1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miito yaongezeka kuitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia mzozo Zimbabwe

23 Aprili 2008

-

https://p.dw.com/p/Dn0m

HARARE

Miito ya kuitaka jumuiya ya kimataifa iingilie kati mgogoro wa kisiasa nchini Zimbabwe inazidi kutolewa.Viongozi wa kidini nchini humo wameutaka Umoja wa mataifa na nchi za Kiafrika kuingilia kati kusuluhisha mgogoro uliopo Zimbabwe wakihofia kwamba ghasia zinaweza zikafia kiwango cha mauaji ya halaiki.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon ameelezea masikitiko yake na kuvunjwa moyo kuhusu hali ya Zimbabwe akisema ni jambo lisilokubalika kwamba matokeo hayajatolewa wiki tatu baada ya uchaguzi. Wakati huohuo gazeti la serikali nchini Zimbabwe la The Herald limesema kwamba nchi za eneo hilo zinapasa kusimamia majadiliano ya kutafuta serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa itakayoongozwa na rais Robert Mugabe ili baadae kufanyike uchaguzi mwingine utakaokuwa huru na wa haki.Kwengineko meli iliyosheheni silaha zilizokuwa zikipelekwa Zimbabwe kutoka China huenda ikalazimika kurudi nyumbani baada ya Afrika Kusini kukataa bandari yake kutumiwa kupakua shehena hizo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China amesema meli hiyo itarudi China kwasababu hakuna bandari ya kutia nanga.