1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misaada yapelekwa, mashariki ya Congo.

Nyanza, Halima3 Novemba 2008

Wakati Msafara wa kwanza wa misaada wa Umoja wa Mataifa ukiwa umewasili katika mji unaoshikiliwa na waasi, mashariki ya Congo, na kukuta kambi zikiwa tupu bila ya wakazi wake, serikali ya Congo, imetangaza hali ya hatari

https://p.dw.com/p/FmnL
Maelfu ya wakazi wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, wanadaiwa kuhangaika msituni, kukimbia uvamizi wa waasi.Picha: AP

Msafara huo, ambao uliwasili katika eneo hilo linalodhibitiwa na waasi huku ukisindikizwa na walinda amani wa umoja wa mataifa, wapatao 50, ukiwa umebeba maji na madawa uliwasili katika eneo hilo na kukuta kambi zimeachwa tupu bila ya maelfu ya wakazi wake.

Afisa wa Umoja wa Mataifa, Francis Kasai amefahamisha kuwa kambi zote zilikuwa tupu na kwamba hakuna kilichobaki.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi limesema linahofia kuwa wakimbizi hao wapatao elfu 50, walitelekezwa ama kufukuzwa katika kambi hizo, zilizo katika eneo hilo la Rutshuru ambazo hazikuwa na ulinzi, zilizoko kilomita 70 kaskazini mwa mji mkuu wa jimbo la Kivu kaskazini, Goma.

Wengi wa watu hao wanahofiwa kuwa bado hakihangaika msituni kwa ajili ya kutafuta mahitaji na msaada mwingine baada ya kukimbia mashambulio ya waasi.

Leo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mashirika hayo ya misaada kufika katika eneo hilo la Rutshuru baada ya Umoja wa Mataifa, wiki iliyopita, kusema kwamba watu takriban elfu 50, hawajulikani walipo baada ya taarifa kwamba waasi wanaoongozwa na Nkunda, kupora mali na kuchoma kambi za wakimbizi katika mji huo.

Rutshuru ni moja ya miji kadhaa iliyodhibitiwa na waasi wa Kitutsi wanaoongozwa na Laurent Nkunda tangu mwezi Agusti, katika mapigano yaliyosababisha watu milioni 1.6 kubaki bila ya makazi, kabla ya kusimamisha mapigano wiki iliyopita.

Mashirika ya misaada yamekuwa yakihangaika kuweza kufikia makumi kwa maelfu ya watu, ambao wanakimbia mapigano katika jimbo la Kivu kaskazini.

Mamia ya watu bado wameonekana barabarani leo wakirudi majumbani mwao, baada ya waasi kusitisha mapigano na kufungua njia kwa misaada ya kibinadamu kutolewa.

Wakati hali ikiwa bado tete, Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imetangaza hali ya hatari, katika mji mkuu wa eneo hilo la mashariki, Goma, ambao unatishiwa kuvamiwa na waasi, walioweka kambi kwenye viunga vya mji huo.

Gavana wa jimbo hilo la mashariki la Kivu kaskazini, Julien Paluku amethibitisha kuwepo kwa hali hiyo katika mji wote wa Goma.

Awali Jenerali muasi Laurent Nkunda alitoa tamko akisema anataka kukutana ana kwa ana na serikali ya Congo la sivyo atahakikisha anaiondoa madarakani, na kudai kuwa majeshi yake nyanayouzingira mji wa Goma sasa yameingia karibu na uwanja wa ndege wa mji huo.

Lakini tayari serikali ya Comngo imeshajibu ikisema haiko tayari hata kidogo kukutana na Jenerali huyo muasi.

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya umesema haujaondoa uwezekano wa kupeleka vikosi vyake kwa ajili ya kusaidia wakimbizi mashariki mwa Congo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uingereza David Miliband, kabla ya kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa umoja huo nchini Ufaransa, lakini akasema kuwa uamuzi hautatolewa mpaka baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likutane kujadili suala hilo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ametuma msaidizi wake anayeshughulikia masuala ya kulinda amani huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuchunguza na kutoa ripoti za kuibuka kwa ghasia hizo.