrika, mzozo wa jamhuri ya Mali wazidi makali, na kupigwa marufuku biashara ya pembe za ndovu China ni miongoni mwa mada za Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii

https://p.dw.com/p/2qk8k
Kongo Protest & Ausschreitungen gegen Präsident Joseph Kabila in Kinshasa
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Bompengo

Tunaanza na gazeti la Neues Deutschland linaloashiria mwaka 2018 utakuwa mwaka wa majanga ziada kwa bara la Afrika. Gazeti linahisi Umoja wa ulaya unatanguliza mbele sera za usalama na kujikinga dhidi ya mikururo ya wakimbizi badala ya kubuni sera za maana za maendeleo."Matatizo ya zamani hayajapatiwa ufumbuzi, mepya yanazuka. Mwaka 2018 utakuwa mwaka wa shida kwa Afrika, linaandika gazeti la Neues Deutschland na kuwataja viongozi wa kimla na mbinu zao za kung'ang'ania madaraka kuwa chanzo cha kitisho hicho. Gazeti la Neues Deutschland limemnukuu msimamizi wa shirika la Umoja wa mataifa la misaada ya dharura Mark Lowcock, akiitaja Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, Sudan Kusini, Kamerun na Zimbabwe licha ya nchi hiyo kujipatia kiongozi mpya baada ya kung'olewa madarakani Robert Mugabe aliyeitawala kwa mkono wa chuma nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kwa muda wa miaka 37, kuwa nyanja ziada za mizozo barani Afrika. Gazeti linahisi Umoja wa ulaya kwa sasa unajishughulisha zaidi na jinsi ya kujikinga dhidi ya wakimbizi. Ndio maana nchi mojawapo masikini kabisa barani Afrika, Niger itapatiwa hadi mwaka 2020 msaada wa maendeleo wenye thamani ya Euro bilioni moja kugharimia huduma za jamii na juhudi za kuzuwia wimbi la wakimbizi kuelekea Ulaya, limemaliza kuandika Neues Deutschland.

 

Hali katika jamhuri ya Mali, Afrika Magharibi nayo pia inatisha. Gazeti la mjini Berlin, die tageszeitung linasema viongozi wanaonyesha wameshindwa na nchi hiyo inazidi kusambaratika. Kuwepo wanajeshi wa Ujerumani Bundeswehr na ahadi za kupatiwa misaada ziada kutoka Umoja wa ulaya hazikusaidia kitu, kinyume chake ndicho kinachoshuhudiwa, limendelea kuandika gazeti hilo la mjini Berlin. Gazeti linazungumzia  kuhusu mashambulio yasiyokwisha  tangu ya makundi ya kigaidi  katika maeneo ya kati na kaskazini mwa Mali mpaka yale kati ya wakulima na wafugaji , mapigano yanayopelekea maelefu ya watu kukimbilia mji mkuuu Bamako.

 

Hali nchini Mali imezidi kusambaratika tangu Libya iliposambaratika, linaandika die tageszeitung linalokadiria kuibuka makundi mepya ya kigaidi , mbali na yale yaliyokuwa yakijulikana hapo awali na ambayo yana mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaida. Mwaka 2016 mashambulio 385 yameripotiwa na kuangamiza maisha ya watu  332-thuluthi mbili kati yao ni raia. Gazeti la die tageszeitung linasema mapigano hayo yametokea licha ya makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka mmoja kabla mjini Algiers. Mali iliyokuwa ikitajwa kuwa mfano wa kuigizwa wa demokrasia Afrika magharibi , inarudi nyuma badala ya kusonga mbele, hali ya umaskini imeongezeka na nafasi za kazi ni adimu. die tageszeitung linamaliza kwa kusema misaada ya maendeleo na juhudi za kuimarisha amani za vikosi vya Umoja wa Ulaya hazitoweza kuleta tija bila ya mageuzi ya kina.

 

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na marufuku ya biashara ya pembe za ndovu katika jamhuri ya umma wa china. Gazeti la Der Tagesspiegel linajiuliza eti uamuzi huo ni "hifadhi kwa wanyama wanaokabiliwa na hatari ya kutoweka au vipi? Jamhuri ya umma wa China imepiga marufuku biashara ya pembe za ndovu tangu wiki moja iliyopita. Marufuku hayo yamelengwa kusaidia kuhifadhi maisha ya ndovu wanaokabiliwa na hatari ya kutoweka. Barani Afrika, kitovu cha biashara haramu ya pembe za ndovu hadi China, marufuku ya China yamepokelewa kwa namna tofauti na hasa linapohusika suala kama uamuzi huo  umelengwa kweli kuokoa maisha ya ndovu walioko katika hatari ya kutoweka.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/ BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE

Mhariri:Yusuf Saumu