1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misaada yaanza kuwasili Haiti

Kabogo Grace Patricia14 Januari 2010

Misaada hiyo ni kwa ajili ya kuwasaidia kaisi watu milioni tatu wanaohitaji msaada wa dharura.

https://p.dw.com/p/LVVr
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.Picha: AP

Serikali kadhaa duniani pamoja na mashirika ya misaada yameendelea kupeleka misaada ya kibinaadam nchini Haiti baada ya nchi hiyo kukumbwa na tetemeko kubwa la ardhi siku ya Jumanne linalohofiwa kusababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu. Marekani kwa upande wake jana imeanzisha operesheni ya misaada ya kijeshi na kiraia kwa ajili ya Haiti, wakati wasaidizi wawili wa ngazi ya juu wa Rais Barack Obama wakiwa wameahirisha safari zao nje ya nchi kwa ajili ya kulizingatia zaidi janga hilo. Rais Obama alisema amewaamuru wasaidizi wake kulishughulikia haraka suala hili kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wa Haiti.

''Watu wa Haiti watapata msaada wote wa Marekani katika jitihada za dharura za kuwaokoa watu waliokwama chini ya vifusi na kupeleka msaada wa kibinaadam, ikiwemo vyakula, maji na madawa, ambavyo watu wa Haiti watahitaji katika siku zijazo, alisema Rais Obama.'' Kikosi cha jeshi la Marekani kitakachokuwa na kazi ya kuokoa watu waliosalimika na kujaribu kutathmini hasara iliyopatikana kutokana na tetemeko hilo la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha saba katika kipimo cha Richter, kimewasili nchini Haiti. Kamisheni ya Umoja wa Ulaya imesema itatoa Euro milioni tatu kwa ajili ya misaada ya dharura. Mataifa mengine pia ya Umoja wa Ulaya, yakiwemo Uingereza, Italia, Ufaransa na Uhispania, yametuma vifaa vya uokoaji pamoja na misaada.

Wito kwa jumuiya ya kimataifa

Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, ambaye kwa sasa ni mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, ameitaka jumuiya ya kimataifa kutoa misaada ya fedha. Bwana Clinton amesema maji, chakula, malazi na madawa vinahitajika haraka kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Haiti, hasa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Port-au-Prince. Rais huyo wa zamani anataka kuokoa maisha ya watu wengi iwezekanavyo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema hali ni ya kutisha na kutoa wito wa kutolewa misaada zaidi. Kwa upande wake, Umoja wa Mataifa umetoa dola milioni 10 kwa jili ya kugharamia kulishughulikia janga hilo. Maafisa wa Umoja wa Mataifa mjini New York wamethibitisha kuwa wanajeshi 16 wa kikosi cha kulinda usalama cha umoja huo wamekufa kutokana na tetemeko hilo la ardhi. Aidha, inadaiwa kuwa mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, Hedi Annabi, hajulikani alipo.

Japan nayo kutoa msaada

Wakati huo huo, serikali ya Japan leo imeahidi kutoa msaada wa dharura wa dola milioni tano kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Haiti. Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Japan imesema kuwa nchi hiyo imepanga kushirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa, likiwemo lile la kuwahudumia watoto-UNICEF- na la Mpango wa Chakula Duniani-WFP- katika kugawa misaada hiyo. Mbali na mashirika ya misaada na serikali kutoa misaada, watu maarufu duniani, wakiwemo wanamuziki, wameanzisha kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Haiti. Mwanamuziki wa hip-hop wa Marekani, Wyclef Jean, ambaye ni mzaliwa wa Haiti, anaongoza kampeni hiyo. Mcheza sinema, Angelina Jolie, na mpenzi wake, Brad Pitt, wamechangia dola milioni moja kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Haiti. Tetemeko hilo la Jumanne lililowaacha watu milioni tatu wakiwa wanahitaji msaada wa haraka ni baya na kubwa kabisa kuwahi kuikumba Haiti, moja ya nchi masikini sana duniani katika muda wa karne mbili.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE,DPAE)

Mhariri: Miraji Othman