1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Iran inaelekea wapi?

Thelma Mwadzaya4 Januari 2010

Mapambano yaliyozuka barabarani katika miji mingi nchini Iran siku ya kuadhimisha Siku Kuu ya Ashura, yametoa sura mpya kabisa ya mivutano mikali ya kisiasa inayoendelea miongoni mwa wasomi katika Jamhuri hiyo ya Kiislam

https://p.dw.com/p/LKlL
Waandamanaji wa kihafidhina IranPicha: AP

Safari hii si waandamanaji wengi tu walionyesha kuwa wapo tayari kuvikabili vikosi vya usalama, bali hata viongozi wenye misimamo mikali wamedhihirisha kuwa wamepania kungángania ukaidi wao na kukabiliana na waandamanaji kwa kuitisha maandamano yao wenyewe na hata kuzusha uwezekano wa kuzidisha machafuko ya kiraia nchini humo.

Iran Demonstration Pro Regierung
Waandamanaji wanaoiunga mkono serikaliPicha: AP

Ikiwa maafisa wa usalama na viongozi wenye misimamo mikali nchini Iran hawatoshawishiwa kuzingatia mkakati utakaotia maanani baadhi ya madai ya wapinzani hao na kurekebisha ukiukaji mkubwa wa mamlaka uliotokea tangu uchaguzi wa Juni 12, basi mara kwa mara, mwaka huu huenda ukashuhudia mapambano ya barabarani kati ya wananchi. Michafuko kama hiyo inamulika dosari na mkwamo wa kisiasa serikalini hata zaidi ya nguvu zinazotumiwa kuzima machafuko.

Kutumia nguvu

Kukamatwa kwa wanaharakati wa kiraia na wanasiasa wanaogombea mageuzi na hata waandishi wa habari, kufuatia maandamano yaliyofanywa siku takatifu ya Ashura,huonyesha kuwa serikali imeazimia kuzima upinzani kwa kutumia mabavu tu. Hata matamshi makali yaliyotolewa na taasisi zinazodhibitiwa na viongozi wenye misimamo mikali kama vile Baraza la Walinzi, ni ishara kuwa serikali imepania kutumia nguvu badala ya kuzingatia angalao baadhi ya malalamiko ya waandamanaji.

Matukio ya hivi sasa nchini Iran yanakumbusha yale yaliyotokea mwaka 1979, kwani viongozi wa kihafidhina wenye misimamo mikali kwa kweli wanasababisha fikra zinazozidi kuenea hata katika nchi za Magharibi kuwa Iran inapitia mageuzi mengine ambayo hatimae yatamaliza utawala wa serikali ya Kiislamu. Kusimama kidete, kutumia mabavu na kuwapeleka wafuasi wake kuandamana barabarani ni njia zinazotumiwa na viongozi hao kuzuia mapinduzi mengine.

Flash-Galerie Iran Aktion Lichterkette
Maandamano ya kuitaka Iran isitishe kamataPicha: United4Iran

Misimamo ya Kihafidhina

Mapambano yaliyotokea siku ya Ashura yamewapa viongozi hao wenye misimamo mikali ya kihafidhina, nafasi nyingine ya kusisitiza kuwa njia pekee ya kuwajibu wapinzani wenye malengo na vitendo vinavyoelekea kufanana na matakwa ya serikali hasimu za kigeni, ni kuchukua hatua kali na zilizo dhahiri. Hadi sasa vitendo na matamshi ya wanasiasa hao wa kihafidhina yanaonyesha kuwa wao wapo tayari kuitumbukiza Iran katika mzozo wa kiraia badala ya kutafuta suluhisho ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Majuma yajayo yataonyesha iwapo mkakati wa kutumia nguvu utafanikiwa.

Mwandishi: Martin,Prema/IPS

Mhariri: Mtullya, Abdu