1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Koblenz kuhamisha maelfu ya wakaazi wake

Mohammed Khelef3 Desemba 2011

Mji wa Koblenz ulio kusini magharibi mwa Ujerumani unajiandaa kuwahamisha maelfu ya wakaazi wake hapo kesho (04.12.2011), baada ya kugunduliwa kwa bomu lenye uzito wa takribani tani mbili kwenye mto Rhine.

https://p.dw.com/p/13Lxi
Bomu la "Blockbuster" lililogunduliwa kwenye Mto Rhine.
Bomu la "Blockbuster" lililogunduliwa kwenye Mto Rhine.Picha: picture alliance/dpa

Uhamishaji huu ambao ni mkubwa kabisa kuwahi kutokezea tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, utawahusu watu 45,000, ambao ni takribani nusu ya wakaazi wa Koblenz. Miongoni mwao ni familia zilizo kwenye nyumba zao, wagonjwa walio hospitalini, wazee walio kwenye vituo maalum vya kuwahudumia na wafungwa walioko kwenye majengo ya jela hapo kesho.

Mvua isiyotegemewa katika mwezi uliopita ilisaidia kulibainisha bomu hilo linaloitwa "Blockbuster" kutoka kikosi cha jeshi la anga cha Uingereza. Bomu hilo lilikuwa na nguvu ya kuuharibu mji mzima. Bwawa limejengwa kuzunguka bomu hilo ili kurahisisha operesheni ya kulitegua hapo kesho.