1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkopo kwa Ugiriki bado una vizingiti

14 Februari 2012

Ugiriki imesema bado inakabiliwa na changamoto kubwa kushawishi Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha Ulimwenguni, IMF, kuipatia mkopo mwingine wa kunusuru uchumi wake na kitisho cha kufilisika.

https://p.dw.com/p/1431K
Licha ya bunge la Ugiriki kupitisha mpango wa kupunguza bajeti, wakopeshaji bado wana mashaka
Licha ya bunge la Ugiriki kupitisha mpango wa kupunguza bajeti, wakopeshaji bado wana mashakaPicha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Ulaya umeitaka nchi hiyo kuwasilisha kwa maandishi, mkataba wa utayarifu wake kutekeleza masharti yote yanayoambatanishwa na mkopo mpya, na kuwasilisha mkataba huo ifikapo kesho Jumatano.

Licha ya bunge la Ugiriki kupitisha mpango wa serikali wa kukaza mkwiji baada ya mjadala mrefu Jumapili usiku, viongozi wa vyama viwili vinavyosalia katika serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu Lucas Papademos wametakiwa kujieleza kwa maandishi, na kufafanua kikamilifu jinsi watakavyotekeleza mpango huo wa kubana matumizi, baada ya uchaguzi wa Aprili mwaka huu.

Lakini sio mkataba huo wa maandishi tu, ambao unatakiwa na maafisa wanaositasita wa Umoja wa Ulaya; maafisa wa Ugiriki wametakiwa pia kueleza namna watakavyorekebisha nakisi ya euro milioni 325, inayoonekana katika mpango wao wa kuweka hazina ya euro bilioni 3.3 mwaka huu, na wanatakiwa kuwa na jibu kabla ya mkutano wa mawaziri wa fedha utakaofanyika kesho mjini Brussels.

Waziri Mkuu wa Ugiriki Lucas Papademos
Waziri Mkuu wa Ugiriki Lucas PapademosPicha: Reuters

Masharti hayo magumu yanapaswa kutekelezwa kabla Umoja wa Ulaya haujachukua uamuzi wa kuipatia Ugiriki mkopo mpya wa euro bilioni 130, kuondoa kitisho cha kufilisika kinachoukabili uchumi wa nchi hiyo.

Msemaji wa serikali ya Ugiriki Pantelis Kapsis amekiri kuwa nchi yake ina mlima mrefu wa kupanda. Amesema mkutano wa Jumatano utakuwa mgumu sana kwa Ugiriki, lakini akaongeza kuwa ana matumaini kwa sababu serikali yake ina utashi wa kisiasa kuendelea mbele.

Lakini matamshi ya ya Antonis Samaras, kiongozi wa chama cha kihafidhina cha New Democracy (ND) ambacho ni mshirika katika serikali ya sasa, hayaelekei kuondoa wasi wasi wa viongozi wa Ulaya. Kiongozi huyo aliwashurutisha wabunge wa chama chake kupiga kura ya ndio kwa mpango huo, lakini wakati huo huo akasema ni imani yake ni kwamba Ugiriki ingeachana na mpango huo mara tu itakapoepuka hatari ya kufilisika.

Mkuu wa chama cha ND Antonis Samaras
Mkuu wa chama cha ND Antonis SamarasPicha: picture-alliance/dpa

''Nawahimiza kupiga kura kuunga mkono mpango huu, kwa sababu napenda kuepusha balaa la kufilisika, na kurejesha utangamano, ili kesho tuwe na uwezo tena wa kujadiliana, na kuondoa hali hii ambayo tumelazimishwa kukubali'' . Alisema Samaras.

Wakati wanasiasa wakikabiliwa na kazi ngumu ya kutoa maelezo ya kuridhisha kwa wakopeshaji, wananchi wanaopinga hatua hizi mpya za kubana matumizi zaidi wamekuwa wakiandamana. Wakazi wa mji mkuu wa nchi hiyo, Athens wanahofia kuwa ghasia zilizofanyika Jumapili usiku zinaweza kuendelea kufikia vurugu za mwaka 2008, ambazo zilienea nchini kote baada ya polisi kumuua kijana mwenye umri wa miaka 15.

Mpango wa serikali kubana matumizi umewaghadhabisha wananchi
Mpango wa serikali kubana matumizi umewaghadhabisha wananchiPicha: dapd

Mwenyekiti wa shirikisho la wafanyabiashara nchini humo, Vassilis Korkidis alisema hali hiyo inaweza kujirudia hata pengine kuwa mbaya zaidi, kwa vile wananchi wana ghadhabu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/Reuters

Mhariri: Abdul-Rahman, Mohammed