1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misaada ya Urusi yaelekea Ukraine

Admin.WagnerD12 Agosti 2014

Watoa misaada ya kibinaadamu, wakiwa na shehena ya misaada hiyo kutoka Urusi leo hii limeelekea nchini Ukraine. Likiwa nchini Ukraine kundi hilo litasindikizwa na wawakilishi wa asasi ya usalama na ushirikiano ya Ulaya.

https://p.dw.com/p/1Csur
Russischer Hilfskonvoi für die Ukraine 12.08.2014
Malori ya misaada ya kitu ya Urusi, yakijiandaa na safari ya kuelekea Ukraine.Picha: picture-alliance/dpa

Akunukuliwa na shirika la habari la Interfax, rais wa zamani wa Ukraine, Leonid Kuchma alisema shehena hiyo ya pamoja na misaada kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya itawasilishwa kwa walengwa chini ya mwamvuli wa shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu na kusindikizwa na wawakilishi wa OSCE katika maeneo yote ya kaskazini-mashariki mwa Ukraine na mji wa Luhansk.

Malori 280 kutoka Urusi yameanza kufanya safari hiyo baada ya makubaliano kufikiwa kuhusu ujumbe wa kimataifa uliyohusu mpango wa misaada ya kibinaadamu. Hata hivyo shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu, ambalo linaratibu zoezi la utoaji misaada likisema, halina taarifa kuhusu kile kilichomo katika malori hayo pamoja na yanakoelekea. Hali hiyo inaweza kuzusha hofu zaidi nchini Ukraine kwenyewe na upande mwingine kwa Mataifa ya Magharibi, ambako tayari baadhi ya viongozi huko kwa nyakati tofauti wamekuwa wakielezea mashaka waliyonayao kwamba Urusi inaweza tumia fursa hiyo kama upenyo wa kutuma vikosi ndani ya eneo linaloshikiliwa na waasi.

Msafara wa malori ya Urusi

Televisheni ya Urusi NTV pamoja na mashirika ya habari yameripoti kwamba tani elfu mbili za msaada zinapelekwa nchini Ukraine, ambako mapigano kati ya wapiganaji wanaotaka kujitenga wanaoegemea upande wa Urusi na majeshi ya serikali yamesababisha zaidi ya watu 1,300 kuuwawa tangu Aprili. NTV imeonesha idadi kubwa ya malori ya rangi nyeupe yakiwa yameegeshwa katika ghala moja mjini Moscow na ikaelezwa wanapakia kila kitu kuanzia vyakula vya watoto na virago vya kulalia. Sergei Lavrov ni waziri wa mambo ya nje wa Urusi" Tumekubalina kwa kina na serikali ya Ukraine. Na matumani wenzetu wa mataifa ya magharibi wataacha maneno na kufikiria juu ya watu wote waliokosa mahitaji muhimu kama tiba na hasa kwa watoto na humua nyingine muhimu kama maji na umeme"

Russischer Hilfskonvoi für die Ukraine 12.08.2014
Malori ya misaasa yakiwa yamepangwa kwa maandalizi ya Safari.Picha: picture-alliance/dpa

Kauli ya shirika la msalaba mwekundu

Andre Loersch, msemaji wa kamati ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu, kwa upande wa Ukraine, amesema mpaka yalipofikiwa makubaliano ya kuwasilishwa kwa misaada ya kiutu katika eneo hilo hakuwa na taarifa zozote kuhusu kilichomo katika malori hayo na wala uelekeo wake. Aidha aliongeza kusema kwa hatua hiyo hakuna makubaliano yaliyofikiwa na inaonekana kuwa kama jitihada ya serikali ya Urusi.

Nayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine ilisema haikuwa tayari kusema chochote kuhusu mlolongo huo wa malori.

Athari kubwa za mapigano nchini Ukraine yameshuhudiwa mjini Luhansk, mji unaoshikiliwa na waasi. Inaelezwa kuwa mji huko kabla ya mapigano ulikuwa na watu 420,000, lakini takwimu za sasa zinaeleza kumebakiwa watu 250,000 tu, na hakuna umeme wala maji kwa siku ya tisa sasa. Hata hivyo hajaweza kufahamika mara moja kwamba malori hayo yatavuka mpaka kuingia katika jimbo hilo ambalo lipo umbali wa kilometa 100 kutoka mpakani mwa Urusi.

Mwandishi: Sudi Mnette APE/RTR
Mhariri:Yusuf Saumu