1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yaishutumu Iran

MjahidA11 Julai 2013

Misri imeishutumu Iran hii leo kwa kuingilia masuala yake ya ndani baada ya nchi hiyo kulikosoa jeshi kwa kumuondoa rais aliyechaguliwa kihalali Mohammed Mursi.

https://p.dw.com/p/1969e
Jeshi la Misri
Jeshi la MisriPicha: Reuters

Mapema wiki hii Iran ilisema kwamba kuondolewa kwa Rais Mohammed Mursi baada ya maandamano dhidi yake kufanyika ni jambo linalopaswa kuangaliwa kwa makini na kusema mkono wa nchi za Kigeni unaingilia maswala ya nchi za kiarabu. Baada ya tamko hilo Misri nayo ikasema taifa hilo la kiislamu la Iran, halina elimu ya maendeleo ya kidemokrasia inayopitia Misri.

Hivi sasa wizara ya mambo ya nchi za kigeni ya Misri imesema jambo la kuingilia masuala ya ndani ya nchi yake kamwe halitakubalika.

Nchi hiyo pia imetoa tamko kama hilo kwa Uturuki, baada ya kuikosoa serikali ya Misri kwa kumuondoa Mohammed Mursi. Mpaka sasa mataifa ya Magharibi yamekuwa makini sana kulikosoa jeshi kwa kumpindua rais Mursi.

Waziri Mkuu Hazem al-Beblawi
Waziri Mkuu Hazem al-BeblawiPicha: picture-alliance/dpa

Huku hayo yakiarifiwa Waziri Mkuu Hazem al-Beblawi, amesema hatazuia chama cha udugu wa kiiislamu kupata nyadhifa katika baraza lake la mawaziri bora tu wawe na ujuzi wa kushikilia nyadhifa hizo.

Hata hivyo taarifa hii inakuja wakati bado polisi nchini humo wakiendelea na oparesheni ya kuwakamata viongozi wa chama hicho. Akizungumza na chombo cha habari cha AFP Belawi amesema bado mpaka sasa yuko katika harakati ya kuunda serikali yake ya mpito.

Chama cha Udugu wa kiislamu chakataa mualiko

Chama cha Mohammed Mursi tayari kimekataa mualiko wa kujiunga na serikali hiyo mpya na kuitisha maandamano makubwa hapo kesho dhidi ya kile wanachokiita mapinduzi.

Hapo jana msemaji wa wizara ya kigeni nchini Misri Badr Abdelatty aliwaambia waandishi habari kwamba Mursi amewekwa mahali salama kwa sababu ya usalama wake.

Kiongozi Mkuu wa chama cha Udugu wa Kiislamu Mohammed Badie
Kiongozi Mkuu wa chama cha Udugu wa Kiislamu Mohammed BadiePicha: picture-alliance/AP Photo

Huku hayo yakijiri polisi nchini Misri wanamtafuta kiongozi mkuu wa chama hicho Mohamed Badie, baada ya amri ya kukamatwa kwake kutolewa akishutumiwa kuchochea ghasia. Amri ya kukamatwa Badie imetolewa na mwendesha mashtaka mkuu wa Misri.

Kutokana na Ghasia zinazoendelea nchini Misri sasa Shirila la Chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa -FAO- limesema hali hiyo huenda ikapelekea uhaba wa chakula.

Marekani bado inaendelea kulifadhili jeshi la Misri

Wakati huo huo Marekani inaendelea na mpango wake wa kupeleka ndege za kivita aina ya F-16 nchini Misri, kando na kuwa na mjadala juu ya mapinduzi yaliofanywa dhidi ya Mohammed Mursi.

Kwa ujumla Marekani mpaka sasa imekataa kuiita hatua ya jeshi kama mapinduzi kwa kuwa hii inaweza kuialazimisha kusitisha msaada wa kijeshi wa takriban dola bilioni 1.3 kwa nchi hiyo.

Ndege za kivita aina ya F-16
Ndege za kivita aina ya F-16Picha: imago/Xinhua

Ndege hizo za kivita ni katika mpango uliotiwa saini mwaka wa 2010 wa dola hizo milioni 1.3 zinazojumuisha pia ndege 20 za kivita.

Ndege nane zimeshapelekwa nchini Misri tangu mwezi wa Januari nyengine nne zinatarajiwa kufikishwa katika wiki kadhaa zijazo huku nyengine nane zikitarajiwa kupelekwa baadaye mwaka huu.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman