1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yaionya Ethiopia kuhusu matumizi ya mto Nile

11 Juni 2013

Misri imeionya Ethiopia kwamba "milango yote iko wazi kwa" katika kushughulikia ujenzi wake wa bwawa la umeme katika mto Nile, ambao unatishia kuitumbukiza Misri katika tatizo la upatikanaji maji.

https://p.dw.com/p/18nXr
Rais wa Misri Mohammed Mursi
Rais wa Misri Mohammed MursiPicha: Imago

Akiwahutubia maelfu ya mafuasi wake waliokusanyika katika mkutano maalumu kwa ajili ya kujadili suala hilo hapo jana, rais Mohammed Mursi alisema "anathibitisha kwamba njia zote ziko wazi katika kushughulikia suala hilo."

Katika onyo hilo kali kabisa kuhusu mradi huo wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme, rais huyo alisisitiza kusema kama tone moja la maji ya mto Nile likipotea, basi mbadala wake itakuwa damu ya Wamisri. Aidha aliongeza kusema taifa hilo hapendi vita lakini halitaki pia yeyote kutishia usalama wa raia wake.

Awali mshauri wa rais huyo, alisema Misri itaishinikiza Ethiopia kusimamisha mara mmoja ujenzi wa bwawa hilo. Mapema jana Waziri Mkuu wa Misri Hisham Qandil alisema, katika siku zijazo taifa hilo litamtuma waziri wake wa masuala ya kigeni Mohammed Kamer Amr kwenda Ethiopia kuwasilisha msimamo wa Misri katika suala hilo.

Ethiopia inasisitiza kuendelea na mradi wake.

Ehtiopia tayari imeanza kutumia maji ya mto Nile kwa kuchimba mabwawa ya kuzalisha umeme mita 500 kutoka katoka mto Nile, huku Cairo ikipinga mradi wowote ule unaoathiri maji ya mto Nile kutiririka katika mkondo wake.

Mradi wa Umeme wa Ethiopia katika mto Nile
Mradi wa Umeme wa Ethiopia katika mto NilePicha: William Lloyd-George/AFP/Getty Images

Ethiopia imeendelea kusisitiza kuwa inadhamini mradi huo na kwamba kwa sasa tayari imepata mkopo wa dola billion moja kutoka China ili kutengeneza mkongo wa umeme.

Kwa upande wake Misri inasema ina haki ya kihistoria ya kutumia mto huo ambayo inadhaminiwa na mikataba miwili tokea mwaka 1929 na hadi mwaka 1959 mikataba ambayo inairuhusu Misri kutumia asilimia 87 ya maji ya mto Nile.

Lakini mkataba mpya uliyosainiwa mwaka 2010 na nchi wanachama wa mto Nile ikiwemo Ethiopia umewaruhusu nchi wanachama wa mto Nile kufanya miradi inayotumia mto huo bila kuzingatia makubaliano ya mwanzo na Misri.

Jeshi la Misri limeonya Ehiopia kuwa iwapo nchi hiyo itakuwa ni tishio kwa vyanzo vya maji kwa Misri hatua za kijeshi zitachukuliwa.

Mwandishi: Sudi/Gulana/AFPE/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman