1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa Umoja wa mataifa afukuzwa Zimbabwe

29 Oktoba 2009
https://p.dw.com/p/KIRy
Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa Manfred .Picha: AP

Wakati serikali ya Zimbabwe ikionesha dalili za kutaka kuwa na uhusiano mwema na mataifa ya kimagharibi, ili kuchochea misaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa katika kujaribu kuujenga upya uchumi wake ulioporomoka vibaya, tayari nchi hiyo imeiingia katika mvutano mwingine na Umoja wa Mataifa, baada ya mjumbe wa Umoja huo kufukuzwa nchini Zimbabwe.

Mjumbe huyo Manferd Nowak, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya haki za binaadamu, ameondoka nchini humo leo na kuelekea Afrika Kusini, baada ya kuzuiwa kuingia nchini humo, ambako alitakiwa kufanya uchunguzi juu ya tuhuma za vitendo vya mateso kwa raia wa nchi hiyo, vinavyodaiwa kufanywa na vikosi vya ulinzi.

Mvutano wa kidiplomasia kati ya Zimbabwe na Umoja wa Mataifa, sasa unaelekea kukua zaidi, kufuatia kushikiliwa kwa Bw. Nowak na maafisa wa uhamiaji katika uwanja wa ndege wa Harare jana jioni, na kumuamuru kuondoka nchini humo na ndege ya kwanza ya leo asubuhi.

Akizungumza na Shirika la Habari la Ujerumani DPA, kutoka katika uwanja wa ndege wa Harare, Nowak alisema amekasirishwa sana na kitendo cha kushikiriwa na maafisa hao usiku mzima, na kuongeza kuwa tukio hilo ni la udharirishaji mkubwa dhidi ya diplomasia, ambalo hajahi kukutana nalo katika nchi yoyote duniani.

Tukio hilo ambalo linagongana na uhusiano unaozidi kulegalega kati viongozi wa serikali ya mseto ya nchi hiyo, Rais Robert Mugabe na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai, linaonekana kutazamwa sana, hasa kwa kuzingatia kwamba Nowak alialikwa na serikali ya Zimbabwe.

Waziri wa Sheria wa nchi hiyo Patrick Chinamasa, aliusogeza mbele zaidi mwaliko wa Bw. Nowak tangu mapema mwezi Februari, baada kuripotiwa matukio mengi ya utesaji yanayofanywa na vikosi vya ulinzi vya rais Mugabe.

Lakini katika dakika za mwisho za kuwasili kwa mjumbe huyo, Waziri wa Mambo ya Kigeni ambaye yuko chini ya chama cha Rais Mugabe cha Zanu-PF, alitangaza kusitishwa kwa mwaliko wa Nowak.

Serikali ya nchi hiyo imetoa sababu ya kusitishwa kwa mwaliko huo kuwa, ni ziara inayofanywa na mawaziri watatu wa mambo ya nje, kutoka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ambayo inajaribu kusuluhisha mvutano katika serikali hiyo ya mseto.

Serikali hiyo ya mpito yenye muda wa miezi minane sasa, ipo katika mgogoro baada ya chama MDC kinachoongozwa na Bw. Morgan Tsvangirai, kususia mikutano yote ya serikali hiyo, wiki mbili zilizopita.

Chama hicho kinaituhumu Zanu-PF kwa kushindwa kutekeleza upande wake mpango huo wa serikali ya mseto, kwa kuzuia baadhi ya marekebisho muhimu. Lazaro Matalange anayo zaidi..........

Manfred Nowak ameitaka serikali ya nchi hiyo itoe maelezo ya kina juu ya hatua yake ya kumfukuza, akidai kwamba mkutano wa mawaziri hao ni wa siku moja tu, wakati uchunguzi wake ulitakiwa ufanyike kwa muda wa wiki moja.

Katika ratiba yake, mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa, alipangiwa kukutana na Bw. Tsvangirai, ambaye ofisi yake ndiyo iliyoidhinisha mwaliko huo, ambao umeshindikana.

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu mjini Geneva, anapofanyia kazi Nowak, imesema ziara ya mjumbe huyo ilikuwa muhimu sana, kufuatia kuwepo kwa kampeni mpya za vitisho dhidi ya wakosoaji wa Rais Mugabe.

Mwandishi:Lazaro Matalange/DPA/RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman