1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yaitisha uchaguzi wa bunge April hii

22 Februari 2013

Rais Mohammed Mursi wa Misri amepitisha kanuni inayoamuru uchaguzi wa bunge uitishwe kuanzia Aprili 27 na kumalizika Juni mwaka huu.

https://p.dw.com/p/17jsK
Rais Mohammed Mursi wa MisriPicha: AP

Awamu ya kwanza ya uchaguzi huo itafanyika katika majimbo matano kati ya 27 ya nchini Hiyo na itadumu siku mbili.Mji mkuu Cairo ni miongoni mwa maeneo ambako awamu hiyo ya kwanza ya uchaguzi wa bunge itafanyika.

Rauni ya nne na ya mwisho itafanyika June 19-20 pakiwepo uwezekano wa duru ya pili ya uchaguzi June 26 hadi 27 mwaka huu.

Kikao cha kwanza cha bunge jipya linatakalokuwa likijulikana kama "Baraza la wabunge" kitaitishwa July sita.

"Uchaguzi utaitishwa kwa awamu tofauti ili kuhakikisha unasimamiwa kikamilifu na majaji kuambatana na katiba",msaidizi wa rais Mursi,Bakinam al Sharqawi amesema kupitia talevisheni ya taifa.

Bunge la Misri lilivunjwa June mwaka 2012 baada ya mahakama kuu ya nchi hiyo kuamua uchaguzi wa mwaka 2011/2012 ubatilishwe kwa hoja kwamba  haulingani na katiba.

Baraza la seneti-Chura,linalodhibiti madaraka ya bunge hadi uchaguzi mkuu utakapoitishwa, limepitisha sheria ya upigaji kura iliyofanyiwa marekebisho-siku tatu baada ya baraza kuu la katiba kusema vifungu vitano vya sheria hiyo iliyotungwa na baraza la Chura linalodhibitiwa na wafuasi wa kiislam-haviambatani na katiba.

Marekebisho ya sheria za kupiga kura yanaambatana na hoja zilizotolewa na korti kuu ya katiba na kuongeza idadi ya viti vya bunge hadi 546 ili kuhakikisha majimbo yote ya nchi hiyo yanawakilishwa kwa usawa na haki.Bunge la awali lilikuwa na viti 498.

Idadi kubwa ya viti hivyo vipya vitakaliwa na wabunge kutoka Cairo na Alexandria.Wapinzani wa Udugu wa kiislam walidai hapo awali kwamba mgawo wa awali wa viti uliyapendelea zaidi maeneo ya vijijini na hasa katika eneo maskini la kusini wanakokutikana wafuasi wengi zaidi wa itikadi kali ya dini ya kiislam.

Kishindo kipo

Ägypten Kairo Proteste
Wakinamama wanalalamikaPicha: Reuters

Kuna wanaoonya kwamba,kwa kupelekewa  sheria hiyo iliyofanyiwa marekebishomoja kwa moja rais Mursi ,badala ya kuirejesha katika korti kuu ya katiba,baraza la shura linakabiliwa na changamoto nyengine mfano wa ile iliyoshuhudiwa hapo awali.

Upande wa upinzani ulitishia kuususia uchaguzi ikiwa serikali inayoungwa mkono na wafuasi wa itikadi kali haitabadilishwa na kuundwa serikali isiyoelemea upande wowote na kama uchaguzi hautasimamiwa na  wanasheria na mashirika yasiyomilikiwa na serikali..

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AP

Mhariri:Josephat Charo