1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mizinga yasikika tena karibu na Goma

Kalyango Siraj7 Novemba 2008

Mapigano yanaripotiwa kuzuka tena leo Ijumaa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

https://p.dw.com/p/FpP4
Mtoto akiwa nje ya nyumba yao iliobomolewa katika mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Picha: AP

Mapigano hayo ni kati ya majeshi ya serikali ya Kinshasa dhidi ya waasi wanaoongozwa na Generali muasi Laurent Nkunda.Yanasemekana kutokea katika maeneo ya umbali wa kilomita 15 kutoka mji wa Goma.

Mapigano haya mapya yasemekana yamezusha hofu miongoni mwa raia wa kawaida mjini Goma.Mwandishi wa habari wa shirika la AFP anasema kuwa maelfu ya wakimbizi walitoroka kambi ya karibu ya Kibati,wakati milio ya risasi ya bunduki za rashasha pamoja na mizinga ilipoanza kusikika huku ndege za Helikopta zikipita juu.

Msemaji wa jeshi la Umoja wa Mataifa Luteni Kanali Jean-Paul Dietrich amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa FARDC,ambalo ni jeshi la serikali ya Kinshasa, limetumia silaha kubwakubwa kutoka Kibati.

Mapigano haya yamekuja huku mkutano wa kikanda ukiwa unafanyika mjini Nairobi nchini Kenya,kujaribu kuhuisha mazungumzo ya kukomesha mapigano na kutafuta njia za kupatikana kwa amani.

Mbali na juhudi hizo lakini taarifa kutoka mashariki mwa Kongo zinatia wasiwasi.

Ukiacha kuzuka tena kwa mapigano kati ya waasi watiifu kwa Laurent Nkunda kuna taarifa kuwa wapiganaji wake wakiwa katika shughuli za safishasafisha baada ya kuwafurusha wanamgambo wa Maimai kutoka mji wa Kiwanja, waliwaua kiholela raia kadhaa.

Mashirika ya habari yanaripoti kuwa zaidi ya watu 20 waliuawa . Shirika linalotetea haki za binadamu la Amnesty International linasema kuwa hayo ni mauji ya halaiki.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inawalaumu wanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Mataifa kinacholinda amani nchini humo cha MONUC kwa kushindwa kuwalinda raia wa nchi hiyo. Msemaji wa rais Joseph Kabila amenukuliwa kusema kuwa watu wanauawa kinyama na MONUC inashindwa kuchukua hatua madhubuti.

Afisa wa ngazi za juu kutoka nchi za magharibi anaehudhuria mkutano wa Nairobi, akigusia mauaji hayo ,amenukuliwa kusema kuwa,hatua zaidi zingechukuliwa.Hata hivyo ametumaini kuwa jeshi la MONUC, lenye wanajeshi wa India, litaweza kumzuia Nkunda kuuteka mji wa Goma, hata bila ya kusaidiwa na vikosi vya serikali.

Moja wa malengo ya mkutano wa Nairobi huo ni kuhimiza marais Paul Kagame wa Rwanda na cheo somo wake Joseph Kabila kutoka Kinshasa kukaa katika meza moja na kuzungumzia mgogoro wa mashariki mwa Kongo.Utawala wa Kabila unaulaumu wa Kigali kwa kuwaunga mkono waasi wa Nkunda madai yanayokanushwa.

Kwa upande wake rais Kagame ameilaumu jamii ya kimataifa kwa kushindwa kushughulikia anachosema ni chanzo cha mgogoro huo,mbali na kumimina madola mengi katika eneo hilo'.Yeye anasema kuwa kiini cha mzozo huo ni kile alichoita 'udhaifu wa utawala wa Kinshasa 'ambao umeshindwa kuwapokonya silaha waasi wa kihutu.

Na hayo yakiendelea mwandishi habari wa kibeligiji anaetumikia gazeti la Ujerumani ambae mapema leo aliripotiwa kutekwa nyara na wapiganaji wa MaiMai hatimae ameachiliwa huru.