1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkondo mpya wa siasa ya Marekani kuelekea Mashariki ya kati

Oumilkher Hamidou18 Agosti 2009

Matumaini ya ulimwengu wa kiarabu na kiislam kwa rais Barack Obama wa marekani

https://p.dw.com/p/JDdW
Rais Barack Obama na mgeni wake rais Hosni Mubarak wa MisriPicha: AP

Miaka mitano imepita tangu rais Hosni Mubarak wa Misri alipofika kwa mara ya mwisho ziarani nchini Marekani.Hii leo anatazamiwa kukutana,tena kwa mara ya tatu,katika kipindi cha miezi mitatu na rais mpya wa Marekani Barack Obama.Wadadisi wanazungumzia juu ya enzi mpya katika uhusiano kati ya mataifa haya mawili,baada ya uhusiano huo kupooza katika enzi za utawala wa rais wa zamani wa Marekani George W. Bush.

"Nnafahari,ya kukuleteeni nia njema ya wananchi wa Marekani na salam za amani za jamii ya waislam katika nchi yangu...Asalam Aleykum...."

Barack Obama akishangiriwa hapo alipokua akihutubia mjini Cairo,mwishoni mwa mwezi June mwaka huu.Na hali hiyo haikutikani pekee nchini Misri,imezagaa katika nchi nyingi tuu.Wadadisi wengi wanazungumzia juu ya enzi mpya iliyochomoza katika uhusiano kati ya Marekani na Misri,na kati ya magharibi na "ulimwengu wa kiislam."

Wakaazi wa mjini Cairo wana maoni tofauti:

"Obama anazungumzia vizuri juu ya mipango yake ya kutaka kuleta mabadiliko katika eneo la Mashariki ya kati.Lakini sijui kama anasema kwa dhati au la.Hadi wakati huu hakuna kilichobadilika.Mzozo wa Mashariki ya kati hajafanikiwa bado kuupatia ufumbuzi.Na hata Irak,wamarekani bado hawajaondoka.Tunasikia maneno tuu,vitendo lakini hatuvioni."

Huyu mwengine anasema:

-"Mubarak hajatia mguu wake Marekani tangu miaka mitano iliyopita,kwasababu ya siasa za wamarekani kuelekea waarab.Hivi sasa siasa ya Marekani inafuata mkondo mpya.Ndio maana tunataraji ziara hii italeta tija."

Kusema kweli ziara hii ya sasa ya rais Hosni Mubnarak mjini Washington inaashiria mageuzi.Katika enzi za utawala wa mtangulizi wa Obama,George W. Bush,uhusiano pamoja na Misri ulipooza.Mara nyingi utawala wa zamani wa Marekani ulikua ukifungamanisha msaada wa fedha wa Marekani kwa Misri,unaofikia dola bilioni moja na nusu za kimarekani kwa mwaka,na utaratibu wa kuleta demokrasia na kuheshimu haki za binaadam.

Katika hotuba yake mjini Cairo,rais mpya wa Marekani Barack Obama alizungumzia pia kuhusu haki za binaadam lakini amekwepa kuilaumu moja kwa moja Misri.

Misri ni mmojawapo wa washirika muhimu wa Marekani katika eneo la mashariki ya kati.

Armut in Ägypten
Wauza mauwa katika barabara za mji mkuu wa Misri-CairoPicha: AP

Nchini Misri kwenyewe ziara ya rais Hosni Mubarak nchini Misri inafuatiliziwa kikamilifu,hasa kutokana na siasa ya ndani ya nchi hiyo.Kwasababu katika ujumbe anaofuatana nao rais Mubarak mjini Washington,anakutikana pia mwanawe wa kiume Gemel,anaeangaliwa kama mtu mwenye nafasi nzuri ya kumrithi mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 81.Kuna wanaohisi pengine Mubarak atataka kuitumia ziara hiyo ili kumjenga mwanawe katika jukwaa la kisiasa la Marekani.

Mwandishi:Ehl,Hans Michael/Kairo(SWR)/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:M.Abdul-Rahman