1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjane wa Navalny kukutana na mawaziri wa EU

Bruce Amani
19 Februari 2024

Mjane wa kiongozi wa upinzani Urusi Alexei Navalny, Yulia Navalnaya, atazuru Brussels hii leo ambako atakutana na mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya na Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel

https://p.dw.com/p/4cYZQ
Mjane wa Navalny, Yulia Navalnaya
Yulia Navalnaya aliuhutubia mkutano wa usalama wa Munich akiwataka viongozi kumuwajibisha PutinPicha: THOMAS KIENZLE/AFP/Getty Images

Navalny aliyekuwa na umri wa miaka 47 alifariki dunia katika gereza la Arctic Ijumaa wiki iliyopita baada ya kuwa kifungoni kwa zaidi ya miaka mitatu, kifo kilichozusha hasira na shutuma kutoka kwa viongozi wa Magharibina wafuasi wake.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema mwaliko wa Navalnaya unatuma ujumbe mzito wa uungaji mkono kwa wapigania uhuru nchini Urusi na unatoa heshima kwa sifa aliyoiacha Navalny.

Serikali ya Urusi imejaribu kukandamiza matukio ya kuomboleza kifo cha Navalny
Watu 400 wakamatwa Urusi baada ya kifo cha NavalnyPicha: AP/picture alliance

Navalnaya aliuhutubia mkutano wa Usalama wa Munich na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kumuwajibisha kisheria Rais wa Urusi Vladmir Putin.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Italia Antonio Tajani anasema maneno ya Navalnaya "yatatufanya tuhisi tishio ambalo linaelemea raia wa Urusi na kila eneo la Ulaya yetu", ambapo "vurugu, ukatili, na vita vimerejeshwa kwa njia ya aibu na bila uwajibikaji".

Urusi yazima matukio ya kumboleza

Maafisa wa Urusi wamekandamiza matukio ya kumuomboleza mwanasiasa huyo.

Mahakama za Urusi zimewahukumu vifungo vifupi jela watu kadhaa waliokamatwa katika matukio ya kuomboleza kifo cha mkosoaji huyo wa Kremlin. Watu 154 wamefungwa jela kwa hadi siku 14 kwa kukiuka sheria kali za kupinga maandamano Urusi.

Mashirika ya haki yanasema polisi imewakamata zaidi ya watu 400 waliokusanyika katika hafla mbalimbali za kutoa heshima za mwisho kwa Navalny.

Waombolezaji waliweka maua mbele ya ubalozi wa Urusi mjini Berlin
Waombolezaji walijitokeza katika miji mbalimbali UlayaPicha: ANNEGRET HILSE/REUTERS

Lula aonya dhidi ya "uvumi"

Wakati viongozi wengi wa Ulaya wamemlaumu Putinmoja kwa moja au kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja kwa kifo cha Navalny, Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva ametahadharisha dhidi ya kutoa kauli za haraka kuhusu kilichosababisha kifo.

Akizungumza na waandishi habari mjini Addis Ababa alikohudhuria mkutani wa kilele wa Umoja wa Afrika, Lula alisema ni muhimu kuepukana na "uvumi" na kusubiri matokeo ya uchunguzi wa maiti.

Rais huyo wa Brazil amekuwa akikosoa hatua za Marekani na Ulaya kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, akisema Kyiv inapaswa kulaumiwa pia kwa mgogoro huo na kukataa kujiunga na jamii ya kimataifa katika kuiwekea vikwazo Moscow.

Katika miji kadhaa kote Ulaya, wafuasi wa Navalny waliendelea kutoa heshima zao jana. Nchini Ujerumani, watu waliweka mashada ya maua na mishumaa nje ya ubalozi wa Urusi mjini Berlin.

Afp