1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mivutano yaanza kati ya Marekani na Israel

Charo Josephat/ IPS12 Aprili 2009

Vyama vinavyounda serikali ya Israel vinapinga suluhisho la mataifa mawili

https://p.dw.com/p/HV8K
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wa mambo ya kigeni Avigdor LiebermannPicha: AP/DPA/DW-Grafik

Mikwaruzano kati ya serikali ya Marekani na serikali ya Israel imeanza kujitokeza. Wiki iliyopita imedhihirisha kwamba uhusiano baina ya Marekani na Israel, ambao haukuwa mzuri sana wakati wa utawala wa rais George W Bush, unaonekana kukabiliwa na mawimbi mazito.

Tangu kuingia madarakani takriban majuma mawili yaliyopita, serikali mpya ya Israel inayoungozwa na waziri mkuu Benjamin Netanyahu, imekosolewa na maafisa wa ngazi za juu wa utawala wa Marekani, ikiwa ni pamoja na rais Barack Obama mwenyewe, ingawa ukosoaji huo haujafanywa moja kwa moja kuilekeza serikali hiyo ya Israel.

Hatua nyingine zilizochukuliwa na utawala wa rais Obama katika wiki iliyopita, hususan ahadi ya kushiriki kikamilifu kwenye mazungumzo ya ana kwa ana na Iran kuhusiana na mpango wake wa nyuklia, yamezusha wazo kwamba serikali ya mjini Washington chini ya rais Obama haielewani tena na taifa la kiyahudi la Israel, haswa utawala wake mpya wa siasa za mrengo wa kulia.

Matukio ya hivi punde yametokea wakati utawala wa Marekani ukiwa umezipa kipaumbele juhudi za kukabiliana na hali inayoendelea kuzorota nchini Afghanistan na Pakistan, kama sehemu ya mkakati unaolenga hatimaye kufikia lengo la kuvuruga, kuvunja na kulishinda kundi la kigaidi la al Qaeda. Uratibu wa mkakati huo mpya uliongozwa na Bruce Riedel, afisa wa zamani wa shirika la ujasusi la Marekani, CIA, mchambuzi wa maswala ya Mashariki ya Kati na Asia Kusini, ambaye kwa muda mrefu amesisitiza kwamba kuumaliza mzozo kati ya Israel na Palestina kutasaidia pakubwa kupunguza ushawishi wa kundi la al Qaeda katika eneo hilo.

Wazo hilo linaonekena kuakisi maoni ya maafisa wengine katika utawala wa Marekani, ikiwa ni pamoja na rais Obama mwenyewe, licha ya ushindi wa vyama vya Israel vinavyopinga suluhisho la mataifa mawili katika mzozo kati ya Israel na Palestina. Ingawa kuna shakashaka ikiwa mkataba wa amani utaweza kufikiwa hivi karibuni, viongozi wa Marekani wamesisitiza umuhimu wa kulifikia lengo hilo.

Ukosoaji

Ukosoaji wa kwanza kwa serikali ya waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wiki iliyopita, lilikuwa jibu la hotuba ya waziri wake mpya wa mashauri ya kigeni, Avigdor Lieberman, ambapo alifutilia mbali kujitolea kwa Israel kwenye makubaliano ya mkutano wa mjini Annapolis yalioandaliwa na utawala wa rais wa zamani wa Marekani, George W Bush mnamo mwezi Novemba mwaka 2007. Mkutano huo uliwakutanisha wapatanishi wa Israel na Palestina kujadili msimamo wa mwisho wa suluhisho la mataifa mawili, badala ya kukwamishwa na kutimizwa kwa masharti ya mpango wa amani wa mwaka 2003 wa kufikia lengo hilo.

"Kuna hati moja inayotuunganisha sote, na sio mkutano wa Annapolis. Makubaliano ya Annapolis hayana uhalali," alisema Lieberman, ambaye maoni yake ya kupinga waarabu, yamepata sifa mbaya nchini Marekani.

Obama wirbt für eine atomwaffenfreie Welt in Prag
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: picture-alliance/ dpa

Wakala wa kiyahudi wenye makao yake nchini Marekani umedokeza kuwa jibu la rais Obama lilitolewa haraka na lilitoka kutoka ngazi ya juu ya utawala wake, pamoja na yeye mwenyewe. "Nataka niwe wazi: Marekani inaunga mkono kwa dhati lengo la mataifa mawili, Israel na Palestina, yatakayoishi kwa amani na usalama," alisema rais Obama wakati alipokuwa akilihutubia bunge la Uturuki mjini Ankara. "Hili ni lengo linaloungwa mkono na Wapalestina, Waisraeli na watu wenye nia njema katika mpango wa kutafuta amani na walioshiriki kwenye mkutano wa Annapolis nchini Marekani."

Wachambuzi wamesema hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa rais Obama kuzungumzia wazi makubaliano ya Annapolis tangu alipoapishwa mwezi Januari mwaka huu na hivyo maneno yake yanachukuliwa kama kuikaripia moja kwa moja Israel.

Obama Veepstakes Biden
Makamu wa rais wa Marekani Joe BidenPicha: AP

Ukosoaji wa pili kwa Israel ulitolewa kufuatia matamshi ya waziri mkuu Benjamini Netanyahu katika mahojiano yake na Jeffrey Goldberg wa jarida la The Atlantic. Mahojaino hayo yalidhihirisha azma ya Netanyahu na viongozi wengine wa Israel kutaka kuvishambulia vinu vya nyuklia vya Iran iwapo juhudi za kidplomasia za Marekani kuishawishi Iran kuachana na mpango wake wa nyuklia hazitazaa matunda haraka. Makamu wa rais wa Marekani, Joe Biden, amesema hana uhakika ikiwa Israel inaweza kuchukua hatua hiyo, akisema haitakuwa jambo la busara kuishambulia Iran.