1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba mpya wa uhusiano baina Umoja wa Ulaya na Urusi

27 Mei 2008

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wameidhinisha paweko na mazungumzo juu ya mkataba wa ushirikiano mpya na Urusi inayozidi sio tu kuwa tajiri lakini kuwa na ushawishi mkubwa.

https://p.dw.com/p/E6n8

Mawaziri hao wa mambo ya nchi za nje wa umoja wa ulaya walimaliza kikao chao jana usiku mjini Brussels na kukubaliana kwamba mazungumzo kuhusu mkataba mpya yaanzishwe rasmi wakati wa mkutano wa kilele wa viongozi wakuu wa umoja wa Ulaya na Urusi utakaofanyika Siberia tarehe 26 na 27 mwezi ujao wa Juni, pale Rais mpya wa Urusi Dmitry Medvedev atakapoiwakilisha nchi yake katika mkutano wa aina hiyo kwa mara ya kwanza.

Mkuu wa sera ya mambo ya nchi za nje wa umoja wa Ulaya Javier Solana alisema mazungumzo hayo yatazinufaisha pande zote mbili, akiongeza " unapokua na jirani ambaye ni jirani muhimu ambaye tuna biashara kubwa ya bidhaa na nishati naye pamoja na mambo mengine mengi, basi ni vyema kuwa na uhusiano imara na wa msingi kwa miaka mingi."

Umoja wa Ulaya umekua ukijaribu kuimarisha mkataba uliopo sasa katika ushirikiano wake na Urusi ambao ni wa zaidi ya muongo mmoja, kwa kuzingatia hali halisi ya wakati huu kijiongrafia na kiuchumi nchini Urusi.

Aidha majadiliano mapya na Urusi yanalengwa katika kuimarisha pia uhusiano uliozorota wakati wa utawala wa rais wa zamani Valadimir Putin ambaye sasa ni waziri mkuu, pamoja na kuhakikisha nchi za umoja huo zinapata nishati kutoka Urusi bila ya usumbufu. Kadhalika uhisiano mpya una lengwa katika kutathimini suala la haki za binaadamu.

Nchi za ulaya zimezidi kuwa na wasi wasi juu ya kutegegemea nishati kutoka Urusi pamoja na uwezo wa Urusi kuitumia hali hiyo katika kutimiza mbinu zake za kisiasa.

Sambamba na hayo pande hizo mbili zina tafauti za kisiasa kuhusiana na Kosovo, Georgia pamoja na mipango ya Marekani ya kuweka mtambo wa kinga dhidi ya makombora katika bara la Ulaya.

Paia panazungumziwa haja ya kuimarishwa ushirikiano na mataifa mengine ya mashariki kama, Ukraine, Belaruss na Moldavia na kuhakikisha kuna utulifu wa kisiasa na kiuchumi katika mataifa hayo.

Mkutano wa kilele kati ya umoja wa Ulaya na Urusi hufanyika kila baada ya miaka miwili, lakini mkataba wa ushirikiano wa pamoja unatokana na makubaliano ya 1997 wakati Urusi ilipokua bado ikijikongoja kutokana na masalio ya Muungano wa kisovieti uliosambaratika.

Bw Eneko Landaburu atakayeuongoza ujumbe wa umoja wa Ulaya katika mazungumzo na Urusi amesisitiza kwamba mbali na masuala ya nishati na kisiasa, suala la haki za binaadamu litakuwemo katika ajenda ya mazungumzo.