1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala wa Televisheni kati ya Merkel na Schulz.

Zainab Aziz
4 Septemba 2017

Mamilioni ya Wajerumani waliutazama mjadala kati ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel na mpinzani wake mkuu Martin Schulz. Mjadala huo uliendeshwa na mashirika manne makubwa ya Televisheni ya hapa nchini Ujerumani. 

https://p.dw.com/p/2jJWZ
TV-Duell Angela Merkel und Martin Schulz
Picha: picture alliance/Dpa/dpa

Mjadala huo kwa kiasi kikubwa ulikuwa ndio fursa ya mwisho kwa viongozi hao ya kuwashawishi  wapiga kura ambao bado hawajaamua ni nani wanayetaka kumpigia kura. Martin Schulz alionekana kuwa na hofu mara mjadala huo wa Televisheni ulipoanza. Kiongozi huyo wa chama cha SPD aliendelea kubadili badili mada na tokea mwanzoni alitumia mkakati wa kuilaumu sera ya uhamiajii ya kansela Merkel na pia  kutoa ahadi kwamba ataichukulia hatua kali Uturuki iwapo atachaguliwa. Martin Schulz hakuweza kumshinda bibi  Merkel katika mjadala uliochukua muda wa dakika 97 ambao ulizingatia  masuala kama vile ya wakimbizi, Uislamu, sera za kigeni, kodi na usalama wa kijamii.

Deutschland TV Duell Merkel Schulz
Kiongozi wa chama cha SPD Martin SchulzPicha: Reuters/F. Bensch
Deutschland TV Duell Merkel Schulz
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/F. Bensch

Kansela Angela alikuwa  mutulivu na alijaribu kuweka muonekano wa  kiongozi mwenye ujuzi ambaye yuko tayari kuiongoza Ujerumani katika nyakati za wasiwasi. Kuhusu Uturuki, Bi Merkel alikubali kuwa ilikuwa muhimu kuweka msimamo mkali dhidi ya Rais Recep Tayyip Erdogan, ambaye serikali yake imewakamata raia wawili Zaidi wa Ujerumani mnamo siku ya Jumamosi iliyopita.

Wagombea wote wawili waliendelea kujadiliana juu ya masuala mengine kwa njia iliyofanana kama walivyojadili juu ya Uturuki. Walikuwa tofauti katika maelezo yao lakini kwa kiasi kikubwa walikubaliana kwenye mambo mengi.

Wote wawili walisema kuwa Ulaya ina jukumu la kimaadili la kuwalinda wahamiaji wanaosafiri kupitia kwenye bahari ya Mediterranea ili wasife maji. Bi Merkel alitetea uamuzi wake wa utata wa kuwasaidia walinzi wa pwani ya Libya katika harakati za kuzuia safari za boti za wakimbizi kwenye pwani ya nchi hiyo. Martin Schulz kwa upande mwingine alitoa wito wa kuanzishwa kwa mfumo mpya wa uhamiaji ambao utawapa wahamiaji hao njia mbadala kuliko safari za hatari katika bahari ya Mediterranea.

Mjadala ulimalizika baada ya dakika 97 bila kuwa na mshindi wa wazi. Uchunguzi wa maoni ya wapiga kura uliofanywa mara baada ya mjadala huo na kituo cha runinga cha ZDF ullionyesha kuwa kansela Merkel alishinda kwa asilimia 32 na mpinzani wake Martin Schulz alipata asilimia 29 na asilimia 39 ya Wajerumani walikuwa hawana uhakika.

Mwandishi: Zainab Aziz/Daniel Pelz

Mhariri:Mohammed  Abdul-Rahman