1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kukutana tena na kiongozi wa waasi nchni Congo

Mohamed Dahman29 Novemba 2008

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa leo amewasili Goma kwa mazungumzo na kiongozi wa waasi Laurent Nkunda katika jaribio la kukomesha mzozo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

https://p.dw.com/p/G5yL
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa mzozo wa Congo Oluseguni Obasanjo.Picha: dpa

Olusegun Obasanjo ambaye alikuwa na mazungumzo na Rais Joseph Kabila mjini Kinshasa hapo jana alikuwa anatarajiwa kuondoka kwa helikopta kutoka Goma kuelekea kwenye eneo la Rutshuru linaloshikiliwa na waasi kwa ajili ya mkutano wake huo na Nkunda.Obasanjo amewaambia waandishi wa habari mjini Goma kwamba anataka kumueleza Nkunda juu ya kile kilichofanyika tokea akutane naye mara ya mwisho.

Rais huyo wa zamani wa Nigeria anaandamana na rais mwengine wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa ambaye anauwakilisha Umoja wa Afrika.Mkpa amasema anataka kumpima Nkunda ambaye anadai kuwahami Watutsi walio wachache mashariki mwa jimbo la Kivu Kaskazini.Amesema anataka kumsikiliza anafikiria nini juu ya kurudisha amani,utulivu na umoja nchini Congo.

Hapo jana Mkapa amekataa kuzungumzia kwa ukamilifu mazungumzo ya wajumbe hao na Kabila lakini amedokeza kwamba sio rahisi kwa Nkunda kutimiziwa adai lake la kukutana moja kwa moja na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.