1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miradi ya kupambana na ukimwi yapata fedha zaidi duniani

Sekione Kitojo1 Desemba 2010

Ripoti ya umoja wa mataifa kuhusu hali ya ukimwi duniani: mataifa tajiri yatoa fedha zaidi.

https://p.dw.com/p/QMcB
Leo ni siku ya ukimwi duniani .Picha: AP

Ripoti ya iliyotolewa jana kuhusu hali ya ugonjwa wa ukimwi na maambukizi ya virusi vya HIV duniani imesema kuwa , mataifa tajiri yameimarisha utoaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya afya katika nchi masikini , zaidi ya mara nne kati ya mwaka 1990 na 2010 , na hii inatokana kwa kiasi kikubwa na hali ya kutambua mahitaji ya kupambana na ugonjwa huo wa ukimwi.

Utafiti uliofanywa na taasisi ya afya na tathmini ya chuo kikuu cha Washington , umegundua kuwa hatua ya upatikanaji wa fedha zaidi kwa miradi ya afya imeongezeka , kutoka dola bilioni 5.66 katika mwaka 1990 hadi kiwango kinachokadiriwa kufikia dola bilioni 26.87 mwaka huu.

Miradi inayohusiana na ukimwi na HIV inapata kiasi cha dola bilioni 6.16, ama karibu robo ya kiasi chote cha fedha zinazotolewa.

Ugonjwa huo wa ukimwi ambao umesababisha watu milioni 25 kupoteza maisha yao tangu pale ugonjwa huo uliporipotiwa kwa mara ya kwanza mwaka 1981, ni moja ya sababu ambazo zimesababisha fedha nyingi zaidi kupatikana kutoka katika mataifa tajiri kwa ajili ya mipango ya afya duniani, mwandishi wa ripoti hiyo kuhusu ukimwi duniani, Chris Murray, amesema .

Ongezeko la utoaji wa fedha kwa ajili ya afya katika mataifa yanayoendelea umechochewa kwa sehemu fulani na hisia za ubinadamu ambazo watu wengi wa mataifa ya Magharibi wamekuwa nazo , kwamba iwapo una fedha unaweza kupata matibabu ya dawa dhidi ya HIV, lakini matibabu kama hayo hayapatikani katika mataifa masikini. Hali hiyo pamoja na wanaharakati wanaopambana na ukimwi pamoja na makundi ya kutoa ushauri limekuwa ni suala kuu linalosukuma hali ya kuongezeka upatikanaji wa fedha kwa ajili ya afya duniani katika mataifa yanayoendelea.

Nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, sehemu ya dunia ambayo imeathirika sana na ukimwi, imepata kiasi kikubwa cha fedha hizo katika mwaka 2008, ambapo ilipokea kiasi cha dola bilioni 6.92, ama asilimia 29 ya jumla ya fedha zote zilizotolewa. Sehemu kubwa ya fedha hizo imekwenda kwa miradi ya ukimwi na HIV.

Wakati huo huo, watoto wengi wanaweza pia kuzaliwa bila ya maambukizi ya ukimwi iwapo jumuiya ya kimataifa itaongeza juhudi katika upatikanaji wa huduma ya matibabu ya HIV, pamoja na kuilinda jamii, ripoti hiyo ya umoja wa mataifa imesema.

Flash-Galerie HIV / Aids 2010
Mama akiwa amevalia kitambaa usoni akitoa tahadhari ya maambukizi ya damu.Picha: AP

Ripoti hiyo iliyotolewa na shirika la kuwahudumia watoto UNICEF limegundua kuwa mamilioni ya wanawake na watoto , hususan katika mataifa masikini wanakosa kupatiwa huduma ya upatikanaji wa dawa za kuwakinga dhidi ya maambukizi, ama na kutokana na jinsia yao ama hadhi yao ya kiuchumi katika jamii ama maeneo watokayo ama elimu yao.

Wakati watoto wamefaidika na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya ukimwi, ripoti hiyo imesema , hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa kuhakikisha kuwa wanawake wote na watoto wanauwezo wa kupata dawa pamoja na huduma za afya ambazo zinalenga katika kumkinga mama kumwambukiza mtoto virusi vya HIV.

Mwandishi : Sekione Kitojo / RTRE

Mhariri: Miraji Othman