1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri kupiga kura rasimu ya katiba mpya

9 Januari 2014

Misri inatarajia kuipigia kura rasimu ya katiba mpya ya nchi hiyo wiki ijayo ambayo kama itapitishwa, itachukua nafasi ya katiba ya zamani ya mwaka 2012.

https://p.dw.com/p/1Ao8l
Raia wa Misri kupiga kura ya maoni kuhusu katiba mpya.
Raia wa Misri kupiga kura ya maoni kuhusu katiba mpya.Picha: Wafaa Al Badry

Katiba ya zamani ilitungwa chini ya rais wa zamani wa Misri aliyeondolewa madarakani na jeshi, Mohammed Mursi. Hata hivyo katiba hiyo mpya imezusha hofu kuwa italipa jesho mamlaka makubwa zaidi ya kulinda maslahi yake ya kisaisa na uchumi.

Rasimu hiyo ya katiba ilitungwa na kamati ya wajumbe 50 ambao walitueliwa na serikali mpya chini ya utawala wa kijeshi, ulioshika madaraka tangu mwezi Julai mwaka jana, baada ya kumwondoa madarakani Mohamed Mursi.

Kwa mujibu wa profesa wa masuala ya katiba katika chuo kikuu cha Cairo, Tharwat Badawi, rasimu hiyo ya katiba inajenga msingi wa udikteta wa kijeshi.

Wachambuzi wanasema kuwa rasimu hiyo inaonekana kuwa na mwelekeo wa kuboresha katiba ya zamani iliyopitishwa chini ya utawala wa Mursi, ambayo pia ilikosolewa kutokana na kusisitiza sheria ya Kiislamu na hivyo kuingilia uhuru wa watu, ingawa bado kuna vipengele vinavyopunguza majukumu ya viongozi wa serikali.

Rais, wabunge hawana mamlaka

Profesa Badawi ameliambia shirika la habari la IPS kuwa ikiwa rasimu hiyo itapitishwa kuwa katiba, rais na wabunge watakaochaguliwa hawatakuwa na mamlaka kwa jeshi, ambalo kiutekelezaji litakuwa ni taifa linalojitegemea.

Chini ya katiba mpya, Baraza Kuu la Jeshi litakuwa na mamlaka ya mwisho kuhusu kuchaguliwa kwa waziri wa ulinzi. Hata kama waziri huyo atateuliwa na rais, jeshi ndilo litakalokuwa na mamlaka ya juu kusimamia utekelezaji wake.

Baadhi wagoma kupiga kura ya maoni.
Baadhi wagoma kupiga kura ya maoni.Picha: picture-alliance/dpa

Kwa msingi huo, anasema Profesa Badawi, jeshi halitawajibika kwa kiongozi wa nchi, jambo ambalo anasema ni la hatari.

Wadadisi wanasema kuwa jeshi la Misri limekuwa likiweka vipingamizi na likididimiza haki ya kuwepo kwa mabadiliko kidemokrasia tangu kutokea kwa machafuko yaliyomuondoa madarakani Hosni Mubarak miaka mitatu iliyopita kutokana na vuguvugu la mapinduzi la mwaka 2011.

Wasimamizi wa sheria wamekatishwa tamaa baada ya kubaini kuwa kuna kipengele ndani ya muswada huo kinachounga mkono kitendo kilicholaumiwa cha kuwashitaki raia kwenye mahaka za kijeshi, kilichotumika kuwakamata na kuwafunga raia wapatao 2,000 kwa madai ya kuchochea vurugu mwaka 2011.

Wasi wasi juu ya mamlaka ya jeshi

Kiongozi wa Vuguvugu la Aprili 6,mwaka jana, Ahmed Maher, anasema kuwekwa kwa kipengele hicho ni "uhaini" uliofanywa na wajumbe 50 kusimamia rasimu hiyo ya katiba.

Maher amesema wale wote wanaounga mkono hatua ya jeshi kuwafunga raia na kusahau kilichotokea mwaka 2011watakuwa wamedhamiria kutojali utu na kuzingatia maslahi yao zaidi.

Maher ambaye alitoa maoni yake kupitia ukurasa wa Facebook, alihukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela mwezi uliopita kwa kosa la kuandaa maandamano kinyume na sheria kuipinga kamati iliyoteuliwa kutunga rasimu ya katiba hiyo mpya.

Waliotisha maandamano kupinga wajumbe 50 wanaoshughulikia rasimu hiyo wafungwa.
Waliotisha maandamano kupinga wajumbe 50 wanaoshughulikia rasimu hiyo wafungwa.Picha: Reuters

Wafuasi wa Mursi wametishia kususia kura hiyo ya kupitisha kwa rasimu ya katiba iliyopangwa kufanyika tarehe 14 na 15 ya mwezi huu.

Zaidi ya watu 1,000 wameuawa tangu Mursi aondolewe madarakani na maelfu ya wafuasi wake kukamatwa, na sasa rais huyo anakabiliwa na kesi ya kuchochea mauaji.

Mwandishi: Flora Nzema/IPS

Mhariri: Mohammed Khelef