1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio ya kibaguzi Dresden

Oumilkheir Hamidou
28 Septemba 2016

Mjadala wa kwanza wa televisheni kati ya wagombea wawili wakuu wa kiti cha rais wa Marekani,na mashambulio ya Dresden ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2QgRs
Mgombea wa chama cha Republican Donald TrumpPicha: Getty Images/AFP/W. McNamee

 

Tuanze lakini na mjadala wa televisheni  kati ya wagombea wawili wakuu wa kiti cha rais wa Marekani,Hillary Clinton wa chama cha Democrats na mpinzani wake Donald Trump wa chama cha Republican. Walimwengu wameshusha pumzi anasema mhariri wa  "Emder Zeitung" na kuendelea:"Bila shaka mie sitokuwa wa mwanzo kubonyeza kifungo cha shambulio la kwanza la kinuklea" amesema Donald Trump katika mjadala huo wa televisheni dhidi ya mpinzani wake Hillary Clinton. Eti kweli hatobonyeza? Si haba! Kwasababu kwa bahati mbaya kila mmoja anaamini anaweza !Mjadala huo umedhihirisha kuwa yeye ni mtu dhaifu,haoni makosa yake,hakadiriki,mshari na mwenye kupandisha hasira mara moja. Hoja yake kubwa kwanini anataka kuwa rais wa Marekani eti kwasababu yeye ni "mfanyabiashara  na eti yeye ni tajiri:"Yeye peke yake ndie anaeweza kuwaonyesha wanasiasa jinsi ya kuiongoza nchi kwa ufanisi. Mradi pindi Trump akishinda basi hofu na wasi wasi vitazagaa ulimwenguni.

Mjadala umemkatisha Kiu cha kuania Madaraka Donlald Trump

 "Mittelbayerische Zeitung" linahisi mjadala huo wa televisheni umeziwekea kizuwizi mbio zake kuelekea Ikulu ya Marekani. Gazeti hilo linaendelea kuandika:"Kusema kweli,kasheshe ya New York itavuruga matumaini yake ya kuongoza makadirio ya maoni ya wapiga kura. Chochote kile alichokuwa amekikusudia kimetiwa munda usiku wa jumatatu kuamkia jumanne. Katika kampeni za kawaida za uchaguzi, na baada ya yaliyotokea,basi mhafidhina huyo angestahili kujitoa mashindanoni. Lakini hadi wakati huu hakuna chochote kilichoweza kutajwa kuwa ni cha kawaida katika kampeni hizi za uchaguzi wa rais wa Marekani. Kwanza wahafidhina wasingemuidhinisha mgombea anaeeneza chuki dhidi ya Waislamu na dhidi ya watu wenye asili ya Mexico,mgombea anaewatukana wanawake na kumheshimu Vladimir Putin. Kilichobakia ni kuonya tu dhidi ya kuashiria chochote kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Novemba nane inayokuja.Wiki sita zilizosalia ni kama muda usiokuwa na mwisho katika kampeni za uchaguzi nchini Marekani.

Mashambulio ya kibaguzi Dresden

Mada nyengine iliyomulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani inahusu mashambulio yaliyotokea katika mji wa Dresden. Gazeti la "Westfalenpost" la mjini Hagen linaandika:"Waliofanya mashambulio hayo bado hawajulikani. Lakini haitostaajabisha ikisemwa wanatokea katika kundi la wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia. Shambulio dhidi ya jengo la mikutano ambako rais wa shirikisho alikuwa awakaribishe watu mnamo siku ya kuadhimisha  siku kuu ya muungano wa Ujerumani,Oktoba tatu inayokuja ni hujuma dhidi ya wawakilishi wa ngazi ya juu wa taifa na shambulio dhidi ya msikiti ni ushahidi bayana dhidi ya Waislamu wanaoishi humu nchini."Polisi wa Dresden hawajakosea wanapohoji pengine hisia za chuki dhidi ya wageni ndio chanzo cha mashambulio hayo. Mashambulio hayo yamelengwa dhidi ya shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani,Maadili yake na wananchi wake."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga