1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mivutano yaendelea Copenhagen.

Halima Nyanza11 Desemba 2009

Mvutano kati ya nchi zilizoendelea kiviwanda na nchi masikini umezidi kuongezeka, katika mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/Kzrr
Lumumba Di-Aping kutoka Sudan, msemaji wa kundi la mataifa yanayoendelea katika mkutano wa Copenhagen.Picha: AP

Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa amelalamika mara kadhaa akisema nchi tajiri zinaonekana kutokua na nia ya dhatia kutoa msaada wa fedha kwa nchi zinazoendelea kuweza kudhibiti uchafuzi wa hali ya hewa.

Katika hali ya kuonesha kutokukubaliana, Msemaji wa kundi la mataifa yanayoendelea la G77, Lumumba Stanislaus Di-Aping amelaumu nchi tajiri kwa kudhoofisha mkutano huo ulioingia katika siku yake ya tano na kukatisha mkutano wake na Mwenyekiti wa Mkutano kutoka nchini Denmark kufuatia upinzani uliotokea usiku wa kuamkia leo, na baadaye aliwalaumu wenyeji kwa kuudhoofisha mkutano huo.

Mataifa masikini katika mkutano huo wa CopenHagen pia yanapinga mipango ya Marekani na Umoja wa Ulaya ya kuzitaka nchi hizo kupunguza viwango maalumu vya moshi unaochafua hali ya hewa.

Mataifa mengi yanayoendelea ndio yameathiriwa vibaya na mabadiliko ya hali ya hewa.

Yvo de Boer ataka makubaliano kamili: Lakini licha ya malumbano yanayotokea katika mkutano huo wa kimataifa wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa, Mkuu wa Kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na Hali ya Hewa Yvo de Boer, anasema makubaliano yatakayofikiwa katika mkutano huo yanapaswa kuwa muafaka.

Anasema anadhani wote wanakubali kwamba matokeo ya mkutano huu lazima yawe wazi kabisa na kwamba lazima ihakikishwe kwamba, hatufikii makubaliano ambayo baadaye yatasababisha tafsiri mbalimbali na maswali.

Aidha anasisitiza kuwa pasiwe na sababu ya kufanyika mazungumzo mengine juu ya kujadili masuala yaliyokwisha kubaliwa.

Yvo de Boer
Mkuu wa Kitengo cha Umoja wa Mataifa, kinachoshughulikia masuala ya Hali ya Hewa, Yvo De Boer.Picha: AP

Wakati huohuo, mataifa yaliyoko katika visiwa vidogo yamesema hayatakubaliana na Mkataba dhaifu utakaofikiwa kuhusiana na hali ya hewa katika mkutano huo wa Denmark, ambao utahatarisha uwepo wao.

Mjumbe kutoka katika visiwa vya Solomon katika jumuia hiyo yenye wanachama 42, Collin Beck amesema wamekuwa wakizungumzia suala hilo la mabadiliko ya hali ya hewa kwa miaka 20 sasa, na kwa bahati mbaya imekuwa ikileta migogoro kadhaa ili kuifanya dunia kuwa makini na hali hiyo.

Kisiwa kidogo cha Tuvalu, kama ilivyo katika kisiwa cha Solomons kilichopo kwenye bahari ya Pasifik, kinahofia pia kufunikwa na maji endapo usawa wa bahari utapanda juu zaidi duniani.

Kwa mujibu wa pendekezo la kisiwa hicho, nchi zinazoinukia zitapaswa kuweka malengo katika kupunguza utoaji wa gesi zinazosababisha kuongezeka kwa joto duniani.

China na India nazo zaweka mikakati yao: Wakati huohuo Waziri Mkuu wa China, We Jiabao na mwenzake wa India Manmohan Singh wamekua na mazungumzo kuhusiana na mkutano huo unaoendelea wa hali ya hewa, huku India ikikamilisha kuandaa msimamo wake katika mkutano huo wa CopenHagen.

Katika mkutano wao huo, viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuwasiliana kwa ukaribu katika mkutano huo wa Denmark.

Viongozi hao wawili wanatarajia kuhudhuria kilele cha mkutano huo Desemba 17 na 18.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa)

Mhariri: Abdul-Rahman