1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miradi ya maji vijijini yaleta mafanikio

Josephat Nyiro Charo4 Septemba 2014

Wakati dunia ikiadhimisha wiki ya maji utafiti kuhusu tatizo la maji barani Afrika umegundua kwamba miradi inayoshusisha kutolewa ada ya kutumia maji ni chanzo cha mafanikio katika nchi nyingi zinazoendelea.

https://p.dw.com/p/1D6Gr
World Water Week Flagge
Picha: by-sa/worldwaterweek

Utafiti huo unaonyesha kwamba miradi mingi ya maji vijijini ambayo inakusanya pesa kwa ajili ya kuisimamia katika shughuli za matengenezo na hata kuihimili imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuliko visima vilivyochimbwa na wafadhili katika nchi hizo.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na chuo kikuu cha North Carolina Chapel Hill nchini Marekani UNC kwa ushirikiana na shirika la msaada la Water and Sanitation for Afrika visima vingi vilivyochimbwa katika nchi zinazoendelea na mashirika ya wafadhili vimeishia kutofanya kazi baada ya mwaka mmoja tu. Lakini katika miradi ambayo inasimamiwa na wanavijiji wanaokusanya pesa kutokana na maji ya visima hivyo imebainika kwamba visima hivyo vimewezekana kukarabatiwa na hatimae kuweza kufanya kazi tena kwa muda wa miongo kadhaa.

Kwa hivyo kwa mujibu wa Jamie Bartram kutoka chuo hicho cha North Carolina aliyeongoza utafiti huo pamoja na Jennifer Holzworth mfumo mzuri katika kumaliza tatizo la maji barani humo ni ule unaotilia mkazo juu ya matunzo ya visima hivyo vya maji pamoja na matengenezo endapo vinavunjika.

Utafiti huo umefanyika nchini Ghana ambapo visima 1,470 vilihusika ambapo 898 kati ya hivyo vilichimbwa na shirika la msaada linalowashughulikia watoto la World Vision.Wanasayansi hao walioendesha utafiti huo wanasema visima vilivyoonekana kuwa katika hali nzuri na vinavyoendelea kutoa maji ni vile vilivyohusisha mfumo wa kutoza fedha wanaotumia maji hayo fedha ambazo zimekuwa daima zikitumiwa kuhakikisha ubora wa visima hivyo unaendelea kuwepo. Visima kiasi ya 80 vilivyochimbwa na shirika hilo la World Vision bado vinaendelea kutunmiwa ikiwa ni miaka 20 baada ya kuchimbwa katika taifa hilo.

Utafiti kuwasilishwa kwenye mkutano wa Stockholm

Utafiti huo uliofadhiliwa na wakfu wa Conrad N Hilton utawasilishwa katika maadhimisho ya wiki ya maji mjini Stockhom nchini Sweden wiki hii. Wakfu wa Conrad Hilton umetumia zaidi ya dolla milioni 80 katika kipindi cha miongo miwili kuhakikisha kwamba kiasi watu milioni 2 wanapata huduma ya maji safi na hasa barani Afrika.

Zentralafrikanische Republik Trinkwasser in Bangui 07.01.2014
Tatizo la maji Bangui, Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: picture-alliance/AP Photo

Kutokana na utafiti huo Steven M Hilton rais na mwenyekiti wa wakfu huo ambao unahusika katika mikakati ya uwekezeji anasema utafiti huo ni jambo la kutia moyo na hasa ikizingatiwa wakfu huo umekuwa ukijihusisha na mpango wa kuziimarisha jamii ili kutoa nafasi ya kuwa na mifumo bora ya kudumu ya maji safi.

Halikadhalika imebainika kwamba katika jamii ambako shirika la msaada la World Vision linaendesha shughuli zake imekuwa jambo la kusaidia ikiwa zinapatikana kwa pamoja huduma za maji, mifumo ya maji taka vyoo na hata kamati za kusimamia usafi. Kamati hizo kimsingi zinahusisha tu watu wa eneo husika wanaobeba pia jukumu la kusimamia miradi yote ya maji ikiwemo mpango wa kukusanya mapato yanayotokana na visima hivyo ambayo baadae hutumiwa katika kulipia matengenezo na ukarabati wa visima hivyo pale inapotokea kwamba visima hivyo haviwezi kutoa maji tena.

Pamoja na hayo ikumbukwe kwamba zaidi ya watoto 1600 hufariki dunia kila siku kutokana na maradhi yanayosababishwa na maji machafu pamoja na mifumo duni ya maji taka na ukosefu wa mazingira safi katika nchi zinazoendelea.Idadi hiyo ya vifo ni zaidi ya idadi inayosababishwa na maradhi ya Malaria na Ukimwi kwa mujibu wa shirika hilo la World vison ambalo zaidi limekuwa likifanyia shughuli zake katika nchi hizo zinazoendelea.Katika nchi za Afrika Magharibi shirika hilo limefanikiwa kuwapatia maji safi mailioni ya watu hatua iliyochangia kupunguza kiwango cha maradhi ya kuharisha,na mengine yanayosababisha na ukosefu wa maji safi.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/World Vision,Press Release

Mhariri:Josephat Charo