1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMamlaka ya Palestina

Misaada ya kiutu itaanza kuingia tena Gaza

10 Aprili 2024

Misaada ya kiutu inayotolewa kwa watu wa Gaza inatarajiwa kuanza kusafirishwa tena hivi karibuni kutokea Cyprus. Mradi huo ulisiitishwa wiki iliyopita kufuatia shambulizi la Israel lililowaua wafanyakazi saba wa misaada.

https://p.dw.com/p/4edGJ
Hilfslieferungsschiff aus Zypern zur Gaza-Küste
Picha: Israel Defense Forces/REUTERS

Cyprus imesema karibu tani 1,000 za msaada wa kuwalisha watu wanaoteseka kwa njaa huko Gaza zimehifadhiwa kisiwani hapo.

Msaada huo umeshikiliwa kufuatia uamuzi wa shirika la hisani la World Central Kitchen kusitisha kwa muda na kutafakari mambo yalivyo katika Ukanda huo baada ya vifo vya wafanyakazi wake saba mnamo Aprili mosi. 
 
Huko Gaza kwenyewe, waumini wa kiislamu walikusanyika mapema alfajiri nje ya Msikiti ulioteketezwa wa Al-Farooq mjini humo, ambapo wamelalamika kwamba mashambulizi yasiokoma ya Israel yamewazuwia hata kusali ndani ya misikiti yao.

Wakati huo mjini Jerusalem, makumi ya maelfu ya waumini walimiminika kwenye msikiti wa Al-Aqsa kwa ajili ya sala ya asubuhi.

Soma pia:Biden: Sikubaliani na mbinu za Netanyahu huko Gaza

Israel imesema malori 468 ya misaada yameruhusiwa kuingia Gaza katika mkesha ya siku kuu ya Eid, lakini wakati Umoja wa Mataifa ukionya kwamba eneo hilo lililozingirwa liko kwenye kingo za baa la njaa, hakukuwa na kikubwa cha kusherehekea kwa wakaazi milioni 2.4 wa Gaza, ambapo hadi milioni 1.5 kati yao wamerundikana kwenye makambi ya mji wa kusini wa Rafah.

Na katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel, Wapalestina wengi katika mji wa Jenin walizuru makaburi na kuwaombea watu waliouawa tangu kuanza kwa vita vya Gaza.

Muafaka wa mazungumzo bado kizungumkuti

Katika mazungumzo yanayoendelea mjini Cairo kutafuta muafaka wa kusitisha vita kati yake na Hamas, Israelimekubali sharti la kuruhusu Wapalestina wapatao laki moja na nusu katika upande wa kaskazini, lakini maafisa wake wamesema wanaamini Hamas haitaki kufikia makubaliano.

Cairo, Misri | Rais Abdel Fattah el-Sisi akiwa na ujumbe mwingine wa kusaka suluhu ya vita vya Gaza.
Wapatanishi katika mazungumzo ya kusaka suluhu mjini Cairo nchini Misri.Picha: Presidency of Egypt/Handout/Anadolu/picture alliance

Huku hayo yakijiri, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez, ameliambia bunge la nchi hiyo kwamba Uhispania iko tayari kulitambua taifa la Palestina, na kuongeza kuwa alikuwa amekutana na wenzake kutoka Ireland na Maltakushinikiza hatua hii muhimu.  

Sanchez amesema utambuzi wa taifa la Palestina ni hatua sahihi kwa Ulaya na kwa jumuiya ya kimataifa.

"Ndiyo jambo sahihi kwa sababu walio wengi kijamii wanataka hivyo. Kwa sababu pia katika maslahi ya Ulaya na kwa sababu jumuiy ya kimataifa haitaweza kulisaidia taifa la Palestina ikiwa haitatambua uwepo wake."

Aliongeza kuwa "Uhispania iko tayari kulitambua taifa la Palestina."

Soma pia:Uturuki yaiwekea Israel vikwazo vya kibiashara

Pia ameishambulia serikali ya Israel chini ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, akisema majibu yake yaliopitiliza kuhusiana na shambulizi la Hamas yanafuatia miongo kadhaa ya sheria ya kiutu na kutishia kuivuruga kanda nzima ya Mashariki ya Kati na dunia nzima. 

Wizara ya afya ya Gaza imesema kwamba watu wasiopungua 33,482 wameuawa katika eneo hilo la Wapalestina katika muda wa miezi sita ya vita kati ya Israel na Hamas.

Idadi hiyo inajumlisha vifo visivyopungua 122 katika muda wa saa 24 zilizopita, imesema taarifa ya wizara hiyo inayosimamiwa na Hamas, na kuongeza kuwa watu 76, 049 wamejeruhiwa Gaza tangu kuanza kwa vita hivyo.

Wizara hiyo ya afya imesema watu 14 wameuawa, wakiwemo watoto, kufuatia shambulizi dhidi ya nyumba yao.

Jeshi la Israel limesema limelenga maeneo kadhaa katika siku ya kwanza ya Eid, ambapo ndege imeshambulia kile kilichodaiwa kuwa kituo cha kufyatulia makombora na kuuwa kundi la magaidi katika mapambano ya ardhini.

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza