1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa Schegen una wanachama 24 hivi sasa

Oummilkheir21 Desemba 2007

Wananchi wa ulaya washerehekea uhuru wa kutembeleana bila ya pingamizi

https://p.dw.com/p/Cedg
Ramani ya nchi za SchengenPicha: AP GraphicsBank

Mkataba wa Schengen umepanuka na kujivunia wanachama 24 kuanzia saa sita za usiku jana kuamkia leo.Wakaazi milioni 400 wako huru hivi sasa kuingia na kutoka kati ya mashariki na magharibi ya Ulaya,kupitia Norway katika pembe ya kaskazini hadi kufikia Ureno pembe ya kusini ya bara kongwe.

Fash fash zimefyetuliwa hewani katika vituo mbali mbali vya mpakani huko Berg-Petrzalka,kati ya Austria na Slovakia,au katika kituo cha Zittau-Hradek nad Nisou kinachopiunganisha Ujerumani na jamhuri ya Tcheki ambako umati wa watu walikusanyika na kushangiria bila ya baridi kali iliyoko.

Kote katika eneo la Ulaya ya kati,maafisa wa forodha waliondowa vizuwizi vya mpakani kabla ya kufungua chupa za Champagne kuadhimisha siku hii ambayo nchi za mashariki zinaiangalia kama awamu ya mwisho ya kukongolewa pazia la chuma.

Huko Cesky Tesin-Cieszyn,katika mpaka kati ya jamahuri ya Tcheki na Poland supu na nyama za kuchoma zilitolewa kuwatunukia wananchi.

Huko Berg-Petrzalka,katika wakati ambapo peremende zilikua zikitawanywa na nyimbo ya furaha ya Beethoven kuhanikiza,taa za barabarani zilibadilishjwa klwa muda na kusalia kijani tuu.

Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya José Manuel Barroso anasema

“”Kuanzia December 21, mipaka ya ndani ya mataifa 24 itakua wazi na watu kutembeleana watakavyo.Huu ni ufanisi wa aina yake wa kihistoria.Hatua ya kuondolewa mipaka ya ndani inawafungulia fursa mpya kabisa watu wote wanaoishi katika nchi zetu hizi,wanaweza kuingia na kutoka wakutakako,na kufanya biashara zao.Ndio maana nnaamini kua hii ni hatua muhimu kabisa kwa umoja mpana wa Ulaya.”

“Hakuna yeyote atakaekaguliwa,safari ni huru ndani ya nchi za Ulaya” amesema kwa upande wake waziri wa mambo ya ndani wa Slovakia Robert Kalinak huku akishangiriwa na wananchi.

“Karibuni Schengenland” amemjibu kwa upande wake meya wa kijiji cha Luxembourg-Schengen,Roger Weber, yalikotiwa saini makubaliano ya kuacha wazi mipaka ya nchi za Umoja wa ulaya mnamo mwaka 1985.

Nchi nane za kikokoministi za zamani zilizojiunga na umoja wa ulaya mnamo mwaka 2004-Estonia,Latvia,Lithuania,Hungary,Poland,Slovakia,Slovenia, na jamhuri ya Tcheki,zimeondowa mipaka iliyokuwepo pamoja na nchi nyengine za ulaya,huku kisiwa cha Malta kikifuta pingamizi zilizowekewa vivukio vyote kuelekea bandari za Umoja wa ulaya.

Leo asubuhi viongozi wa Umoja wa ulaya wanatazamiwa kuongozana na kuitembelea mipaka iliyokongolewa.March 30 ijayo,itakua zamu ya viwanja vya ndege vya nchi tisaa zilizijiunga na makubaliano ya Schengen,kuacha wazi mipaka .

Pamehitajika miezi kadhaa ya maandalizi ya kina kusimamia mfumo wa viza ya aina moja,kutia njiani daftari kwa njia ya internet maarufu kama SIS,linalokusanya maelezo kuhusu watu wote wanaoshukuiwa na visa vya uhalifu,kuanzisha ukaguzi nwa pamoja na kulinda kilomita elfu tisaa za mipaka mipya dhidi ya wahalifu na wahamiaji wa kichini chini.