1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miripuko katika mji mkuu wa Msumbiji wauwa zaidi ya 80

Mohammed Abdul-Rahman23 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CHlN

Miripuko katika katika ghala moja ya silaha karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa mji mkuu wa Msumbiji-Maputo, umewauwa watu karibu 80 na zaidi ya 100 kujeruhiwa. Taarifa ya serikali na idara ya huduma za dharura leo imesema wengi walioathirika kutokana na ajali hiyo ni watoto.

Miripuko ya mabomu na risasi ilisababisha kuripuka kwa silaha nyengine katika ghala hiyo jana usiku na kusikika katika mji mkuu huo Maputo. Makombora yalifyatuliwa kwa mripuko na kuangukia katika baadhi ya nyumba karibu na eneo hilo katika wilaya ya Mazharine na nyumba nazo kuwaka moto na kusababisha wakaazi kukimbia katika hali ya wasi wasi mkubwa , huku watoto wakionekana kuranda randa mabarabarani.

Msemaji wa idara ya huduma za dharura Bonificio Antonio alisema kwamba zaidi ya watu 80 wameuwawa na karibu 165 wengine wamejeruhiwa .

Waziri wa afya alitaja idadi ya waliouwawa kuwa 72 na majeruhi 360. Wakaazi wametakiwa kuyahama makaazi yalio karibu na ghala hiyo ya silaha, kukihofiwa juu ya uwezekano wa kuripuka silaha nzito zaidi. Taarifa zinasema mitaa 10 ya jirani imeathirika kutokana na ajali hiyo. Polisi walilizingiara eneo hilo na magari ya wagonjwa yalikua hadi leo mchana yakisafirisha maiti na majeruhi hadi hospitali kuu, huku wakaazi wakijazana kuangalia orodha ya majina kuwatafuta ndugu na jamaa zao.

Akizungumza katika televisheni ya taifa-TVM,maji wa wizara ya ulinzi Joaquim Mataruca amesema huenda joto kali kabisa katika miezi ya hivi karibuni ndiyo chanzo cha kuripuka silaha hizo. Joto hilo limefikia digirii 38. mripuko huo ni wa pili katika muda wa miezi miwili. Mripuko wa kwanza Januari uliwaua watu 3 na kuwajeruhi wengine kadhaa.

Serikali ya Msumbiji imekua katika zoezi kuziharibu silaha za hatari katika ghala hiyo na hivi karibuni ziliharibiwa karibu tani 100 za silaha za aina hiyo. Bw Mataruava akaongeza kwamba silaha zaidi zitaharibiwa katika siku zijazo.

Rais Armando Guebuza aliikatiza ziara yake nchini Afrika kusini amelitembelea eneo hilo la mripuko leo asubuhi pamoja na majeruhi katika hospitali kuu ya Maputo. Rais Guebuza na Waziri wake wa ulinzi Tobias Dai wametoa wito kuwataka raia wabakie watulivu.