1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Migomo ya reli Ujerumani na Ufaransa

Maja Dreyer15 Novemba 2007

Madereva wasiopungua elfu tatu wa treni wa hapa Ujerumani walishiriki leo katika mgomo wa reli na kuzuia kwa kiasi kikubwa usafiri wa reli nchini humu. Lakini si tu abiria wa treni wa Ujerumani walioathirika, bali pia wale wa nchini Ufaransa ila tu sababu ya mgomo wa reli katika nchi hiyo jirani ya Ujerumani ni tofauti.

https://p.dw.com/p/CHap
Hakuna treni kwenye kituo kikuu cha treni jijini Berlin
Hakuna treni kwenye kituo kikuu cha treni jijini BerlinPicha: AP

Tangu jana madereva wa treni walianza tena mgomo wao ambao uliwahi kufanyika mara kwa mara katika mgogoro kati ya chama cha waendeshaji treni na shirika la reli la Ujerumani juu ya mikataba ya kazi unaendeleo kwa miezi kadhaa sasa. Safari hii lakini, mgomo umefika kiwango ambacho hakijawahi kutokea. Pamoja na treni za mizigo, madereva hao walizizuia pia treni za kawaida nchini kote tangu asubuhi. Katika eneo la Magharibi, nusu ya treni zote za mikoa hazikufanya kazi, Mashariki mambo yalikuwa mabaya zaidi.

Shirika la reli limeweka ratiba ya dharura, lakini haliwezi kutegemea treni tu, kama alivyosema mkuu wa usafiri wa abiria wa shirika la reli, Bw. Karl-Friedrich Rausch: “Tutatumia mabasi katika usafiri wa masafa ya mbali, kwa mfano kutoka Berlin kwenda Dresden au Frankfurt. Eneo la Mashariki linaathirika zaidi, huko asimilia 10 au 15 tu ya treni za mikoa zitafanya kazi. Kwa ujumla tutatumia na basi 450 nchini kote.”

Upande wa usafiri wa mizigo ambao unasusiwa tangu jana, hali inazidi kuwa mbaya, shirika la reli lilikiri. Nchini kote asilimia 40 ya treni za bidhaa zilifutwa. Hivyo, mgomo huu unayahusu pia makampuni mengine, kama kwa mfano viwanda vya magari. Shirika la magari ya BMW limearifu kwamba ililibidi kufunga kiwanda chake kimoja mjini Brussels kwa sababu sehemu fulani za vipuri hazikuweza kupelekwa kutoka Tchechnia na Ujerumani.

Naibu msemaji wa serikali ya Ujerumani, Thomas Steg, alionya juu ya matokeo ya mgomo kwa uchumi wa Ujerumani: “Mgomo huu ni athari kwa maendeleo ya kiuchumi ambayo yalikuwa mazuri hadi sasa. Ikiwa mgomo utaendelea utaweza kuwa na matokeo ya hatari ambayo hayatarajiwi hivi sasa.”

Hata hivyo, chama cha madereva wa treni walitishia kwamba wataendelea na mgomo wiki ijayo ikiwa shirika la reli halitatoa pendekezo jingine. Madereva hao wanataka mishahara yao iongezwe pamoja ya kupewa mkataba kwa chama hiki cha madereva wa treni. Hapa, madereva hao wanatofautiana na wenzao wa Ufaransa ambao pia walisababisha michafuko katika usafiri huko Ufaransa.

Licha ya serikali kuwa tayari kupatana na wafanyakazi wa reli, mgomo uliendelea. Kinyume na madereva wa treni wa Ujerumani wanaopigania nyongeza ya misharaha, wafanyakazi wa reli nchini Ufaransa wanapinga hasa mpango wa serikali kugeuza mfumo wa kustaafu. Kutokana na kufanya kazi saa za usiku na wikiendi, wafanyakazi wa reli nchini Ufaransa wanaruhusiwa kustaafu miaka miwili na nusu mapema kuliko wafanyakazi wengine wa mashirika ya umma nchini humo. Serikali lakini inalipa Euro Billioni tano kwa mwaka kugharamia mfumo huu, ndiyo maana rais Sarkozy anataka sheria hiyo ifutwe. Kinyume na wenzao wa Ujerumani lakini, madereva wa treni nchini Ufaransa wanapata mishahara mizuri, na kwa hivyo mgomo huu hauungwi mkono na Wafaransa wengi.

Wakati huo huo, mashirika ya ndege na kukodisha magari nchini Ujerumani wanafurahia kuwa na wateja wengi. Wale lakini waliotumia magari badala ya treni katika eneo la Kusini mwa Ujerumani walikabiliwa na hali ngumu mabarabarani kutokana na theluji na barafu zilizosababisha ajali na misongamano na lilolongo mirefu ya magari.