1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa Marekani Mitchell ziarani Mashariki ya Kati

C.Hennen - (P.Martin)25 Februari 2009

Mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati George Mitchell anafanya ziara yake ya pili katika kanda hiyo katika juhudi ya kufufua majadiliano ya amani kati ya Waisraeli na Wapalestina.

https://p.dw.com/p/H0tV
Former Senate Majority Leader George Mitchell addresses the media at a news conference in New York to announce the results of his 20-month investigation into performance-enhancing drugs by Major League Baseball players, 12 December 2007. EPA/JASON SZENES +++(c) dpa - Report+++
George Mitchell,mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati.Picha: picture-alliance/ dpa

Rais wa Marekani Barack Obama siku chache tu baada ya kuingia madarakani,aliarifu kuwa Washington itajitahidi kutafuta suluhisho la amani litakalodumu kati ya Waisraeli na Wapalestina. Hilo ni lengo lake licha ya hali ya mambo kuwa ngumu zaidi kufuatia mashambulio ya Israel katika Ukanda wa Gaza.Na atakaesaidia kutimiza lengo hilo ni George Mitchell aliechaguliwa na Obama kama mjumbe maalum wa serikali ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.Kwa kuchukua hatua hiyo Obama aliashiria umuhimu unaotolewa na serikali yake kwa mgogoro wa kanda hiyo. Alisema:

"Itakuwa sera ya serikali yangu kushughulikia kwa dhati jitahada za kupata suluhisho la amani litakalodumu kati ya Israel na Wapalestina na pia kati ya Israel na majirani wake wa Kiarabu."

Baada ya kuchaguliwa kwa Mitchell,Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton alisema,Mitchell ataongoza jitahada za kufufua majadiliano ya amani kati ya Israel na majirani wake.Atasaidia kupanga mkakati utakaohifadhi usalama wa Israel na kumaliza mgogoro wa Waisraeli na Wapalestina - ili kupatikane mataifa mawili jirani yatakayoishi kwa amani na usalama.

Mdemokrat George Mitchell alie na miaka 75 anasifika kama mpatanishi stadi hata katika hali ngumu bila ya kuelemea upande wo wote.Mwishoni mwa miaka ya 90,vipaji hivyo vilimsaidia Mitchell,kama mjumbe wa rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, kumaliza mgogoro wa Ireland ya Kaskazini uliosababisha umwagaji mkubwa wa damu miongoni mwa Wakatoliki na Waprotestanti.

Mitchell,wakati wa ziara yake hii ataungana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton nchini Misri tarehe 2 mwezi Machi kushiriki katika mkutano wa wafadhili wa Gaza.Ziara yake inafanywa yakiwepo makubaliano tete ya kuweka chini silaha katika Ukingo wa Gaza,unaodhibitiwa na Hamas.Makubaliano yaliyoingia kazini Januari 18 yalisitisha mashambulio makali ya Israel katika Gaza.Mashambulio hayo ya siku 22 yalisababisha vifo vya Wapalestina 1,330.

Wakati wa ziara hii ya pili,Mitchell anakwenda Uturuki,Umoja wa Falme za Kiarabu,Misri,Israel na Ukingo wa Magharibi.