1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa ushirikiano kati ya BICC na EASBRICOM

Nijimbere, Gregoire13 Juni 2008

Shirika la kimataifa linalohusika na kuisuluhisha mizozo na kudumisha amani la BICC, limesaini mkataba wa ushirikiano na idara ya kuratibu shughuli za kikosi tayari kuingilia kati mizozo Afrika ya mashariki EASBRICOM

https://p.dw.com/p/EJMd
Barabara ya mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa, makao makuu ya EASBRICOMPicha: AP

Kikosi hicho cha EASBRICOM kitakuwa na askari jeshi ambao watajumuika katika kile kilichotajwa Eastern Africa Standby Brigade ama EASBRIG yaani kikosi cha kijeshi cha Afrika ya mashariki tayari kuingilia kati mizozo, kutakuwa pia askari polisi pamoja na wafanyakazi wengine watakaosaidia kufanikisha shughuli za kikosi hicho cha kijeshi.

Kikosi hicho kiliundwa mwaka jana tu na kinahitaji watu, mafunzo na fedha.

Shirika la kimataifa la BICC linalohusika na kuisuluhisha mizozo na kudumisha amani lenye makao yake hapa Bonn Ujerumani, tayari limekubali kushirikiana na kikosi hicho kwa kutoa mafunzo yanayohitajika katika kudhaminia amani. Hayo ni katika mkataba wa ushirikiano ambao umesainiwa hapa mjini Bonn.

Peter Marwa mkuu wa idara inayohusika na maswala ya kisiasa katika kikosi cha Afrika ya mashariki cha kuingilia kati mizozo EASBRICOM, amesema wameliomba BICC kuwasaidia kwa sababu lina ujuzi wa kutosha katika maswala hayo.


Mkurugenzi wa BICC Peter Croll, amesema malengo ya kikosi hicho cha Afrika ya mashariki yanakwenda sambamba na shughuli za shirika la BICC ambalo lingependa litowe mchango wake katika kufanikisha malengo hayo ya kudhaminia amani.

Kikosi hicho maalum cha kijeshi katika kanda ya Afrika ya mashariki kitakuwa cha 6 cha aina hiyo kuundwa barani Afrika, mfano wa ECOAS katika kanda ya Afrika magharibi. Nchi 13 wanachama ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Sudan, Rwanda, Mauritius, Madagascar, Eritrea, Ethiopia, Djibuti, Ushelisheli, Somalia, Tanzania na Burundi zitachangia kwa wanajeshi, vifaa na hatimae fedha kwani Shirika la BICC tayari limesema sio mfadhili.