1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mito yafurika Thailand

29 Oktoba 2011

Serikali ya Thailand yawalazimisha wakaazi kuondoka mji mkuu Bangkok

https://p.dw.com/p/131QM
Mwanamume apeleka baiskeli katika barabara iliyojaa maji mjini BangkokPicha: dapd

Mto mkuu mjini Bangkok nchini Thailand umefurika hapo jana na kupasua baadhi ya kingo zake.

Übeschwemmung Thailand Bangkok
Mto Chao Phraya ulioko BangkokPicha: dapd

Wataalamu wanahofia kuwa maji ya mto Chao Phraya huenda yakavuka vizuizi na kujaa katika eneo la biashara la mji huo. Kuta za kuzuia maji zina urefu wa mita 2.5 lakini maji yanatarajiwa kufikia hadi mita 2.6 hii leo.

Barabara nje ya Bangkok zimejaa magari, wakati maelfu ya watu wakiyakimbia mafuriko hayo, ambayo ni mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika nusu karne. Magunia ya mchanga yamewekwa katika majengo mbalimbali mjini humo ili ya kuyakinga dhidi ya maji yanayozidi kufurika.

Serikali imeachilia mbali pendekezo la kuchimba mitaro katika baadhi ya barabara ili kuyatoa maji hayo mashariki mwa Bangkok, fikra ambayo imeungwa mkono na mwenyekiti wa tawi la kampuni ya kutengeneza magari Toyota Thailand, ambae kiwanda chake kimejaa maji.

Akizungumzia athari za mafuriko hayo mshauri mmoja mkuu wa benki ya Bangkok, Ling Hong, alisema kuwa uharibifu uliosababishwa na mafuriko hayo ni pigo kubwa kwa nchi hiyo.

Übeschwemmung Thailand Bangkok
Magunia ya mchanga yamewekwa kuzuia majiPicha: dapd

Alisema uharibifu wa viwanda vitano muhimu ambavyo vilifurika maji katika eneo la kaskazini la Bangkok, umesababisha hasara ya kati ya dola milioni 11.4 hadi milioni 14.7 .

Wakaazi wamekumbana na mamba na nyoka ambao wanaokimbia mashamba yaliofurika. Televisheni nchini humo zinaonyesha msongamano wa magari yaliokuwa yakiondoka mjini humo lakini idara ya trafiki imesema, haikuweza kutoa idadi kamili ya watu wanaouhama mji wa Bangkok, kwani kamera nyingi za barabarani zimefunikwa na maji.

Wizara ya ulinzi imesem, wanajeshi 50,000 walio na maboti 1000 na magari 1000, wapo tayari kusaidia kuhamisha wakaazi. Kituo cha serikali cha kukabiliana na hali za dharura, kimesema hivi karibuni, kutakuwepo vituo vya kuwahamisha wakaazi katika majimbo 8 ambavyo vitaweza kupokea kati ya watu 100,000 na 200,000. Mpaka sasa, janga hilo la mafuriko la miezi mitatu nchini humo, limekuwepo katika majimbo ya kaskazini na ya kati. Takriban watu 400 wameuawa.

Mwandishi: Maryam Abdalla/RTRE/DPA/AFP
Mhariri: Prema Martin