1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Ghouta wakombolewa na vikosi vya serikali Syria

Mjahida14 Desemba 2015

Duru kutoka jeshi la Syria imesema wanajeshi wameudhibiti tena uwanja wa ndege wa kijeshi na mji uliokuwa karibu, Mashariki mwa mji wa Damascus, miaka mitatu baada ya kushindwa nguvu na makundi ya waasi.

https://p.dw.com/p/1HNCn
Baadhi ya wanajeshi wa Syria
Baadhi ya wanajeshi wa SyriaPicha: Getty Images/AFP/Y. Karwashan

Duru hiyo imesema, jeshi limedhibiti kwa ukamilifu mji wa Marj al-Sultan pamoja na uwanja wake wa ndege Mashariki mwa mji wa Ghouta iliyokuwa ngome ya waasi. Mwezi Novemba mwaka 2012, makundi ya waasi yaliuteka uwanja huo wa ndege ulioko takriban kilomita 15 Mashariki mwa mji wa Damascus.

Kulingana na shirika la uangalizi la haki za binaadamu lililo na makao yake nchini Uingereza, Vikosi vya serikali viliungwa mkono na wapiganaji wanamgambo wa kishia wa Hezbollah katika mapigano ya kuuchukua mji huo.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Rami Abdel Rahman, amesema wanajeshi hao wameudhibiti uwanja wa ndege Jumatatu mchana lakini kwa sasa bado wako katika harakati ya kuudhibiti mji walikobakia baadhi ya waasi. Mkurugenzi huyo amesema operesheni hiyo ya pamoja ya kuukomboa mji wa Marj al-Sultan ilianza mwezi mmoja uliopita na kusababisha mapigano makali pamoja na mashambulizi ya maroketi katika eneo hilo.

Rais Bashar al Assad wa Syria
Rais Bashar al Assad wa SyriaPicha: picture alliance/dpa/Sana Handout

Juhudi za kuwaondoa waasi mjini Ghouta zinaendelea

Rami Abdel Rahman, ameendelea kusema kwamba tukio hilo ni hatua muhimu ya kuimarisha uwepo wa vikosi vya serikali katika kuuzingira mji huo wa Ghouta, na kuuimarisha uwanja huo wa kimataifa wa ndege wa Damascus na barabara zinazoelekea uwanja huo. Vikosi vya serikali vimekuwa vikiuzingira mji wa Mashariki wa Ghouta ambao sehemu kubwa ilikuwa inashikiliwa na waasi wanaompinga rais wa Syria Bashar al Assad.

Jeshi la Syria linashambulia baadhi ya miji katika eneo hilo huku wapiganaji wa upinzani wakirusha maroketi, Magharibi mwa mji huo. Siku ya Jumapili watu 45 waliuwawa katika miji minne ya Mashariki mwa Ghouta na maroketi yaliyokuwa yanarushwa na vikosi vilivyotiifu kwa serikali. Taarifa zimearifu kuwa watu wengine sita waliuwawa kufuatia maroketi yaliorushwa katika maeneo yanayoshikiliwa na serikali.

Serikali ya Syria imeanzisha operesheni ya ardhini kote nchini humo kwa usaidizi wa wanamgambo wanaoiunga mkono serikali pamoja na ndege za kivita za Urusi. Mgogoro nchini Syria ulianza wakati wa maandamano ya kuipinga serikali mwezi Machi mwaka 2011 lakini baadaye ukageuka kuwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyosababisha mauaji ya watu 250,000 na kuwalazimu mamilioni ya wengine kuikimbia nchi hiyo.

Mwandishi : Amina Abubakar

Mhariri: Daniel Gakuba