1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miili ya watu 150 yaendelea kutafutwa

Admin.WagnerD25 Machi 2015

Wafanyakazi wa shughuli za uokozi wa Ufaransa wanaendelea kuitafuta miili ya watu 150 wakiwemo watoto wa shule 16 walipoteza maisha katika ajali ya ndege ya Shirika la Ujerumani iliyotokea katika eneo la milima ya Alps

https://p.dw.com/p/1ExDs
Frankreich Seyne les Alpes Absturz Germanwings A320
Helkopta za Ufaransa zikiwa katika eneo la milima ya AlpsPicha: picture-alliance/dpa/P. Kneffel

Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Barcelona, Uhispania kuelekea mji wa Ujerumani wa Dusseldorf.Maafisa wanachunguza kwanini ndege hiyo ya Germawings, tawi la Shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa ilianguka. Hakukuwa na mawasiliano yoyote kutoka kwa marubani ambao pia hawakujibu mawasiliano kutoka kwa maafisa wa ardhini wanaosimamia safari za ndege.

Jitihada za msako

Helikopta zimekuwa zikiwendelea na msakao katika eneo ilipoanguka ndege hiyo chapa 4U9525. hadi sasa chombo kinachorekodi mawasiliano ya safari kimepatikana kikiwa kimeharibika, na duru zilizo karibu na shughuli za uchunguzi zimesema leo asubuhi kwamba kimepelekwa mjini Paris kwa ukaguzi. Lakini chombo cha pili kinachojulikana kama sanduku jeusi na ambacho hurekodi taarifa zote za safari bado hakijapatikana. Mabaki ya ndege hiyo yametawanyika kila mahala. Familia za marehemu zinatarajiwa kuwasili kwenye kituo kinachoongoza shughuli za uokozi, katika kijiji kimoja karibu na eneo la ajali. Rais wa Ufaransa Francois Hollande, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy pia wanatarajiwa kufika eneo hilo baadae leo mchana. Kansela Merkel akielezea kushtushwa na taarifa hizo alisema nchi hizo tatu zimekubaliana kushirikiana.

Frankreich Seyne les Alpes Absturz Germanwings A320
Jitihada za uokozi wa miili ya waliokufa katika ajaliPicha: picture-alliance/dpa/A. Estevez

Wengi wa waliouwawa miongoni mwa abiria 144 na wahudumu sita wa ndege hiyo ni Wajerumani na Wahispania, wakiwemo wanafunzi 16 wa Kijerumani waliokuwa wakirudi nyumbani kutoka ziara ya shule nchini Uhispania. Shule yao katika mji mdogo wa Haltern itakuwa na misa maalum ya maombi leo kuwakumbuka vijana hao na bendera zitapepea nusu mlingoti hadi Ijumaa kote nchini.

Siku tatu za maombolezo

Wakati huo huo Uhispania imetangaza siku tatu za maombolezi na kutakuwa na dakika moja ya ukimya kuwakumbuka marehemu leo mchana. Mfalme Felipe VI alikatisha ziara yake Ufaransa kurudi nyumbani mara baada ya kupata taarifa ya msiba huo. Waimbaji Opera Oleg Bryjak aliyekuwa na umri wa miaka 54 na Maria Radner waliokuwa wakisafiri kurudi nyumbani Dusseldorf , pamoja na mumewe Radner na mtoto wao mdogo, pia walikuwemo ndani ya ndege hiyo.

pia kulikuwemo raia watatu wa Mexico, wawili kutoka Colombia, Waargentina wawili ,raia wawili pia wa Australia, Muingereza na Mdeni na Mbeligiji.

Mwenyekiti mtendaji wa Germanwings Thomas Winkelmann amesema ndege hiyo aina ya AirBus A320 ilikuwa imefanyiwa ukaguzi wa mwisho wa usalama Jumatatu iliopita. Ajali hii ni mbaya zaidi miongoni mwa ajali za ndege katika ardhi ya Ufaransa tokea 1974 ilipoanguka ndege ya Shirika la ndege la Uturuki na kuwauwa watu 346.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman,afp, epd

Mhariri: Mohammed Khelef