1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri inapiga kura ya maoni ya katiba

22 Desemba 2012

Misri inapiga kura ya maoni kuhusu rasimu ya mswada wa katiba ambayo wachambuzi wanasema kuwa ina nafasi kubwa ya kupitishwa jambo ambalo litakuwa na athari kwa mustakabali wa siasa za nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/177q6
Picha: Reuters

Rasimu ya mswada wa katiba nchini Misri ambayo imeandikwa na wanasiasa kutoka chama cha Udugu wa Kiislamu nchini humo inatarajiwa kupitishwa leo (22.12.2012) katika kura ya maoni inayofanyika kwa awamu ya pili jambo ambalo wapinzani wanasema kuwa litasababisha mgogoro zaidi wa kisiasa.

Rasimu hiyo ilipigiwa kura kwa awamu ya kwanza wiki iliyopita na kupata uungaji mkono wa asilimia 57. Wapinzani tayari wameanza kulia kuhusu vitendo vya ubadhirifu katika awamu ya kwanza ya zoezi hilo na hivyo wanataka lirudiwe upya.

Lakini kamati inayosimamia mchakato huo wa kura ya maoni imesema kuwa hakuna kasoro zozote zilizojitokeza katika zoezi hilo ambazo zinaweza kubatilisha kura hiyo.

Maandamano ya kumpinga rais Mursi katika mji mkuu wa Misri, Cairo
Maandamano ya kuminga rais Mursi, CairoPicha: AP

Wafuasi wa Rais Mohammed Mursi aliyechaguliwa mwezi Juni mwaka huu, wanasema katiba hiyo ni muhimu ili kuiwezesha Misri kusonga mbele kuelekea mapinduzi ya kidemokrasia ikiwa ni miaka miwili tangu kuondoloewa madarakani kiongozi wa zamani Hosni Mubarak kupitia vuguvugu la umma lililozikumba nchi za kiarabu.

Wanasema kuwa katiba hiyo inasaidia kurejesha utulivu unaohitajika kuurejesha uchumi wa nchi hiyo ulioporomoka katika hali imara. Kama katiba hiyo itapitishwa, uchaguzi wa bunge utafanyika katika kipindi cha miezi miwili ijayo.

Muda wa kupiga kura vituoni

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa majira ya saa mbili asubuhi na vinatarajiwa kufungwa majira ya saa moja za usiku ingawa zoezi hilo huenda likaendelea zaidi ya muda huo kama ilivyokuwa katika awamu ya kwanza.

Raia akipiga kura eneo la Wahllokal mjini Mahalla el-Kubra
Raia akipiga kura eneo la Wahllokal mjini Mahalla el-KubraPicha: Reuters

Taarifa zisizo rasmi kuhusu matokeo ya kura hiyo zinatarajiwa kutolewa baada ya saa kadhaa, lakini kamati inayosimamia mchakato huo inaweza isitangaze matokeo rasmi ya jumla hadi hapo Jumatatu (24.12.2012) baada ya kusikiliza rufaa.

Wapinzani wanasema kuwa kura hiyo ya maoni haina manufaa kwa taifa na wanamtuhumu Rais Mursi kwa kulazimisha kufanyika haraka kwa zoezi hilo kupitia wafuasi wake wa chama cha Udugu wa Kiislamu licha ya madai kuwa rasimu hiyo inakiuka haki za Wakristu ambao wanaunda asilimia 10 ya Wamisri wote pamoja na wanawake.

Machafuko mjini Alexandria

Makundi ya upinzani na wafuasi wa Mursi yalipambana hapo jana (21.12.2012) katika mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Alexandria ambapo walirushiana mawe nje ya msikiti mkubwa pamoja na kwenye mitaa. Mabasi mawili yalichomwa moto wakati polisi walijaribu kuwatawanya watu hao kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi.

Maandamano katika mji wa Alexandria, Misri
Maandamano katika mji wa Alexandria, MisriPicha: Mahmud Hams/AFP/Getty Images)

Wachambuzi wanasema kuwa awamu ya pili ya kura hiyo inaonyesha kwa kiasi kikubwa kuwa itaungwa mkono kwa sababu inafanyika kwenye maeneo ya vijiji na mengineyo ambayo wana idadi kubwa ya wafuasi wanaopendelea mfumo wa dini.

Mkuu wa Chama cha Kiliberali cha Free Egyptians na mwanachama wa National Salvation Front ambao ni muungano wa wapinzani nchini humo ulioundwa baada ya Mursi kujiongezea madaraka Novemba 22, Ahmed Said anasema kuwa anaona machafuko zaidi yakiikumba nchi hiyo kutokana na hatua hiyo.

Said anasema kuwa "watu hawatakubaliana na namna utawala unavyoendesha mchakato huo na mambo mbalimbali nchini humo".

Mwandishi: George, Stumai/Reuters

Mhariri: Mtullya, Abdu