1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa Lisbon wasitishwa na mahakama nchini Ujerumani.

Sekione Kitojo30 Juni 2009

Mahakama nchini Ujerumani imeamuru kuwa mkataba wa Lisbon wa umoja wa Ulaya hauendi kinyume na katiba ya Ujerumani lakini bunge linapaswa kuimarishwa wajibu wake kabla ya kuidhinishwa mkataba huo.

https://p.dw.com/p/IeMG
Mwenyekiti wa chama cha Die Linke Oskar Lafontaine, ambapo chama chake ni sehemu ya upinzani dhidi ya mkataba huo wa Lisbon.Picha: AP

Mahakama nchini Ujerumani imeamua leo Jumanne kuwa mkataba wa Lisbon wa umoja wa Ulaya unaendana na sheria za Ujerumani , lakini imesema pia kuwa wajibu wa bunge unapaswa kuimarishwa kabla ya kuidhinishwa rasmi.

Wakati huo huo rais wa halmashauri ya umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso ameeleza imani yake kuwa mkataba huo wa mageuzi katika umoja wa Ulaya utaidhinishwa na mataifa wanachama wa umoja huo hadi ifikapo majira ya mapukutiko mwaka huu, licha ya uamuzi wa mahakama nchini Ujerumani wa kusitishwa kwa muda mkataba huo.


Wapinzani nchini Ujerumani dhidi ya mkataba huo , ambao umepangwa kupunguza uendeshaji na utoaji maamuzi katika umoja wa Ulaya, wameupinga katika mktaba huo katika mahakama ya katiba, wakidai kuwa waraka huo unakwenda kinyume na uhuru wa taifa hilo.

Mabaraza yote ya bunge la Ujerumani yameuidhinisha mkataba huo, ambao ulitiwa saini na viongozi wa umoja wa Ulaya mwaka 2007. Lakini rais Horst Koehler alijizuwia kutia saini yake akisubiri uamuzi wa mahakama hiyo ya katiba.Makamu wa rais wa mahakama hiyo ya katiba Andreas Vosskuhle amesema kuwa uidhinishaji wa mkataba huo wa Lisbon utakamilika baada ya kuimarishwa kwa jukumu la bunge la kila nchi.

Katiba haina matatizo kwa mkataba huo wa Lisbon, lakini unataka kuimarishwa kwa majukumu ya bunge katika kiwango cha taifa.


Mahakama inamatumaini kuwa kikwazo cha mwisho kitakuwa kimekiukwa kabla ya kuidhinishwa kwa mkataba huo.

Kutokana na uamuzi huo wa mahakama bunge la Ujerumani, Bundestag , limekubali kukutana mwezi August kutunga sheria inayolipa bunge la Ujerumani madaraka zaidi katika masuala yanayohusiana na umoja wa Ulaya.

Muswada huo utasomwa tena mara ya pili kabla ya tarehe 8, mwezi wa Septemba, ikiwa ni wiki mbili kabla taifa hili kufanya uchaguzi mkuu hapo Septemba 27.

Kansela Angela Merkel amesema kuwa anamatumaini kuwa hatua za uidhinishaji zitakamilika kabla ya uchaguzi mkuu. Upinzani dhidi ya mkataba huo kisheria ulianzishwa na wabunge zaidi 50, miongoni mwao akiwemo Peter Gauweiler kutoka chama cha CSU chama ndugu cha kansela Angela Merkel cha CDU.

Chama cha mrengo wa shoto cha Die Linke pia kimeupinga mkataba huo kikidai kuwa unakwenda kinyume na haki za bunge.

Rais wa halmashauri ya umoja wa Ulaya Jose manuel Barroso amesema katika taarifa baada ya uamuzi wa mahakama kuwa anaukaribisha uamuzi huo wa mahakama ya katiba nchini Ujerumani, na kwamba unathibitisha kuwa mkataba huo wa Lisbon haukiuki katiba ya Ujerumani.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Sweden Carl Bildt , ambaye nchi yake inakuwa rais wa umoja wa Ulaya kuanzia kesho tarehe mosi Julai, pia amesema kuwa hana wasi wasi juu ya uamuzi huo wa mahakama ya Ujerumani.


Mwandishi Sekione Kitojo/AFPE/DPAE


Mhariri Mohammed Abdul Rahman.