1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miripuko ya New York haihusiani na ugaidi wa kimataifa

18 Septemba 2016

Gavana Andrew Cuomo amesema Jumapili (18.09.2016) mripuko uliotingisha wilaya ya Manhattan New York na kujeruhi watu 29 hauonekani kuwa unahusiano na ugaidi wa kimataifa na ameapa wahusika watasakwa na kushtakiwa.

https://p.dw.com/p/1K4XK
Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Ruttle

Amesema kwamba polisi wa ziada 1,000 wanawekwa kufuatia mripuko huo wa Jumamosi usiku huko Chelsea ambacho kimsingi ni kitongoji cha wakaazi upande wa magharibi wa Manhattan ambao unajulikana kwa maduka mengi ya sanaa na kuna na idadi kubwa ya mashoga.Gavana huyo amewataka wakaazi wa New York waendelee na shughuli zao kama kawaida.

Amesema "Hatutowaachia washinde.Hatutowaachia walete hali ya hofu"

Gavana huyo wa chama cha Demokratik amesema uchunguzi wa awali hauonyeshi kuwepo na uhusiano na ugaidi wa kimataifa na kwamba hakuna kundi la kigaidi lililodai kuhusika.

Maafisa wa serikali wanasema mripuko huo wa Manhattan hauonekani kuwa na uhusiano na mripuko wa bomba ulitokea mapema Jumamosi huko New Jersey na kulazimishwa kufutwa kwa mbio za hisani.

Vifaa vya mripuko

Afisa mmoja wa polisi ameliambia shirika la habari la AP kwamba kifaa cha pili ambacho maafisa wamekichunguza kutoka majengo manne kutoka eneo la tukio inaonekana ilikuwa ni kifaa cha kuivisha chakula "pressure cocker" ambacho kimeunganishwa na waya na simu ya mkono.

Gavana wa New York Andrew Cuomo (kulia) na Meya wa mji huo Bill de Blasio wakiwasili katika eneo la tukio.
Gavana wa New York Andrew Cuomo (kulia) na Meya wa mji huo Bill de Blasio wakiwasili katika eneo la tukio.Picha: picture-alliance/newscom/J. Angelillo

Afisa huyo ambaye hakutaja jina lake litajwe kwa kuwa haruhusiwi kuzungumzia uchunguzi unaoendelea amesema kifaa hicho kimekutikana ndani ya mkoba wa plastiki katika Mtaa wa 27 Magharibi . Kifaa hicho kiliondolewa kwa kutumia roboti na kupelekwa idara ya zima moto kwa uchunguzi.

Mripuko ulitokea Mtaa wa 23 Magharibi mbele ya makaazi ya walemavu wasioweza kuona karibu na eneo lenye mikahawa mingi na duka kubwa la viatu.Mripuko huo inaonekana kutokea ndani ya kisanduku kiliokuwa na zana za ufundi.

Majeruhi waruhusiwa kuondoka hospitali

Kwa mujibu wa Gavana Cuomo wote waliojerubhiwa ambao walifikishwa hospitali wameruhusiwa kurudi nyumbani.Wengi wamejeruhiwa kutokana na vipande vya vioo na vitu viliovunjika.

Watu wakiangalia eneo la mripuko katika kitongoji cha Chelsea cha Manhattan mjini New York.
Watu wakiangalia eneo la mripuko katika kitongoji cha Chelsea cha Manhattan mjini New York.Picha: Reuters/R. Umar Abbasi

Baadhi ya njia za reli za chini ya ardhi ziliathiriwa na mripuko huo ambao uliwatia hofu baadhi ya wakaazi wa wageni wa New York ikiwa ni siku chache baada ya kufanyika kwa kumbukumbu ya miaka 15 ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11.

Ikulu ya Marekani imesema Rais Barack Obama amejulishwa juu ya mripuko huo ambao umekuja wakati viongozi wa dunia wakielekea Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo Jumatatu kuzungumzia suala la mzozo wa wakimbizi na mzozo wa Syria.Mkutano huo unafanyika kama maili mbili kutoka eneo la mripuko.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP/AP

Mhariri : Sekione Kitojo