1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkenya auza bidhaa zilizotengenezwa kwa mikono katika soko la Krismasi Ujerumani

19 Desemba 2011

Wajerumani hupenda kununua zawadi za Krismasi katika masoko maalum yanayouza bidhaa mbalimbali. Kutana na Mkenya anauza vifaa vilivyotengenezwa kwa mkono katika soko mojawapo.

https://p.dw.com/p/13Vi7
Timothy Matia
Timothy Matia kutoka KenyaPicha: DW

Timothy Matia ni kijana mwenye umri wa miaka 31 kutoka Mkoa wa Mashariki, nchini Kenya. Kwa kawaida Timothy huishi Kenya lakini mara mbili kwa mwaka huja Ulaya kwa ajili ya kuuza bidhaa zilizotengenezwa kwa mkono kutoka nchini mwake. Katika mwezi huu, Timothy anauza bidhaa hizo katika kibanda chake kilichopo kwenye soko maalum la kuuzia vitu vya Krismasi, lililopo mjini Cologne, Ujerumani.

Masoko ya Krismasi, ambayo hujulikana kama Weihnachtsmarkt, hufunguliwa wiki chache kabla ya Krismasi katika sehemu mbalimbali za miji na vijiji. Katika masoko hayo huuzwa hasa bidhaa zilizotengenezwa kwa mkono pamoja na vyakula na vinywaji mbalimbali. Masoko hayo huwa yamepambwa kwa taa mbalimbali na hupendeza sana hasa wakati wa usiku. Vinyago, hereni, bangili na vijiko vya kupakulia ni baadhi tu ya vitu ambavyo Timothy anaviuza katika kibanda chake. Yeye anaeleza ni bidhaa gani, ambazo wateja wake wanazipenda zaidi.

"Wanapenda sana hivi vipuli vya mkono, bangili na hata 'salad spoon' za kutumia nyumbani. Wanapenda pia twiga na haya mawe madogo madogo," anasema Timothy.

Baadhi ya bidhaa anazouza Timothy
Baadhi ya bidhaa anazouza TimothyPicha: DW

Timothy anaeleza pia kwamba wateja wake wanaonyesha kupenda kufahamu zaidi kuhusu bidhaa zake na hivyo humuuliza zimetokea wapi, zimetengenezwaje na kama zina maana yoyote ya kiutamaduni.

Mkenya huyo alikuja Ujerumani kwa mara ya kwanza mwaka 2009. Kabla ya hapo alikuwa akiuza bidhaa zake katika miji mbali mbali huko Uholanzi, Ureno na hata Uhispania. Timothy anaeleza ni kwa nini aliamua kuacha kuuza katika nchi hizo na kuja kutafuta soko jipya huku Ujerumani.

"Nilialikwa hapa na rafiki yangu. kabla ya hapo nilikuwa nikifanya kazi Uhispania na Ureno," anasema Timothy. "Hali ya uchumi ulipokwenda chini niliona ni vizuri nibadilishe 'site' na kuja sehemu ambapo uchumi uko juu."

Kwa sababu ya kusafiri katika nchi mbalimbali, Timothy ameshajifunza lugha ya Kireno, Kihispania, Kijerumani, mbali na kufahamu Kiswahili na Kiingereza. Ujuzi wa lugha hizo unamsaidia sana, hasa anapohudumia wateja waliofika kutoka nchi nyingine kuutembelea mji wa Cologne.

Timothy akiwa kwenye kibanda chake
Timothy akiwa kwenye kibanda chakePicha: DW

Mipango yake ya baadaye ni kuipanua biashara yake na ikiwezekana kuuza bidhaa zake nchini Ufaransa. Timothy, ambaye ana shahada ya elimu ya Masoko kutoka chuo kikuu cha kanisa la Methodist, Kenya Methodist Univerisity, pia ana mpango wa kujiendeleza kimasomo na kuchukua shahada ya uzamili huku Ujerumani. Lakini lipo jambo moja linalompa shida Mkenya huyo akiwa huku Ujerumani.

"Baridi imezidi, lakini nashukuru kwa sababu mwaka jana nilikuwa Uholanzi na baridi ilikuwa imezidi sana lakini mwaka huu afadhali kidogo," anaeleza.

Timothy atasherehekea sikukuu ya Christmas huku Ujerumani, pamoja na rafiki yake wa kike ambaye ni Mjerumani. Lakini utakapofika mwezi Januari mwaka kesho itabidi arejee Kenya ili kuendelea kuishughulikia biashara yake.

Mwandishi: Elizabeth Shoo

Mhariri: Josephat Charo