1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri bado hakujatulia

21 Agosti 2013

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wakutana Jumatano kwa dharura mjini Brussels kujadili juu ya kuishinikiza serikali ya Misri kutafuta suluhisho kwa njia ya amani na wafuasi wa rais aliyepinduliwa madarakani.

https://p.dw.com/p/19SMh
Wafuasi wa Mursi wakaidi jeshi na waendelea kuandamana
Wafuasi wa Mursi wakaidi jeshi na waendelea kuandamanaPicha: Reuters

Serikali kadhaa za nchi za Umoja wa Ulaya zimeshasema kwamba Ulaya inabidi kupunguza msaada wake wa kifedha kuelekea Mirsi lakini baadhi zimesita kuunga mkono hatua hizo ambazo huenda zikazidisha athari katika nchi hiyo na hasa kwa wananchi kuliko ilivyo kwa serikali.

Msaada unaozungumziwa hapa ni wa yuro bilioni 5 ambao Umoja huo wa Ulaya pamoja na taasisi zake uliweka ahadi ya kuipa Misri mwaka jana pamoja na vichocheo vingine vya kiuchumi.

Hata hivyo katika mkutano unaofanyika jioni hii mjini Brussels mawaziri wa mambo ya nje hawajaweka wazi ni mapendekezo gani yanayofikiriwa kujadiliwa katika kikao cha siku ya Jumatano.

Ulaya itafanikiwa kuibana serikali Misri?

Hata hivyo uwezo wa Umoja wa Ulaya wa kuitia kishindo Misri katika suala la kuibana kiuchumi ni mdogo na hasa kwasababu kiwango kikubwa cha msaada unaotoka Ulaya kimeshazuiwa tangu hapo kutokana na ukosefu wa mageuzi ya kidemokrasia katika nchi hiyo ya Misri.

Mawaziri wa mambo ya nje waandaa kikao siku ya Jumatano(25.08.2013)
Mawaziri wa mambo ya nje waandaa kikao siku ya Jumatano(25.08.2013)Picha: AFP/Getty Images

Lakini Umoja huo unategemea kwamba kupunguza zaidi msaada huo ni hatua itakayoweza kusaidia kumaliza matumizi ya nguvu ya serikali dhidi ya chama cha Udugu wa Kiislamu cha rais aliyetimuliwa madarakani Mohammed Mursi, yaliyosababisha kiasi watu 800 kuuwawa pamoja na kuzuwiya umwagikaji wa damu kati ya pande mbili zilizopo kwenye mgogoro huu.

Kila mwamba ngoma avutia kwake

Saudi Arabia imetowa taarifa hivi punde ikisema nchi za Kiarabu na Kiislamu zitaingilia kati kuisaidia Misri iwapo nchi za Magharibi zitaikatia msaada nchi hiyo kutokana na suala hilo la kuwapa mkong'oto waandamanaji wanaomuunga mkono Mursi.

Taarifa hiyo imetolewa na waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Saud-Al Faisal aliyezungumza baada ya kutokea Ufaransa alikokuwa na mazungumzo na rais wa nchi hiyo Francois Hollande ambaye anapinga kwa sauti kubwa kinachotokea Misri.

Ndani ya Misri kwenyewe leo jamii ya madhehebu ya wakatoliki na Koptic yametowa taarifa kuunga mkono hatua inayochukuliwa na jeshi dhidi ya kile ilichokiita magaidi wanaosababisha ghasia.

Wajumbe wa Marekani John McCain na Lindsey Graham wakiiwakilisha nchi yao kuhusu mzozo wa Misri
Wajumbe wa Marekani John McCain na Lindsey Graham wakiiwakilisha nchi yao kuhusu mzozo wa MisriPicha: picture-alliance/AP Photo

Mamia ya watu wameuwawa nchini Misri tangu vikosi vya usalama vilipoanza opresheni kubwa ya kuyazima maandamano na harakati za Udugu wa Kiislamu wiki iliyopita.

Nchini Marekani, Seneta John McCain ambaye ni mjumbe maalum wa nchi hiyo katika suala la mgogoro wa Misri ameitaka nchi yake kufuta msaada wa yuro bilioni 1.3 unaotolewa kila mwaka kwa ajili ya kulisaidia jeshi la Misri lakini baadhi ya wabunge nchini humo wamezungumzia wasiwasi wao juu ya hatua hiyo wakihofia huenda ikautia mashakani mkataba wa amani kati ya Misri na Israel au ikaleta madhara katika suala zima maslahi ya Marekani kuelekea Suez Kanal.

Wakati huohuo mahakama ya Misri imetangaza kumuondolea mashataka ya rushwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak aliyepinduliwa mwaka 2011, uamuzi ambao kwa mujibu wa wakili wake utafunguwa njia ya kuachiliwa kwake hivi karibuni.

Itakumbukwa Mubarak aliyetawala Misri miaka 30 alikamatwa punde baada ya kungolewa madarakani na kuwa kiongozi wa kwanza katika nchi za kiarabu kukabiliana na mashtaka.

Mwandishi: Yusuf Saumu/Reuters/Ap
Mhariri: Mohammed Khelef