1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miripuko yasababisha maafa makanisani Misri

9 Aprili 2017

Mabomu yameripuka katika makanisa mawili kwenye miji tafauti nchini Misri na kuuwa takriban watu 38 na kujeruhi wengine takriban 100 katika mashambulio yanayodaiwa kufanywa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu.

https://p.dw.com/p/2axA2
Ägypten weiterer Anschlag auf Kopten in Alexandria
Picha: Reuters/Str

Mabomu yameripuka katika makanisa mawili kwenye miji tafauti wakati waumini wakiadhimisha Jumapili ya Mnazi nchini Misri na kuuwa takriban watu 38 na kujeruhi wengine takriban 100 katika mashambulio yanayodaiwa kufanywa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu.

Katika shambulio la kwanza Jumapili (09.04.2017) bomu liliripuka katika mji wa mwambao wa Alexadria ambao ni makao ya kihistoria ya Wakristo nchini Misri na kuuwa watu 11 na kujeruhi wengine 35 muda mfupi tu baada ya Papa Tawadros wa Pili kumaliza misa.Wasaidizi wake baadae wamekiambia chombo cha habari cha eneo hilo kwamba kiongozi huyo wa kidini amenusurika bila ya kujeruhiwa.

Kundi la Dola la Kiislamu limedai kuhusika na shambulio hilo kupitia shirika lake la habari la Aamaq baada ya kuonya hivi karibuni kwamba itazidisha mashambulizi yake dhidi ya Wakristo wa Misri.

Miripuko hiyo inakuja mwanzoni mwa Wiki Takatifu kuelekea Pasaka na ikiwa ni wiki chache tu kabla ya Papa Francis kuanza ziara yake katika nchi hiyo yenye idadi kubwa kabisa ya watu katika ulimwengu wa nchi za Kiarabu.

Ägypten weiterer Anschlag auf Kopten in Alexandria
Milipuko iliyalenga makanisa ya KoptikPicha: Reuters/Str

Kituo cha televisheni cha CBC kimeonyesha mkanda kutoka ndani ya kanisa huko Tanta ambapo idadi kubwa ya watu walikuwa wamezunguka kile kinachoonekana kuwa ni miili ya watu waliokufa ikiwa imefunikwa makaratasi.Naibu waziri wa afya wa mkoa Mohammed Sharshar amethibitisha maafa hayo.

Papa Francis alaani mshambulizi

Papa Francis amelaani mashambulio hayo ya mabomu na kutuma rambi rambi nzito kwa nduguye Papa Tawardos wa Pili, Kanisa la Koptik na watu wote katika taifa hilo la Misri.Habari za mshambulizi hayo zimekuja wakati Papa Francis mwenyewe alipokuwa akiadhimisha Jumapili hiyo ya Mitende katika uwanja wa kanisa la Peter huko Vatikani.

Sheikh Mkuu Ahmed el Tayeb ambaye ni mkuu wa Al-Azhar kituo kikuu cha elimu kwa Waislamu wa madhehebu ya Sunni pia amelani mashambulio hayo kwa kuyaita kuwa "miripuko ya kigaidi ambayo imewalenga wau wasiokuwa na hatia."Israel na kundi la Hamas linalotawala Gaza pia wamelani mashambulio hayo.

Mashambulizi hayo yameongeza hofu kwamba Waislamu wa itikadi kali ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipambana na vikosi vya usalama katika rasi ya Sinai sasa wanaelekeza mashambulizi yao kwa raia.

Kundi la Dola Kiislamu laonya

Ägypten nach Anschlag auf Kirche inTanta
Wamisri wakiwa nje ya Kanisa la Koptik huko Tanta baada ya mripuko.Picha: Reuters/M. Abd el Ghany

Kundi lenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu limedai kuhusika na shambulio la kujitowa muhanga katika kanisa la Cairo hapo mwezi wa Disemba ambalo limeuwa watu 30 wengi wao wakiwa ni wanawake pamoja na kufanya mfululizo wa mauaji katika eneo tete la Sinai na kusababisha mamia ya Wakristo kukimbilia maeneo yalio na usalama zaidi nchini humo.

Hivi karibuni kundi hilo limetowa mkanda wa video likiapa kuzidisha mashambulizi dhidi ya Wakristo ambao imewaita "makafiri" wenye kuyawezesha mataifa ya magharibi dhidi ya Waislamu.

Wakristo wa Kikoptik kwa kiasi kikubwa wameunga mkono kupinduliwa na jeshi kwa Rais Mohammed Mursi Muislamu wa itikadi kali na wameshukiwa na ghadhabu za Waislamu wengi wa itikadi kali ambao wameshambulia makanisa na taasisi nyengine za Wakristo baada ya kupinduliwa kwake.

Mwandishi :Mohamed Dahman AP/AFP

Mhariri :Yusra Buwayhid