1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Miito ya usitishwaji mapigano Gaza yatolewa

26 Oktoba 2023

Wakati vita vikiendelea huko Gaza, miito ya usitishwaji mapigano imeendelea kutolewa huku mataifa kadhaa ya kiarabu yakilaani vitendo vya kuwalenga raia katika mashambulizi ya anga ya Israel.

https://p.dw.com/p/4Y4T3
Gazastreifen | Trauer nach Raketeneinschlag | Ahli Arab Krankenhaus in Gaza
Muuguzi na raia wengine wa Kipalestina wakilia baada ya kupewa taarifa ya vifo vya wapendwa wao katika Hospitali ya Al-Shifaa huko Gaza: 17.10.2023Picha: Abed Khaled/AP/picture alliance

Tukianza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyad al-Maliki ambaye ametoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza na kuomba misaada ya kibinadamu isizuiliwe.

 Al- Maliki ameyasema hayo akiwa ziarani mjini The Hague nchini Uholanzi, na kusisitiza kuwa Israel inaendesha vita vya kulipiza kisasi kwa lengo la kuwaangamiza kabisa Wapalestina.

Siku ya Jumatano, Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Palestina alitembelea katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC na kukutana kwa mazungumzo na Mwendesha Mashtaka Mkuu Karim Khan pamoja na Rais wa Mahakama hiyo Piotr Hofmansk, ambapo amewataka kuichunguza Israel kwa uhalifu wa kivita huko Gaza.

USA New York | UN-Sicherheitsrat | Debatte über Nahost | Riyad al-Maliki, Palästinensische Autonomiegebiete
Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyad al-Maliki Picha: Shannon Stapleton/REUTERS

Mahakama ya ICC imekuwa ikilichunguza kundi la Hamas pamoja na Israel kwa madai ya uhalifu wa kivita huko Gaza tangu 2021.

Nao viongozi wa  Umoja wa Ulaya  wamekutana mjini Brussels, nchini Ubelgiji kujadili mzozo huu wa Mashariki ya Kati na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema watashughulikia suala la kupeleka misaada ya kibinaadamu kwa wakazi wa Gaza ambao amesema pia ni wahanga wa kundi la Hamas ambalo linazingatiwa na Umoja wa Ulaya, Marekani na mataifa kadhaa kuwa kundi la kigaidi.

Soma pia:Bunge la Marekani laidhinisha azimio la mshikamano na Israel

Naye, Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Ulaya ECB Christine Lagarde amesema wanafuatilia kwa makini athari za kiuchumi zinazo weza kutokea kufuatia mzozo kati ya Israel na Hamas, hasa kuhusu bei ya nishati au kiwango cha imani itakayoendelea kuonyeshwa na wadau wa kiuchumi.

Gazastreifen, Khan Yunis | Essenverteilung durch das UN-Flüchtlingshilfswerk UNRWA
Wapalestina wakiwemo watoto wakipokea msaada wa chakula kutoka shirika la kimataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA huko Khan Yunis, Gaza: 24.10.2023Picha: APA Images/ZUMA/picture alliance

Aidha, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limesema linahitaji haraka mno bidhaa ya mafuta ili kuendelea na jukumu lake la kuokoa maisha ya watu katika operesheni za kibinadamu huko Gaza ambako kumeshuhudiwa mashambulizi ya anga ya Israel kwa karibu wiki tatu.

Mashirika ya misaada yamekuwa yakilalamika kwamba msaada unaowasili Gaza hautoshi ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo:

 "Sisi ni wafanyakazi wa kujitolea, tunasaidia katika usambazaji wa chakula, lakini kiasi kilichopo hakitoshi kabisa. Tunahitaji hadi mara kumi ya kiasi wanacholeta kwa sasa."

Mataifa ya kiarabu yalaani vitendo vya kuwalenga raia

Mawaziri wa mambo ya nje wa Falme za Kiarabu, Jordan, Bahrain, Saudi Arabia, Oman, Qatar, Kuwait, Misri na Morocco wamedhihirisha msimamo huo na kusisitiza kwamba kumekuwepo na ukiukwaji wa sheria ya kimataifa eneo hilo.

Saudi-Arabien | Besuch chinesischer Staatschef Xi Jinping in Riad
Rais wa China Xi Jinping, Mwanamfalme wa Saudia na Waziri Mkuu Mohammed bin Salman Al Saud, Mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa Al Khalifa, Mwanamfalme wa Kuwait Sheikh Mishal Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah , Naibu Waziri Mkuu wa Oman katika Baraza la Mawaziri Sayyid Fahd bin Mahmoud Al Said, Mtawala wa Fujairah wa Falme za Kiarabu (UAE) Sheikh Hamad bin Mohammed Al Sharqi, na Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba (GCC) Dk Nayef Falah Al-Hajraf wakati wakihudhuria Mkutano kati ya China na GCC, mjini Riyadh, Saudi Arabia: Desemba 9, 2022.Picha: Xie Huanchi/Xinhua/picture alliance

Taarifa ya pamoja ya mataifa hayo ya kiarabu ilitaja kuwa haki ya kujilinda haihalalishi uvunjwaji wa sheria na kupuuza haki za Wapalestina huku wakikemea vitendo vya Israel kuwahamishwa kwa lazima na adhabu ya jumla huko Gaza.

Soma pia: UN yatishia kusimamisha misaada ya kiutu Gaza

Israel inasema uvamizi wa Hamas wa Oktoba 7 ulisababisha vifo vya takriban watu 1,400 huku Wizara ya afya ya Gaza ikisema leo Alhamisi kuwa zaidi ya watu 7,028 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel tangu wakati huo.

Idadi hiyo ya vifo huenda ikaongezeka upande wa Palestina ikiwa Israel itaaanzisha mashambulizi mengine ya ardhini yanayodhamiria kuliangamiza kabisa kundi la Hamas.