1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkasa wa mauaji Ufaransa wamalizika

10 Januari 2015

Majeshi ya usalama nchini Ufaransa, Ijumaa (09.01.2015)yakitumia mabomu na bunduki yalifikisha mwisho siku tatu za ugaidi mjini Paris, wakiwauwa ndugu wawili wenye mahusiano na kundi la al-Qaeda.

https://p.dw.com/p/1EIFr
Schießerei und Geiselnahme in Pariser Supermarkt 09.01.2014
Mapambano katika duka kuwasalimisha matekaPicha: A. Antoniol/Getty Images

Ndugu hao walifanya mauaji ya watu 12 katika jarida la vikatuni vya dhihaka la Charlie Hebdo na mtu mwingine ambaye alishiriki katika mauaji hayo aliwakamata mateka watu kadhaa katika duka la Wayahudi akijaribu kuwasaidia ndugu hao kutoroka.

Ghasia mbaya kabisa za kigaidi nchini Ufaransa kuonekana kwa miongo kadhaa zimesababisha kuuwawa kwa kiasi ya watu 20, ikiwa ni pamoja na watu hao watatu waliokuwa na silaha. Mshukiwa na nne, mke wa mtu aliyeshambulia katika eneo la soko, bado anatafutwa na anaaminika kuwa ana silaha.

Schießerei und Geiselnahme in Pariser Supermarkt 09.01.2014
Msako kuwatafuta magaidi mjini ParisPicha: A. Antoniol/Getty Images

Al-Qaeda walishiriki kupanga mashambulizi

Tawi la al-Qaeda nchini Yemen limesema limeongoza shambulio hilo dhidi ya jarida hilo la Charlie Hebdo kulipza kisasi kwa heshima ya mtume Mohammad, ikiwa ni lengo la mara kwa mara dhidi ya jarida hilo la kila wiki la dhihaka.

Ndugu hao walikuwa wanafahamika na maafisa: Mmoja alikuwa amehukumiwa kwa makosa ya kigaidi kwa kuwa na mahusiano na mtandao unaowatuma wapiganaji kupambana na majeshi ya Marekani nchini Iraq, na wote walikuwa katika orodha ya Marekani ya kutoruhusiwa kusafiri katika ndege, kwa mujibu wa afisa wa Marekani.

Rais Francois Hollande amelitaka taifa lake kuendelea kuwa na umoja na kujilinda, na mji umefunga kitongoji kimoja maarufu cha Wayahudi kutokana na hofu ya ghasia zaidi.

Frankreich Anschlag auf Charlie Hebdo Fahndung Polizei Dammartin-en-Goele
Wanajeshi wakiwasaka magaidi mjini ParisPicha: C. Furlong/Getty Images

"Kitisho kinachoikabili Ufaransa bado hakijamalizika," Hollande amesema. "Sisi ni watu huru na hatuwezi kupiga magoti kutokana na mbinyo."

Mkasa huo , ambao ulioneshwa katika televisheni moja kwa moja na katika mitandao ya kijamii, ulianza wakati ndugu wawili Said na Cherif Kouachi walipowauwa watu 12 siku ya Jumatano katika ofisi za jarida la Charlie Hebdo, wakimpiga risasi polisi ambaye alikuwa amejeruhiwa kichwani kabla ya kukimbia kwa kutumia gari.

Utekaji nyara

Siku ya Alhamis, mtu mmoja mwenye silaha ambaye alitambuliwa na polisi kuwa Amedy Coulibaly alimpiga risasi polisi mwanamke na kufariki kusini mwa mji wa Paris, licha ya kuwa maafisa hawakuwa na hakika mwanzoni kuwa shambulio hilo lilihusika na mashambulizi dhidi ya ofisi za Charlie Hebdo.

Mkasa huo ulimalizika jioni ya Ijumaa (09.01.2015) kwa mashambulizi karibu kama hayo katika maeneo mawili: Kiwanda cha uchapishaji katika mji wa Dammartin-en-Goele, kaskazini mashariki mwa Paris, ambako ndugu hao wawili Kouachi walikuwa wamejificha, na katika dula mjini Paris, ambako Coulibaly amewauwa mateka wanne na kutishia kufanya mauaji zaidi hadi pale polisi watakapowaachia huru ndugu wawili Kouachi.

Wakati wanajeshi waliovalia sare nyeusi walipozingira maeneo yote hayo mawili, miripuko ilisikika, milio ya bunduki na moshi mkuzbwa ulionekana kutoka na kuashiria taarifa kuwa matukio hayo mawili ya utekaji nyara yamemalizika.

Schießerei und Geiselnahme in Pariser Supermarkt 09.01.2014 Verdächtige
Mmoja kati ya magaidi aliyeuwawa Coulibaly (kushoto) na msichana anayesakwa badoPicha: picture-alliance/French Police/Handout

Marekani yaonesha mshikamano na Ufaransa

Rais Barack Obama ameeleza kuiunga mkono Ufaransa jana Ijumaa baada ya utekaji nyara na umwagaji wa damu kumalizika mjini Paris, akiapa kutoa usaidizi kupambana na kitisho cha wanamgambo wa Kiislamu.

"Nataka watu wa Ufaransa watambue kuwa Marekani inasimama pamoja nanyi leo, itasimama pamoja nanyi kesho," Obama amesema wakati akizungumza mjini Tennessee, akiieleza Ufaransa kuwa "mshirika mkongwe" wa Marekani.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry ametoa heshima zake kwa wahanga na kuwapongeza wanajeshi Ijumaa jioni katika ubalozi wa Ufaransa nchini Marekani , ambako alitia saini kitabu cha maombolezi.

Reaktionen auf Anschläge in Frankreich Obama
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: AFP/Getty Images/Mandel Ngan

Katika ziara ya ghafla katika ubalozi huo siku moja kabla, Obama ametia saini na kuandika "Vive la France", idumu Ufaransa.

Kesho Jumapili kutakuwa na mkusanyiko mkubwa mjini Paris kuwakumbuka wahanga wa shambulio hilo ambapo viongozi kadhaa watahudhuria.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Sudi Mnette